6. Malezi

Mambo yaletayo ufanisi katika malezi ya familia za Kiislamu

Ndoa ni mahusiano ya kina na yenye mizizi mirefu na ni ahadi nzito. Mwenyezi Mungu anasema:

“Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao.” [Qur’an, 2:187].

Kila kitu hufanyika kwa malengo maalumu. Hivyo basi, lengo la maisha ya ndoa ni kupata utulivu. Katika Uislamu, ndoa hufungwa ili idumu na ili mke na mume wapate amani na utulivu katika maisha yao, waburudike, na wazae watoto wema.

Kama ndoa ni jambo zito, si vema basi mwanandoa kufanya uharibifu au kutenda upuuzi. Mwenyezi Mungu anasema:

“Na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo nzito?” [Qur’an 4: 21].

Kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kuipa mafanikio familia ya Kiislamu. Makala hii inalenga kujadili mambo hayo.

Yanayoweza kuipa mafanikio familia ya Kiislamu

Kuchagua mke kuzingatie misingi ya dini

Mwanaume anatakiwa atafute mke mwenye dini. Ni dini pekee ndiyo inaweza kumpatia Muislamu maisha yaliyojaa upendo na masikilizano.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.” [Qur’an 24:32].

Naye Bwana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Chagua mwanamke mwenye dini utabarikiwa.” [Bukhari na Muslim].

Kwa upande mwingine, walii/ mzazi wa mwanamke pia anawajibika kumchagulia mwanawe mume mwenye dini na maadili mazuri, kama alivyoagiza Bwana Mtume kwa kauli yake (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Anapowajieni mtu mnayeiridhia dini na tabia yake, basi muozesheni, msipomuozesha, mtasababisha uharibifu na ufisadi mkubwa.” [Tirmidhi].

Waume kuishi na wake zao kwa wema

Kuishi kwa wema hakuwezi kufikiwa kama kila mmoja kati ya wanandoa hajui haki na wajibu wake kwa mwenzake. Mwenyezi Mungu anasema:

“Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao.” [Qur’an 2: 228], na neno la Mwenyezi Mungu “Na kaeni nao kwa wema.” [Qur’an 4:19].

Pia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Zindukeni! Ninyi mna haki kwa wake zenu, na wake zenu wana haki kwenu. Haki yenu kwa wake zenu ni kutoketi kwenye godoro lenu msiyemridhia, na kutomruhusu kuingia ndani ya nyumba zenu mnaowachukia. Na zindukeni pia, na haki za wanawake kwenu, ni kuwatendea wema katika chakula na mavazi.” [Ibn Majah].

Na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa na huruma, uvumilivu, na muamala mzuri mno kwa wakeze. Kuna nyakati yalikuja maudhi kutoka kwa baadhi ya wakeze, kama ilivyo kwa wanawake wengine wowote. Lakini, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) hakuwa akikasirika wala kuyapatiliza. Alipuuza na kusamehe.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu mwenye imani kamili ni yule mwenye tabia njema zaidi; na mwema zaidi kwenu ni yule aliye mwema kwa wakeze.” Na Mtume amesema: “Ninawausieni kuwatendea wema wanawake.” [Bukhari na Muslim].

Muamala mzuri

Muamala mzuri katika ndoa ni chanzo cha kupata mafanikio, upendo, na kuhurumiana kati ya wanandoa. Pia, muamala mwema ni chanzo cha kupata watoto wema na kuimarisha uhusiano wa wanandoa. Kuhurumia n a kun- aipa famil- ia utulivu na mafanikio.

Kati- ka mazingira haya ya ukarimu na muamala mzuri, furaha huingia kwenye nyumba na mtu kupata amani na utulivu wa akili kwa kuwa ana mke mwema anayemsaidia katika dini yake, anayemlelea watoto wake malezi ya kiimani. Hali hii inaleta baraka kwenye mali na watoto.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na anayemcha Mwenyezi Mungu, humtengezea njia ya kutokea. Na humruzuku pasipo kutazamia.” [Qur’an, 65:2-3].

Lengo kuu la wanandoa iwe maisha ya Akhera

Maisha ya dunia kwa wanandoa yawe ni kama njia na daraja kuelekea katika kumtii Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie). Hili ndiyo hasa lengo la kuumbwa kwetu hapa duniani na ndiyo njia ya kupata raha na furaha.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na utafute, kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu, makazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la Dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.” [Qur’an, 28:77].

Wanandoa wawe kiigizo chema kwa watoto wao

Wanandoa wanatakiwa wawe ruwaza njema kwa watoto, kiibada, kimaadili, na kimiamala kwani watoto huiga nyenendo za wazazi wao, na hasa wanapokuwa wadogo.

Wazazi wanatakiwa wawatunze vema watoto wao, na wafuatilie nyendo zao, wajue watoto wao wanavyoutumia wakati wao. Pia wazazi wawajue marafiki wa watoto wao kwani mtu hufuata dini ya rafiki yake. Pia, ni jukumu la wazazi kuwanasihi watoto wao na kuwafunza yenye tija kwao.

Vilevile, ni muhimu wazazi wasiwe bize na kazi/ misafara inakayowapelekea kuwatelekeza watoto wao. Wazazi pia waelewe kuwa watoto ni dhamana zilizo kwenye shingo zao; hivyo wazazi waelewe kuwa wataulizwa Siku ya Kiyama kuhusu walivyowalea watoto. Watoto ni mali yenye thamani kubwa, na iwapo itapotea tutakuwa tumepoteza kitu kikubwa.

Kuwahurumia watoto hata wakikosea

Huruma ndiyo msingi wa malezi, hivyo ukali usitumiwe isipokuwa katika hali ya dharura. Kheri na baraka ipo kwenye upole, kama ilivyokuja katika Sahihi Muslim kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimwambia Bi Aisha (Allah amridhie):

“Mwenyezi Mungu ni mpole, na anapenda upole, na hulipa thawabu katika upole, thawabu asizozilipa kwenye ukatili.”

Familia ina mchango mkubwa katika kudumisha usalama na amani katika taifa. Pia, hakuna apingae mchango wa familia katika kutatua tatizo la mmomonyoko wa kimaadili na kifikra, hasa ule unaowahusu watoto. Mchango wa kwanza wa familia katika kudhibiti mmomonyoko wa kifikra ni wazazi kuwa na fikra sahihi, kiakili na kimaudhui.

Itikadi sahihi

Aidha, wazazi wanatakiwa wawalee watoto wao kwa fikra sahihi na itikadi safi isiyo na mkengeuko na kufurutu desturi. Mtume wetu (rehema za Allah na amani zimshukie) ametutaka tuwaelekeze watoto katika njia sahihi.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimwambia Ibn Abbas (Allah amridhie) angali kijana mwenye umri mdogo:

“Ewe kijana! Mimi ninakufundisha maneno, ‘Mhifadhi Mwenyezi Mungu, naye atakuhifadhi. Mhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta mbele yako. Ukiomba muombe Mwenyezi Mungu, na ukitaka msaada mtake msaada Mwenyezi Mungu.”

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close