6. Malezi

Msingi wa malezi bora ni huruma, si ukali, si ukatili

Mtoto anapotendewa ukatili na wazazi wake kwa aidha kukaripiwa bila sababu, kutwezwa, kubezwa, kipigo kikali au njia nyingine zisizo sahihi za kimalezi hupelekea athari kwenye tabia, nyendo na vitendo ya kijana huyo; na athari hizo huweza kudumu katika maisha yake yote.

Miongoni mwa athari za njia hizo mbaya za malezi ambapo mzazi anaamiliana na watoto kwa hasira, ukatili, chuki, matusi, ngumi na kila aina ya uonevu ni mtoto kuwa muoga, kunyong’onyea na hali ya kutojiamini.

Si hayo tu, kwa kule kukosa kujiamini, mtoto pia anaweza kuwa tegemezi maisha yake yote. Anaweza kushindwa kufikiri sawasawa au kukosa ubunifu na vilevile kushindwa kutoa maoni na kushiriki majadiliano. Pia, anweza kupata msongo wa mawazo, aibu na mzio (allergy). Athari nyingine zinazoweza kutokea ni pamoja na mtoto kukosa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujihisi udhaifu na kukosa ufanisi.

Uasi, utukutu

Katika athari zote hizo za malezi yasiyofaa, jambo baya zaidi linaloweza kutokea ni mtoto kujenga tabia ya utukutu, uasi na hivyo kuwa mharibifu wa vitu vya wengine kwa sababu ya kule kuhisi kuonelewa, hali ya kukata tamaa, chuki, kisasi na kadhalika.

Kwa wazazi wenye malezi ya aina hiyo – wanaotumia njia hasi za malezi huvuna matunda machungu ya malezi yao ya hovyo. Mtoto anaweza kutamani kutoroka nyumbani ili kujikwamua na miamala ya kikatili na kimanyanyaso inayomsononesha. Ama mtoto anaweza kutamani kuua wazazi wake au hata kujiua. Ama mtoto anaweza hata kuishia kwenye magenge ya kihalifu ya umalaya, ukahaba, utumiaji wa dawa za kulevya na maisha mengine ya aibu na ajabu.

Mfano hai

Na hizi si hadith za kutunga bali vipo visa vilivyohusisha watu wema vinavyothibitisha kuwa watoto wanaweza kuasi kwa sababu wazazi walishindwa kuwalea vema. Mfano ni kisa maarufu cha kilichomuhusisha Khalifa wa PIili Muongofu, Umar bin Khattwab (Allah amridhie).

Katika kisa hicho, mtu mmoja alimwendea kumshitakia uasi wa mtoto wake. Umar alipomuita yule mtoto ili kumuonya, alijitetea kwa kuhoji:

“Ewe Amir wa Waumini, hivi mtoto hana haki, kwa baba yake?” Umar akasema: “Anazo.” Akamuuliza: “Ni zipi?” Akasema: “Amchagulie mama mwema, ampe jina zuri, na amfundishe kitabu (Qur’an).”

Basi yule mtoto akasema:

“Ewe Amir wa Waumini, mzazi wangu hajanifanyia lolote kati ya hayo… (akaeleza kwa nini).” Umar akageuka na kumtaza yule mtu na kumwambia: “Hivi umekuja kushitakia uasi wa mwanao? Wewe ndiyo uliyeanza kumfanyia uasi kabla ya yeye hajakuasi; na umemfanyia ubaya kabla yeye hajakufanyia mabaya.”

Umar (Allah amridhie) alimtwika yule mzazi dhima ya kumfanyia uasi mwanawe, na kusababisha mwanawe naye awe mkorofi kwa sababu mzazi hakufuata njia bora na sahihi ya malezi ya mtoto tokea awali.

Mafunzo ya Uislamu

Mafunzo matukufu ya Uislamu yanamtaka kila mwenye dhamana ya malezi kubeba jukumu la kutoa miongozo na malezi. Miongoni mwa hao ni baba na mama. Katika miongozo hiyo, Uislamu unawahimiza wazazi waongozwe na msingi ya heshima, huruma na busara ili watoto nao wakue wakiwa na unyoofu wa tabia na ubinadamu.

Mkuu wa Wakufunzi, Mtume Muhammad, (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Hakika Mwenyezi Mungu ana huruma na hupenda huruma, na hulipa penye huruma (malipo) asiyoyalipa kwenye ukatili, na (hapo kwenye huruma) hutoa malipo asiyoyatoa penginepo.” [Bukhari na Muslim].

Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah ana amani zimshukie) ambaye ndiye Kiigizo Chetu, amesifiwa na Mwenyezi Mungu kwa sifa ya huruma na upole, pale Allah aliposema:

“Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndiyo umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukishakata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaomtegemea.” [Qur’an, 3:159].

Kwa mujibu wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), akiwapenda watu wa nyumba fulani, huwaingizia upole baina yao.

Amesema Mtume: “Kwa hakika Mwenyezi Mungu anapowatakia kheri watu wa nyumba, huingizia upole baina yao. Na laiti upole ungekuwa ni kiumbe (kinacho onekana) pasingekuwa na kiumbe kizuri kuliko upole. Na laiti ukatili ungekuwa ni kiumbe (kinachoonekana); basi watu wasingeshuhudia kiumbe kibaya kuliko hicho.” [Ahmad na Baihaqiy].

Basi kwa nukuu hizo nilizozitoa, naomba nitoe rai kwa wazazi, kwamba, tuongeze kupanda mbegu halisi ya huruma kwenye nafsi za watoto ili wawe wema kwetu. Pia, wazazi tufuate mafunzo ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye inatajwa katika hadith kuwa, ilikuwa akimuona bintiye Fatima (Allah amridhie) yuaja alikuwa akiinuka alipoketi na kuushika mkono wake na kuubusu. Kuna wakati bedui mmoja alimjia na kumwambia:

“Hivi nyinyi mnawabusu watoto wenu!? sisi hatuwabusu.” Mtume (rehema za Allah na amani akamwambia) akamwambia: “Hivi naweza kuambulia lolote ikiwa Mwenyezi Mungu ameondosha huruma moyoni mwako.”

Pia, tukumbuke neno la Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa Al-aqra’a bin Habis aliyeruzukiwa watoto 10 lakini hakuwahi kumbusu hata mtoto wake mmoja. Mtume alimwambia:

“Asiyehurumia (naye) hapaswi kuhurumiwa.” [Bukhari na Muslim].

Na hivi ndivyo Uislamu unavyotuelekeza na kututaka tuwe na huruma na upole kwa watoto wetu katika kuwapa mafunzo na miongozo ili wasije kuwa watukutu, wenye tabia mbaya na kutoroka nyumbani na kuwa mbali na wazazi.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close