6. Malezi

Mzazi, mfunze mwanao kwa kuwa mfano bora kwake

Maneno muhimu ambayo kila mzazi na mlezi anapaswa kuyasikia ni haya: “Yoyote anayetaka mwanawe awe na mwenendo fulani, basi lazima kwanza yeye mwenyewe mzazi awe na mwenendo huo.” Hii maana yake ni kuwa, hasa baba, mzazi anapaswa kuwa kielelezo cha tabia njema za kuigwa kwa mwanawe.

Ni muhimu mzazi aelewe kuwa, mtoto amefungamana naye. Yeye ni mtu wa kwanza ambaye mtoto anayemuangalia na kumuiga. Waingereza wanasema ni ‘role model’ wa kwanza. Wewe pia ni kiongozi wake na kigezo chake cha tabia.

Ukiwa kama kiongozi, elewa kuwa utaulizwa mbele ya Allah kwa dhamana uliyopewa ya kuchunga familia, kama alivyosema Mtume:

“Kila mmoja wenu ni mchungaji na ataulizwa kwa alichokichunga… Mwanaume ni mchunga wa familia yake na anawajika kwao…”

Kigezo chema

Kuhusu kuwa mzazi kuwa kigezo cha tabia, hujawahi kumsikia mtoto kakutwa anafanya jambo fulani baya halafu akajitetea kwa kusema, ‘Mbona baba/mama pia kafanya.’? Huo ni ushahidi tosha kuwa mzazi ni kipimo.

Binafsi, nimewahi kuona watoto wanamuiga mzazi anayebeua mbele ya watu kwa sauti. Nimeona watoto wachonganishi, wanaosonya, wanaotukana, wasiochunga adabu wakati wa kula na wanaotumia lugha za viapo vya uongo, kejeli, mipasho yote kwa sababu wameona wazazi wanafanya hivyo, nao wanaiga.

Kwa maana hiyo, ni muhimu uwe kiigezo chema kwa wanao katika kila nyanja kitabia, kiutekelezaji wa ibada, katika mafungamano na mahusiano na watu nk. Kwa maana nyingine, kuwa kigezo chema kwa maana pana ya neno lenyewe, yaani kwenye kila kipengele cha maisha.

Wengi wetu, kama wazazi wa Kiislamu tunapenda sana watoto wetu wawe wachamungu, lakini sisi wenyewe hatuutafuti huo uchamungu. Sasa watoto waige wapi huo uchamungu, jambo ambalo namna bora ya usomeshaji wake ni kwa vitendo? Tunapotamani wenetu wawe wachamungu, tujue kuwa sisi ndiyo walimu wao wa huo uchamungu, walau katika hatua za awali za maisha ya watoto wetu.

Ukiacha utekelezaji wa ibada, sehemu nyingine kubwa ya uchamungu ipo katika tabia na mienendo. Hivyo basi, wakati tunahimiza watoto waende msikitini, pia tuwaoneshe upande huu mwingine wa uchamungu yaani tabia njema za Kiislamu kama ukarimu, upole, ukweli, uaminifu, subira na kadhalika.

Ni muhimu mzazi aanze kujenga tabia nzuri za Kiislamu kwa mtoto kwa kuanza kuonesha tabia hizo nyumbani kwani hisani huanza nyumbani. Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema katika hadith iliyopokewa na Tirmidh:

“Mbora miongoni mwenu ni yule aliye mbora kwa familia yake; na mimi ni mbora kati yenu kwa kwa familia yangu.”

Tumia muda kukaa na watoto

Ili uweze kuleta ushawishi wa kuwajenga watoto kitabia njema kupitia kukuiga wewe, ni muhimu sana upate muda wa kukaa nao. Hakuna kisingizio kinachokubalika cha mzazi kutotumia muda wako kukaa na wanawe ili apate kuwalea na kuwaongoza. Hii ni haki ya mtoto kwa mzazi, lakini pia ni jukumu lako ulilopewa na Mwenyezi Mungu, kama mchungaji wa familia.

Mzazi kuwa bize hadi kukosa muda wa kukaa na wanawe ni kosa ambalo anaweza kulijutia kwani anaacha ombwe la ulezi ambalo litazibwa na watu wengine ambao hatuna hakika kama watawaongoza watoto wetu katika wema.

Pia, kuna uwezekano mkubwa kwa watoto waliotelekezwa kukosa ukaribu na wazazi waliowatelekeza hapo baadae, kiasi kwamba mzazi, akifikisha umri mkubwa, naye atahisi wanawe hawamjali. Kutelekeza watoto siyo tu kutowahudumia, bali hata kuwa nao mbali, bila kujali unatoa mapesa kiasi gani. Kwa hiyo muda, muda, muda. Tenga muda wa kukaa na watoto wajifunze kutoka kwako.

Kuwa rafiki kwao

Kukaa na watoto pekee haitoshelezi bali pia uwe unafikika kihisia. Kuwa mpole kwao, isipokuwa inapobidi ukali. Ukali wa muda wote na kuwakaripia watoto kila mara, kunaweza kuwafanya watoto washindwe kukaa na wewe kwa uhuru, bila hofu, na kujifunza kutoka kwako.

Kumbuka, tumesema, ‘Mzazi awe vile anavyotaka wanawe wawe’, lakini mzazi mkali kupitiliza anajenga kizuizi cha maingiliano na watoto na hivyo kuwanyima fursa ya kumkaribia, kumzoea na kuiga tabia njema. Kwa upande mwingine, mzazi ajiulize, je tabia hii ya ukali ndiyo ambayo nataka watoto waige?

Kwa nyongeza tu, waataalamu wengi wa malezi wanasema, ukali haujengi katika suala la malezi, bali unaweza kuleta matokeo hasi. Mara nyingi tabia ya mtoto inayojengwa kwa kukaripia na kitisho cha adhabu hudumu tu mpaka kitisho cha adhabu kikiondoka. Kwa upande mwingine, ni mawaidha mema, yanayotolewa kwa upole na hoja za kimantiki ndiyo zinaweza kurekebisha tabia ya mtoto.

Mbinu tofauti

Tumesema, mzazi ana jukumu kubwa katika kumjenga mtoto kitabia kwa sababu yeye ni kiongozi wa kwanza wa mtoto. Yeye pia ni kiigizo chake na kipimo cha baya na zuri. Tumesema pia kuwa ili mtoto aige mema kwanza lazima mzazi amuoneshe hizo tabia njema, lazima mzazi atumie muda wake kukaa nao na awe anafikika (siyo mkali kupitiliza).

Haya yakitimia, mzazi anachohitaji ziada ni kutumia mbinu ndogondogo za kufanya mambo kwa makusudi ili kuwafundisha watoto wema. Mfano wa hayo ni kuwasomea hadith za watu wema na kuambatana nao sehemu ambazo anaamini watajifunza mambo mazuri, mfano kwenye mikutano ya waja wema ua kwenye kutoa sadaka.

Sambamba na jitihada zote hizi, muombe Mwenyezi Mungu akuongoze na aiongoze familia yako kwani kila jambo ili lifanikiwe linahitaji kwanza msaada wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close