6. Malezi

Mama baada ya kujifungua

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alijibu: “Mama” mara tatu, kisha ndio akasema baba. Mama anastahili kutendewa wema zaidi na wanawe kwa sababu ya jukumu zito alilopewa la uzazi na ulezi. Hakika Pepo, kama ilivyonukuliwa katika Hadithi, iko chini ya nyayo za mama zetu.

Ni mtu wa ajabu ambaye humuudhi mama yake hadi mama afikie kiwango cha kumlaani kwa sababu katika hali ya kawaida, mapenzi ya mama kwa mwanawe ni makubwa mno kiasi kwamba hata mtoto akimuudhi, mama huwa tayari kumsamehe na kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu. Mama hamfukuzi mwanawe kwa sababu yu mkorofi, anaumwa, hana pesa katika hali hizo za udhaifu usikute mapenzi ndio huzidi!

Tulisema, jukumu la umama linaanzia pale mwanamke anapogundua kuwa yu mjamzito. Kuanzia hapo mama anawajibika kuzingatia ustawi wa mtoto kwa kila afanyacho kwa sababu maisha ya mtoto – lishe yake, pumzi yake, usalama wake na anachohitaji ataki- pata kupitia mama.

Kupata ujauzito ni neema kubwa. Kwa kuwa ni neema, mama hana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hiyo na pia kumuomba usalama wa huyo mtoto ajaye, sio tu usalama wa kiafya lakini pia wa kidini yaani awe mtoto mwema na mchamungu. Neema huhusudiwa, hivyo basi mwanamke wa Kiislamu, ficha ujauzito wako isipokuwa kwa watu wake muhimu katika zile hatua za mwanzo.

Katika makala iliyopita, pia tulitaja tahadhari mbalimbali ambazo mama anapaswa kuchukua ili kumlinda na kumtunza mwanawe, ukizingatia kuwa ustawi wa mtoto hutegemea ustawi wa mama.

Baadhi ya hatua za kuchukua tulizozitaja katika kumlea mtoto aliye tumboni ni pamoja na kujielimisha kuhusu ujauzito, hatua na changamoto zake ili kujiandaa kukabiliana nazo. Pia, tulisisitiza umuhimu wa kuanza kliniki, kuchunga lishe, kuacha matumizi holela ya dawa na vitu vingine vinavyoweza kumdhuru mtoto, kunywa maji ya kutosha, kupumzika na kufanya mazoezi.

Mama, baada ya kujifungua

Mtoto anapozaliwa anakuwa hajui ulimwenguni kuna nini. Hivyo, mama anabeba jukumu muhimu la uenyeji, akimtambulisha duniani na kumpa maelekezo muhimu – ulaji, usafi, mavazi na kadhalika. Waingereza wanaita ‘orientation.’

Mtoto ajapo ulimwenguni, mama anaweza kuwa amepatwa na dharura, labda amefariki au anaumwa, ikawa hawezi tena kumuangalia mwanawe. Katika hali hii, mama ni mtu yoyote aliyebeba jukumu lile alilotegemewa mama kulifanya. Anaweza kuwa mama mdogo, shangazi, dada nk. Katika hali chache anaweza kuwa baba.

Anapokuja duniani, maisha ya mtoto yanamtegemea mama kwa hali zote. Kama mama atafanya wajibu wake, mara nyingi, ndiye kiigizo cha kwanza kwa mtoto (role model). Mitazamo ya mtoto, tabia, dini yake inajengeka kutokana na malezi ya wazazi, hususan mama ambaye ndiye huwa karibu naye zaidi.

Mtoto anapokuwa na kukutana na watu wengine, marafiki, walimu shuleni na madrasa, vyombo vya habari; akili na mtazamo hubadilika, lakini athari ya malezi aliyopokea utotoni haifutiki kabisa.

Kabla hatujajadili majukumu zaidi ya mama katika makala zijazo, leo tukumbushe tu taratibu za jumla za Kiislamu za namna ya kumkaribisha mtoto katika siku chache za kwanza duniani, ambazo tulishawahi kuzitaja katika matoleo ya nyuma.

Kwanza mtoto akishazaliwa tu, aadhiniwe kama ambavyo imeripotiwa kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimfanyia mjukuu wake, Hasan katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Raafi na kupokewa na Imam Ahmad, AtTirmithi na Abu Dawud]. Wanazuoni wamependeka aadhiniwe sikio la kulia.

Ni sunna pia kumfanyia mtoto Tahneek na kumuombea. Tahneek ni kitendo cha kuweka kitu kitamu, hususan tende, mdomoni mwa mtoto aliyezaliwa punde. Hufanyika kwa kuilainisha, mfano tende, kuiweka kidoleni na kumpangusia mtoto muda mchache baada ya kuzaliwa. Kitendo hiki kinatajwa katika Hadithi kadhaa ikiwemo ile iliyosimuliwa na Abu Musa.

Mtoto pia anatakiwa kupewa jina ndani ya siku saba tangu kuzaliwa. Jambo muhimu lililosisitizwa ni kumpa jina zuri. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Siku ya Kiyama, mtaitwa kwa majina yenu na majina ya baba zenu, hivyo, jipeni majina mazuri.” (Abu Dawud). Watoto wa Kiislamu mara nyingi hupewa majina ndani ya siku saba tangu kuzaliwa.

Jambo jingine muhimu ni kumnyoa mtoto nywele. Imeripotiwa kuwa, Mjukuu wa Mtume, Hasan alipozaliwa, Mtume alimuelekeza bintiye amnyoe nywele [Ahmad, AtTabaraani na Al-Bayhaqi].

Aqiqah ni sunna nyingine muhimu anayofanyiwa mtoto. Aqiqah ni kuchinja aidha mbuzi au kondoo, ikiwa ni shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mtoto wa kiume ni sunna kumchinjia mbuzi wawili au kondoo wawili, na mtoto wa kike ni sunna kumchinjia mbuzi au kondoo mmoja. Mnyama huyo atakayechnjwa awe na maumbo na sifa za ukamilifu.

Jambo la mwisho ni tohara. Uislamu umeagiza wanaume watahiriwe kwa lengo la kuleta usafi. Tohara ni sunna iliyotiliwa mkazo kwa watoto wa kiume. Mtoto wa kiume anaweza kufanyiwa tohara muda wowote bila sherehe ingawa imekuwa desturi kwa wazazi wengi siku hizi kufanya sherehe. Baadhi ya wazazi hupendelea kumfanyia mtoto tohara akiwa mchanga, baadhi husubiri hadi akuekue. Kilicho bora ni kuwahisha tohara.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close