6. Malezi

Kuheshimu Wakubwa na Kuwahurumia Wadogo ni Katika Nidhamu za Kiislamu

Jukumu la kwanza la mwanadamu ni kwa Mola wake. Mwanadamu anapaswa kumuamini Allah, kumtii na kumpwekesha katika ibada. Haki zetu kutoka kwake ni kuturuzuku, kutupa msamaha na radhi zake na mwisho kututia katika makazi ya milele peponi huko Akhera.

Uislamu umebainisha haki za Mitume ambapo kubwa kuliko zote ni kuwatii kwa kuwa wao ndio wawakilishi na wafikishaji wa Allah kwa viumbe wenzao. Vilevile, mwanadamu amebebeshwa majukumu mengi kama kuzingatia haki za viumbe wenzake wakiwemo wazazi, mke/ mume, watoto, majirani, marafiki, maskini, mafukara, na vilevile wasafiri wenzake, wafanya kazi wenzake, wanafunzi wenzake na wengineo.

Lakini haki haziishii kwa wanadamu wenzake tu, wanyama wana haki zao pia anazopaswa kuwapatia.

Katika muktadha huu, iwapo haki zitafikishwa kwa wenyewe kama ilivyotakiwa, kinachotarajiwa ni ulimwengu huu kutawaliwa na utulivu, amani na ustawi wa kweli wa maisha, kwa watu wote, mahala popote na kwa nyakati zote. Pia, ulimwengu ungetakasika na dhiki, mabalaa na ufisadi.

Tabia njema

Uislamu umetuhimiza kushikamana na tabia nyingi tukufu ambazo husaidia sana katika kujenga mahusiano mema baina ya wanajamii. Makala hii imeitupia jicho moja ya vipengele asili vya nidhamu za Kiislamu ambacho ni kuwaheshimu wakubwa na huruma kwa wadogo.

Uislamu unazingatiwa kuwa ni mfumo wa maisha, unaomuheshimu mwanadamu na kutunza hadhi na nafasi yake bila kujali ni mwanamume au mwanamke, mkubwa au mdogo na katika hatua zote za maisha yake kuanzia utotoni hadi uzeeni.

Uislamu ni dini ya huruma na upole. Kigezo kikuu cha huruma ya Uislamu ni agizo lake la kuwahurumia watoto, wanyonge, yatima na wenye uhitaji.

Anas bin Malik (Allah amridhie) amehadithia kuwa siku moja alikuja mzee fulani anamuhitaji Mtume lakini watu wakachelewesha kumpisha aonane naye. Mtume (hakupenda) ndipo akasema: “Si katika sisi ambaye hamhurumii mdogo wetu na hamheshimu mkubwa wetu.” [Tirmidh].

Katika hadith tuliyoirejea, kumetajwa umuhimu wa kuwahurumia wadogo na kuwaheshimu wakubwa. Hizi ni nidhamu mama za Kiislamu kiasi kwamba Mtume amemtenga mtu ambaye hatajipamba na tabia hiyo.

Baadhi ya njia za kuonesha taadhima kwa wakubwa

Kuna vigezo kadhaa vya kuwatii wakubwa. Kwanza, ni kuwatii kwa kila wanachoamrisha au kukataza, madhali tu hawendi nje ya mipaka ya Allah. Namna nyingine ya kuwaheshimu wakubwa ni kuwaweka mbele katika vikao na kuacha kutosema jambo ila kwa idhini yao. Pia, inatakuwa kusema nao kwa upole na kwa sauti ya chini.

Pia, katika adabu za kuheshimu wakubwa ni kusimama kwa ajili yao. Hii ina maana, mtu mzima hususan mwenye elimu au aliyehiadhi Qur’an anapoingia sehemu inawapasa vijana kuinuka kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha.

Namna nyingine ya kuwawaheshimu wakubwa kuwasalimia kwa kuwashika mikono na kuibusu pamoja na kuwasaidia kubeba mizigo yao.

Kadhalika, wadogo wanatakiwa kuwaita wakubwa kwa majina ya nafasi zao kama vile baba, mama, mzee wangu, bibi, kaka, mjomba na kadhalika. Wadogo waache kuwaita wakubwa kwa majina yao.

Kadhalika, wakati wa kutembea katika msafara ni haki ya wakubwa kuwa mbele na wadogo kuwa nyuma. Hii ni kuonesha taadhima kwa wakubwa.

Haki nyingine ya wakubwa ni kuheshimu maoni na rai zao. Hii ni haki kubwa sana na ya msingi ya wakubwa. Ni kawaida sana kuwakuta vijana wakidharau rai za watu wazima tena mbele ya kadamnasi au kuwakosoa kwa kauli za kejeli pale wanapofanya au kusema kinyume na waonavyo wao. Hili ni kosa kubwa. Vijana tunapaswa kujirekebisha.

Kuwahurumia watoto

Maumbile ya watoto wadogo ni kuwa wategemezi kwa wakubwa na kuwa na mapungufu mengi yanayowafanya washindwe kujihudumia. Pia, watoto ni viumbe wenye hofu na hivyo hutegemea himaya, matunzo na huduma za wakubwa.

Kutokana na hali hizo za watoto, Uislamu umewataka wakubwa wawapende na wawahurumie.

Kuwahurumia watoto hupandikiza tabia ya upendo katika nyoyo zao. Wanapoleleka kwa namna hiyo, inatarajiwa kuwa nao watawahurumia wengine wanapokuwa wakubwa. Katika hadith iliyohadithiwa na Anas, tunajifunza kwamba, Mtume alimshika Ibrahim (mwanawe) akambusu na akamnusa. [Bukhari].

Na katika hadith ya Abu Huraira (Allah amridhie), Aqraa bin Habis alimuona Mtume akimbusu Hassan (mjukuu wake). Habis akamwambia Mtume: “Mimi nina watoto 11 lakini sijawahi kumbusu hata mmoja.” Mtume akasema: “Nitakusaidieni nini ikiwa Allah amezin’goa huruma katika nyoyo zenu!? Asiye na huruma harehemewi.” [Muslim].

Kuwatisha, kuwafanyia ukali na kuwanyanyasa watoto si katika nidhamu za Kiislamu. Wakati ulimwengu wote unalalamika juu ya unyanyasaji na ukandamizaji wa wanawake na watoto ikiwemo kuwaua, kuwajeruhi, kuwafanya wawe wakimbizi; sheria za Kiislamu zilishaharamisha hayo karne nyingi zilizopita.

Upole na huruma kwa watoto na heshima kwa wakubwa zetu ni utambulisho wetu Waislamu tukilenga kuifanya duniaiwe tulivu, yenye amani na ustawi wa kweli.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close