malezi

Makosa sita ya kimalezi yafanywayo na wazazi

Tukisema tabia njema bila shaka kila mtu anaelewa. Ni tabia ambazo zimekubalika katika jamii husika kupitia vigezo na vipimo vya jamii husika. Kwa mfano, Uislamu unahimiza tabia njema na Mwenyezi Mungu na Mtume wametufundisha ni zipi tabia njema.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika aliye bora kati yenu ni yule mwenye tabia njema.” [Bukhari na Muslim]. Pia kasema: “Mambo yatakayo waingiza sana watu peponi ni uchamungu na tabia njema.” [Tirmidhiy Hadithi Na. 2004. Ibnu Majah Hadithi Na. 4246].

Mifano ya tabia njema ni mingi. Mathalan, kuheshimu wazazi ni tabia njema. Kusalimia watu ni tabia njema. Kuishi vema na majirani ni tabia njema. Kutopandisha sauti unapoongea na wakubwa, kadhalika kuwatii waliotuzidi, uaminifu, ukweli – zote hizi ni tabia njema zilizohimizwa katika Qur’an na Sunna.

Zipo mbinu za kujenga tabia njema ambazo hutumiwa na wazazi tofauti kwa watoto wao. Hata hivyo, mara nyingi kuna kutokubaliana juu ya mbinu ipi ni mujarabu mbinu hizo. Kwa sababu hiyo, suala la kupambana na tabia mbaya ya mtoto na kujenga tabua njema, wakati mwingine, si jambo rahisi sana hasa katika ulimwengu wa leo.

Wataalamu wametaja makosa kadhaa katika kutafuta mbinu sahihi za malezi katika kumjenga mtoto kitabia. Hebu tuone makosa hayo.

Mzazi ‘kuasi’ mbinu alizolelewa
yeye na wazazi wake
Baadhi yetu wazazi tuna kumbukumbu mbaya za namna tulivyolelewa tukiwa watoto. Baadhi ya wazazi wanakumbuka vipigo vikali wakiwa watoto. Wengine wanakumbuka maonevu ya kulaumiwa mara kwa mara kwa makosa ya wengine. Baadhi ya wazazi wengine wamenyimwa uhuru wakiwa watoto na wengine wamekulia katika mazingira ya kukaripiwa muda wowote. Wapo pia wazazi waliofanyishwa kazi nyingi za ndani.

Mzazi anapopitia haya anaweza kujiapiza kuwa akipata mtoto/ watoto atawalea kinyume kabisa na alivyolelewa. Hali hii hupelekea kupitiliza na kumharibu mtoto. Mathalan, mzazi aliyenyimwa uhuru utotoni, kwa kuwa anachukia mapito hayo, atataka mwanawe alelewe kwa kupewa uhuru. Wakati mwingine uhuru huo huzidi sana na kumharibu mtoto.

Unaweza kutoa mifano mingine mingi katika jambo hili. Mzazi ambaye utototni alikaripiwa, alichapwa na kufanyishwa kazi nyingi, atataka mwanawe asipitie hayo, na matokeo yake katika kuasi huo malezi ya wazazi wake, anaweza kumdekeza mtoto na kumharibu.

Kulea kama alivyolelewa yeye/kuiga mbinu za wazazi
Kosa hili ni kinyume na lile la awali. Wakati mzazi yule wa kwanza anachukia namna alivyolelewa na hivyo kutaka kuepuka makosa hayo kwa wanawe; mzazi huyu mwingine alipenda sana alivyolelewa kiasi cha kwamba anatamani na wanawe walelewe hivyo hivyo.

Kuiga mbinu za malezi uliyopewa na wazazi hutokana mazuri uliyopitia utotoni na Imani kwamba wazazi wana uzoefu zaidi yako, hivyo wanafaa kuigwa. Hata hivyo, wazazi nao ni binadamu, wanafanya makosa kama wengine. Kwa hiyo huenda baadhi ya mbinu zao hazikuwa sahihi. Pia, hapa unazungumzia kizazi tofauti. Malezi ya miaka hii yana changamoto tofauti na haya ya miaka yetu.

Tofauti ya itikadi za malezi kati ya wazazi wawili
Wakati mwingine hutokea wazazi wawili wakawa na falsafa tofauti za mbinu za malezi. Jambo moja linaweza kuwa baya kwa mama wa mtoto, lakini kwa baba akaliona kuwa ni sawa tu. Hii hutokana na wazazi hawa wawili kulelewa katika mazingira tofauti au kutoka jamii tofauti. Mfano, kuna jamii, malezi hayaendi bila viboko, na jamii nyingine viboko havipendelewi sana.

Migongano ya mbinu za wazazi mbele ya watoto huchanganya mtoto. Anajiuliza: “Nishike lipi?” Watoto wengine huelemea kule ambako kuna ulaini; ingawa urahisi huo unaweza usiwe na maslahi na faida kwake kwa mtazamo wa muda mrefu. Wakati mwingine, akiona migongano hiyo anaweza kuhisi yeye ni tatizo, na ndio maana wazazi wanagombana.

Jamii kuingilia malezi
Inasemwa kuwa mtoto hulelewa na jamii nzima. Ni kweli, lakini kuna changamoto zake. Ikiwa wazazi wawili tu wanapishana katika mtazamo juu ya mbinu sahihi za malezi, nambie hali ya jamii nzima, tena katika zama hizi ambapo kuna maingiliano makubwa ya watu katika jamii, ukoo na hata familia moja! Miluzi mingi, wanasema, humpoteza mbwa.

Mbinu ya ‘kijiji kizima kulea mtoto’ inafaa katika mazingira ambapo jamii huzika ina vigezo wazi vya tabia ambazo mtoto anatakiwa awe nazo. Mfano, jamii inayofuata Uislamu, bila shaka wana kiigizo chema kwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Mzazi kukosa umakini katika kumsoma mwanawe
Wazazi wengi hufuata kanuni za jumla (generalization) za kimalezi. Kuna kanuni za kimalezi katika kujenga tabia nzuri zinafanya kazi katika mazingira kwa watoto wengi lakini zinaweza kuleta matokeo hasi kwa mtoto mwingine. Kuna watoto wanaoelewa lugha ya viboko tu, wengine huchapwa kwa maneno. Wakisemwa, wanabadilika.

Kuna mbinu tofauti ya kupambana na tabia mbaya kwa mtoto anayefaya kosa kwa mara ya kwanza ukilinganisha na anayerudirudia kosa. Kadhalika, aliyekosea kwa makusudi na bahati mbaya. Umri, jinsia pia ni vitu maalumu vya kuzingatia katika malezi.

Kurekebisha tabia mbaya wakati mzazi ana hasira
Wazazi wengi wanakosea pale wanapojaribu kurekebisha tabia mbaya za watoto wao wakati wametawaliwa na adhabu. Badala ya kuzungumza na watoto kwa utaratibu, mzazi anaishia kumkaripia, kumsonya na kumpiga. Jambo hili linajenga mtazamo mbaya kwa mtoto kuhusu suala zima la tabia njema.

Mtoto anayekebishwa tabia kupitia vipigo, huishia kuoanisha tabia njema na kugombezwa, adhabu na vipigo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close