6. Malezi

Mwana umleavyo ndivyo akuavyo

Mara nyingi tunashangaa kuhusu tabia za watu na kuulizana: “Mbona huyu yuko hivi, ana tabia hizi na zile?” “Mbona yule ana mambo haya?” Au wakati mwingine tunasifia: “MaashaAllah, fulani amejaaliwa tabia njema, anapendwa na kila mtu!”

Je, unadhani kitu gani huchangia tabia ya mtu ikawa hivi au vile? Mathalan, jambo gani linapelekea baadhi ya watu wakawa wanajiamini sana na wengine hawajiamini na waoga mbele za watu? Hawa ni wapole wengine ni wakorofi na watovu wa adabu, baadhi unafurahia mazungumzo yao lakini wengine hawaongei sentensi bila kuchanganya na matusi, hawa waelewa wengine ni wabishi, wasioambilika?

Kwa nini kuna watu wanakuwa wakarimu, wachangamfu na wapenda watu lakini wengine ni wachoyo, bahili na wana roho mbaya? Jambo gani hufanya mtu awe na tabia fulani na mwingine tabia nyingine kinyume na tofauti? Kwa nini tabia zinatofautiana?

 Haya ni maswali yaliyojadiliwa na kufanyiwa utafiti na wanasayansi kwa muda mrefu. Na katika jambo hili kuna mitazamo miwili mikubwa.

Tabia zinarithiwa au ni athari ya malezi na mazingira?

Mjadala mkubwa uliopo ni je, tabia zinatokana na vinasaba vya kurithi au zinachangiwa na malezi na mazingira ambayo mtu alikulia? Wanasayansi wengi wamekubaliana kuwa mambo yote hayo mawili yanachangia katika kujenga tabia ya mtu.

Bahati mbaya ni kuwa, hatuna udhibiti juu ya suala la vinasaba unavyorithi kwani ni Mwenyezi Mungu anayeamua uzaliwe na wazazi gani na wapi. Hata hivyo, tuna kiasi fulani cha udhibiti juu ya malezi na mazingira tunayolelea watoto wetu, hususan katika nafasi yetu kama wazazi na walezi.

Nasema, tuna kiasi fulani cha udhibiti kwa sababu mazingira tunayokulia yanategemea pia hali zetu za kiuchumi. Licha ya kuwa, wengi tungetamani kuishi maeneo mazuri – mfano kwa jiji la Dar es Salaam sehemu kama Masaki, Oysterbay na Mbezi Beach; lakini tunafanyaje kama uwezo wetu unaturuhusu tu kuishi Mbagala, Tandika, Manzese au Tandale na si zaidi ya hapo?

Hata ukibahatika kuishi na familia yako katika maeneo mazuri yanayoonekana kuwa na ustaarabu, bado pia huna udhibiti wa asilimia 100 katika malezi ya mtoto. Kwa mfano, huwezi kumfuata mwanao kila aendapo. Kadri anavyokua, atahitaji uhuru zaidi. Hivyo, mwanao atakuwa anakutana na marafiki ambao wanaweza wakawa wazuri au wabaya, na wakawa na ushawishi kwake kwa namna moja au nyingine.

Lakini yote kwa yote, tunasema, kwa kiasi fulani, aina ya malezi ina athari katika makuzi ya watoto na watoto wake. Hivyo basi, bila kujali hali ya eneo unaloishi, yapo mambo yaliyo ndani ya uwezo wako unayoweza kuyafanya ya kimalezi ili kumfundisha na kumjenga mtoto kitabia ili hatimaye afuate uelekeo unaofaa wa maisha.

Muhimu zaidi, sambamba na jitihada unazoweza kufanya, ni muhimu kumuomba Mwenyezi Mungu, akuongoze na akusaidie kuongoza vizazi vyako.

Sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka akuongoze na vizazi vyako, jitihada zako katika kumfundisha na kumuongoza mtoto ni muhimu sana. Walisema wasemaji, “Mwenye kujitahidi, hupata.” Pia, Waswahili walisema, mtoto umleavyo hakika ndivyo akuavyo.

Kwa vyovyote, kama mzazi, huwezi kupanda bangi, halafu utegemee kuvuna mchicha; na kadhalika kinyume chake – labda Mwenyezi Mungu akadirie vinginevyo.

Tunachosema, kwa mfano, ni kuwa mtoto aliyekulia katika mazingira ya kuzodolewa, kuabishwa, kufokewa na kupigwa si ajabu akija kuwa mkimya mnyonge, asiyejiamini na hata akakosa uthubutu. Mtoto atajiamini vipi iwapo hakupewa nafasi ya kujieleza na muda wote amekuwa na hofu ya kufokewa kwa kukosea?

Kuna wakina mama wanawafundisha watoto wao roho mbaya bila kujua au kwa kujua. Wazazi wa aina hii hutumia muda wao mwingi kuwasema watu kwa ubaya kwa sababu tu wana mafanikio! Tena, wanaweza wasiishia kusema tu, bali hata kuharibia watu wengine vitu vyao ili tu wawakomoe! Jambo la kusikitisha ni kuwa mtoto naye aghlabu hutumika katika vita hiyo ya kuonesha roho mbaya.

 Katika mfano mwingine chanya, mtoto ambaye amelelewa katika mazingira ya kupendwa na kusifiwa na wazazi na jamii inayomzunguka, basi naye atajifunza kuwapenda na kuwakubali wengine, na kuwasifia wafanyapo mazuri.

Misingi ya malezi ya Kiislamu

Katika suala hili la malezi, ninachoweza kushauri ni kufuata misingi ya malezi ya Kiislamu. Misingi hiyo ni pamoja na kuelewa kuwa, watoto huzaliwa wakiwa na mioyo safi. Ili watoto wapate uongofu, wazazi wanapaswa kuwaelekeza yaliyo mema, kujenga mazingira mazuri ya nyumbani na pia wenyewe kuwa mfano bora.

Jambo jingine lililohimizwa sana katika Uislamu ni kuwaonea huruma watoto na kuishi nao kwa upole na wema; bila kusahau kuwaombea dua, kama ambavyo wema waliotangulia wakiwemo Mitume walivyofanya kwa ushahidi wa Qur’an Tukufu na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Misingi mingine ya malezi ya Kiislamu ni kujenga ukaribu na watoto lakini wakati huohuo pia kuzingatia mipaka ya kimaadili. Elimu nayo ni muhimu, hususan ile ya muongozo wa dini. Ni elimu hii ndiyo inayompa mtoto ueelekeo sahihi wa maisha na kumkumbusha lengo la kuumbwa kwake, yaani kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Nidhamu ni jambo jingine muhimu. Kumuelekeza mtoto kusali afikishapo miaka saba na kumuadhibu afikishapo miaka 10 iwapo hatasali, kama alivyoagiza Mtume, ni sehemu muhimu ya nidhamu. Nina hakika, ukifuata misingi hiyo muhimu ya Kiislamu, utakuwa tayari umefanya wajibu wako wa malezi na inshaAllah atakuwa mtoto mwema. Mwenyezi Mungu atuongoze kwa hili na mengineyo ili tupate radhi zake na hatimaye tuingie katika Pepo yake tukufu.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close