6. Malezi

Muongozo wa Uislamu kwa mjamzito

Baada ya wawili kufunga ndoa kinachotarajiwa ni kupata watoto. Watoto ndio mazao ya ndoa. Kupata watoto ni moja ya neema kubwa alizotunukiwa mwanadamu hapa ulimwenguni.

Waswahili husema: “Azaliwaye naye huzaa,” lakini ukweli ni kwamba, sio kila mtoto huwa neema kwa wazazi wake. Mtoto anaweza kuwa ni chanzo cha mabalaa, aibu na mitihani kwa wazazi, familia, mtaani na hata kwa jamii anayoishi nayo.

Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya wazazi wakikumbana na misukosuko kwa sababu ya vitimbi vya watoto wao. Watoto wao wamekuwa wakiwaendesha mbio wazazi na kuwafanya wajute na kutamani bora wasingelipewa kizazi kabisa!

Mapungufu katika kuilea mimba

Inaaminika kwamba binadamu ana maeneo makuu matatu: mwili, roho na akili. Kila eneo katika hayo matatu niliyoyataja lina mahitaji yake. Na ili binadamu awe kamili na wa maana, lazima kila eneo lipewe mahitaji yake ipasavyo. Kwa bahati mbaya sana wadau wengi katika vitabu, makala, semina na makongamano yao, hutoa mafunzo ya afya ya mama waja wazito (afya ya uzazi) upande wa mwili na akili tu, na ni nadra kusikia ikitolewa miongozo ya kujilea na kuzilea mimba kiroho.

Hivyo, makala hii ni kwa kadri inavyowezekana, kutoa muongozo wa kiroho ambao ndio msingi wa ustawi wa mwili na akili. Katika hadithi tunajifunza kwamba, roho/ moyo umefananishwa na kinyama kidogo mwilini, kikitengenea, mwili mzima hutengenea, na kikiharibika mwili nao huharibika.

Makala ina lengo la kufafanua taratibu wanazotakiwa kuzifuata akina mama wanapokuwa katika kipindi cha ujauzito ili familia ipate kizazi bora na salama na jamii iwe na raia wema walioleleka vyema katika hali zote: kimwili, kiroho na kiakili.

Makala hii haijihusishi sana na kutoa miongozo ya malezi ya kimwili kwani tunaamini kwamba wakina mama wanapata taaluma hiyo wanapokuwa kliniki kwa wataalamu wetu.

Utukufu wa mama

Licha ya kwamba mwanamke kubeba uja uzito, kuzaa na kulea ni katika maumbile aliyojaaliwa na Allah; kwa mtazamo wa Uislamu, iwapo atayafanya hayo kwa dhati, na kwa ikhlasi na kwa kufuata mafundisho ya dini, huzingatiwa kuwa ni ibada, na ni matendo yanayomtukuza sana.

Mwanamke hutukuka hapa duniani kwa kupata watoto wema atakaowafurahia na kutuuliza moyo wake, na hutukuka huko akhera pale atakapokuwa miongoni mwa wanawake bora na pale familia yake itakapoendelea kuwa pamoja.

Qur’an, Sunna na utukufu wa mama

Katika Qur’an Tukufu na Sunna, maumbile hayo yametajwa. Kumetajwa tendo la ndoa kama sababu ya kupata ujauzito, kutunga mimba, kujifungua, kunyonyesha na kumlea mtoto mpaka kufikia umri wa kujitegemea.

Na kumetajwa usumbufu mkubwa mwanamke anaokutana nao katika kuyafanya hayo. Kwamba, usumbufu huo ni jambo ambalo humpatia hadhi, fakhari na heshima kubwa mbele ya walimwengu. Jambo hili la uzito na usumbufu wa uzazi limepelekea kuja amri nzito ya kuwashukuru wazazi baada ya kumshukuru Allah, kuwatii na kuwafanyia wema, hususan akina mama.

Allah Aliyetukuka anasema: “Na tumemuusia mwanadamu (kuwafanyia) wazazi wake ihsani, mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha) na kumuachisha katika miaka miwili, ya kwamba, nishukuru mimi na wazazi wako. Marejeo yenu ni kwangu.” [Qur’an, 31: 14].

Kwa hiyo mashaka, maradhi na madhila yanayomkuta mjamzito, shida wakati wa kujifungua, kumnyonyesha pamoja na usumbufu wa malezi ya awali kwa mwanawe – yote haya humpatia thawabu iwapo masharti yatazingatiwa.

Si hayo tu, bali ikitokezea kufa wakati wa kujifungua atakufa shahidi kwa mujibu wa mafunzo ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Katika hadithi iliyosimuliwa na kutoka Jabir (Allah amridhie), Mtume aliwataja mashahidi saba ambao wanakuwa na kibali cha kuingilia Peponi alisema: “ …na mwanamke atakayekufa uzazi ni Shahidi.” [Abu Daud na Ibn Majah].

Uzoefu unatuonesha kwamba juhudi za mama kwa mtoto wake haziishii katika ujauzito, kujifungua na kumnyonyesha tu, lakini huendelea kuwa karibu naye muda wote wa uhai wake.

Hivi ni kusema kwamba walimwengu wote hulelewa na mwanamke zaidi kuliko na mwanamume. Mathalan , kijana akiondoka katika uangalizi wa mama huenda katika uangalizi wa mwanamke mwengine naye ni mke.

Kwa msingi huo, mtu mmoja alipokwenda kumuuliza Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni mtu gani amfanye kuwa rafiki yake zaidi, alimwambia: “Mama yako.” Yule mtu akauliza: “Kisha nani?” Akamwambia: “Mama yako.” Akauliza tena: “Kisha nani?” Akasema: “Kisha mama yako.” Akauliza tena: “Kisha nani?” Akasema: “Kisha baba yako.” [Bukhari].

Athari za mama kwa mwanawe

Kutokana na maelezo ya hapo juu, tunajifunza kwamba mama ana uwezo mkubwa wa kumuathiri mtoto wake katika hatua zote anazozipitia. Athari hizo zinaweza kuwa njema au mbaya. Zinaweza kuwa za kibaoloji, kiimani na kitabia.

Ona: anakaa tumboni mwake miezi tisa. Baada ya kujifungua, chakula chake cha awali na kinachodumu kwa miaka miwili (kwa watimizao muda wa kunyonyesha) hutoka mwilini mwake.

Katika kipindi chote hiki, mikono na mapaja yake inakuwa ndio kitanda chake, huku ujoto-ujoto wa kifua, mbavu na mgongo wake humpa faraja na utulivu. Na kwa hiyo, mtu wa kwanza kumjua na kumzoea kupitia harufu na sura yake ni mama yake.

Zaidi ya hayo, mama humsimamia mwanawe usafi wa nguo na malazi yake na humuandalia chakula wakati tayari ameshakuwa na kuanza kusoma. Basi mtoto pia huyazowea na kuiga maneno, vitendo na tabia za mama yake kwanza ama zaidi kuliko mtu mwengine.

Haya tunayaeleza kwa kuwa tunaamini kuwa mazingira ya mama humuathiri mtoto kiafya akiwa bado yu tumboni, hivyo inafanya ashauriwe kubadili baadhi ya mienendo aliyoizowea.

Kwa mfano, mjamzito anaweza kukatazwa kutumia baadhi ya vyakula na kusisitizwa kutumia vyengine ili kutunza afya yake na ya mtoto wake.

Kama ukweli ndio huo, mjamzito Muislamu anahitaji mafunzo ya lazima ya jinsi ya kujilea yeye na kuilea mimba yake kiimani ili amuachie mtoto wake athari njema akiwa bado hajapata hata upepo wa dunia

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close