6. Malezi

Namna ya kumfundisha mtoto kuongea

Kabla mtoto hajaanza kuzungumza kwa matamshi, huwasiliana kwa namna nyingine mbalimbali. Kwa hiyo lugha ya kwanza ya mtoto hutokea mara tu baada ya kuzaliwa, yaani kilio. Kisha hujifunza kufura, tabasamu, kucheka zote hizo zikiwa ni namna ya mtoto ya kuelezea mahitaji yake na hisia mbalimbali kama maumivu, njaa, kushiba, furaha nk. Mzazi bora ni yule anayejifunza ishara hizi na kujua namna ya kutafsiri mahitaji ya mwanawe.

Kisha, mara nyingi afikishapo miezi sita, mtoto huanza kujifunza kutamka kwa kutoa ‘sauti’ mbalimbali, ingawa hata hajui maana yake; na sauti hizi zinafanana kwa watoto duniani kote. Anaweza kusema, ‘da – da’, ‘ba – ba’ nk. Kisha mtoto huanza kutambua jina lake aitwapo, kuitambua lugha yake na pia huweza kutumia sauti kuonesha kuwa wanafuraha au wamechukia.

Miezi tisa, mtoto anaweza kuelewa baadhi ya maneno kama ‘bye’ au ‘acha,’ lakini afikishapo mwaka mmoja hadi miezi 18, anaweza akaanza kutamka maneno rahisi kama ‘baba’ ‘mama’ huku akielewa maana yake. Kipindi hicho pia anaweza kuanza kuelewa maagizo rahisi kama, ‘Kaa chini,’ ‘Simama’ ‘kunywa’ nk. Miaka miwili ataunganisha maneno na kutengeneza tungo rahisi, mfano ‘Mama bye.’

Katika kipindi chote hiki cha ukuaji wa mwanao, uwezo wake wa kutamka maneno na kisha kuongea utategemea sana kipawa alichobarikiwa na Mwenyezi Mungu cha uelewa lakini pia itategemea uwezo wako wewe mzazi katika kumsaidia kujifunza kuzungumza vizuri.

Soma ishara zake, ongea

Wataalamu wanasema, mtoto mwenye mwaka mmoja anaelewa maneno mengi kuliko anavyoweza kuzungumza. Kwa hiyo, mara nyingi atatumia ishara kusema. Tumia fursa hiyo kuzungumza naye. Akikupungia mkono, sema, ‘Bye’. Akionesha kitu, muulize, ‘Unataka hiki?’ Namna hii, mtoto kusema mahitaji. Si ajabu kesho anapotaka kitu akasema, ‘Taka.’ Mwanzo mzuri, kilichobaki ni kumrekebisha tu, aweze kusema, ‘Nataka’ badala ya taka.

Usimuigize makosa yake

Ni kosa kwa mzazi kumuigiza mtoto asemapo neno kwa makosa, badala yake rekebisha. Ni kwa kusikia matamshi sahihi ya neno ndiyo mtoto atajifunza kulitamka vema taratibu. Kurudia alichokosea inaweza kuwa kichekesho kwenu mnaosikiliza lakini hakumjengi mtoto. Hata hivyo, hii haina maana kuwa uwe unamkosoa, ila tu kulitaja neno analolikosea kulitamka, usirejee makosa yale. Sema kwa usahihi wake.

Anzisha mazungumzo

Mtoto hajifunzi kusema darasani bali katika maisha halisi. Lakini kadri mtoto anavyowasiliana, ndivyo anavyojifunza. Kwa hiyo, anzisha mazungumzo na mtoto mara kwa mara kila upatapo fursa kuhusu mambo mbalimbali yanayoendana na umri wake: majina ya vitu, vitendo mbalimbali na kadhalika.

Tumia nyimbo

Utafiti mbalimbali unaonesha kuwa watoto huzingatia zaidi wasikiapo nyimbo. Nyimbo huwafurahisha watoto kwani kwao ni kama mchezo. Nyimbo ikichanganywa na mafunzo, ni rahisi mtoto kushika na ndiyo nyimbo ni kisaidizi muhimu cha kusomesha watoto wa chekechea. Hivyo, hata wewe mzazi nyumbani unaweza kutumia nyimbo nzuri kumfundisha matamshi na maana ya maneno, hasa nyimbo inapoendana na ishara.

Elezea neno kwa vitendo

Kutamka neno huku ukionesha maana yake kwa vitendo husaidia mtoto kujifunza haraka. Mfano wa hii ni kama kusema ‘kunywa’ ‘kula’ ‘lala’ huku ukionesha ishara hiyo. Wakati huohuo, refusha voweli za neno kuonesha msisitizo wa tamko. Mfano, ‘baaaba’, ‘kuula’.

Mjumuishe na watoto wenzake

Panga mjumuiko wa michezo na watoto wenzake wa umri huo. Kuwa pamoja na wenzake kutampa fursa ya kucheza, kusikiliza, kujaribisa misamiati yake. Ukiwa pamoja nao kama mzazi unaweza kuratibu mambo yao na kuwasaidia kwenye mkwamo wa mawasiliano. Mmoja akimpatia mwenzake kitu, mwambie, ‘Ohh! Amekupa biskuti, sema asante.’

Muongezee misamiati

Mtoto wa miezi 18 mpaka miaka miwili huwa ameanza kutengeneza tungo rahisi za maneno mawili, kama, ‘Nataka maji.’ Tumia fursa hiyo kumuongezea misamiati zaidi juu ya ile aliyonayo aweze kutengeneza tungo nyingi za aina hii. Mfano, akisema ‘Mpira’ mwambie, ‘Mpira mkubwa’ na ‘Mpira mdogo.’ Namna hii mtoto ataongeza misamiati na kuboresha uwezo wake wa kuongea.

Mwache akuongoze

Iwapo mtoto ana hamu ya kulijua jambo, atataka kuyajua maneno yanayoendana na jambo hilo. Mchunguze mambo gani yanamvutia na zungumaza naye kuhusu mambo hayo. Mfano, anaweza kuvutiwa na wanyama wa nyumbani, kama paka, zungumza kuhusu paka – muonekano, rangi na chakula chake.

Badili ‘toni’ yako/ msomee hadithi

Watoto wanatakiwa kujifunza siyo tu matamshi na lugha lakini pia matumizi mabadiliko mbalimbali ya sauti na toni katika muktadha mbalimbali. Watoto wanajifunza kunong’oneza, kupaza sauti kuonesha hasira, kubembeleza, kuonesha hisia za upendo – na haya yote yanaendana mabadiliko ya sauti na toni ya mzungumzaji. Ukionesha mabadiliko haya, anaye anajifunza. Moja ya mbinu ya kumfundisha mtoto matumizi mbalimbali ya sauti na toni katika muktadha mbalimbali wa maongezi ni kumsomesa vitabu vya hadithi, hususan za wanyama: “Simba akasema kwa hasira, ‘Wewe nani?’” (sauti iakisi hasira): “Sungura akajibu kwa woga, huku akitetemeka, ‘Mimi ni mtumwa wako Sungura’” (sauti iakisi woga)

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close