6. Malezi

Khiyana, dhambi mbaya inayopelekea unafiki

Kutoka kwa Abuu Huraira (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Uaminifu utakapokosekana kwa watu basi subiri Kiyama (kwa maana hakuna lolote litakalotengemaa).” Mtume (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake) akaulizwa: “Ni kwa jinsi gani uaminifu utakosekana ewe Mtume wa Allah?” Mtume akasema: “Ni pale atakapopewa jukumu mtu asiyekuwa na sifa ya kulisimamia jukumu hilo” (Bukhari).

Naam! Hii ndio hali halisi iliyopo ulimwenguni hivi sasa. Zama za sasa khiyana imekuwa ni donda-ndugu lenye athari mbaya kwa mtu mmoja mmoja na pia kwa jamii. Khiyana husababisha maangamizi na hasara kwa umma, huharibu murua wa jamii, huleta ugomvi mahala pa amani, dhulma mahala pa haki, na hofu mahala pa utulivu.

Allah Aliyetukuka anasema: “Na atakayefanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyoyafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyoyachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.” (Qur’ an, 3:161).

Kwa kutambua madhara ya kukhini, Uislamu unawataka wafuasi wake wajitenge na vitendo viovu vya kuvunja ahadi na mikataba kwa kuwa vinasababisha matatizo na migogoro ndani ya jamii. Na hakika kadhia ya kukhini itapelekea udhalili na majuto kwa watu Siku ya Kiyama ila kwa mtu ambaye atasimamia kwa haki na akateleza majukumu yake ipasavyo.

Allah Aliyetukuka anasema: “Na atakayefanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyoyafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyoyachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.” (Qur’ an, 3:161). Hivyo, ni wajibu mtu kusimamia uaminifu kwa njia ya haki na ya uadilifu. Wadhifa wa hakimu ni amana, na wadhifa wa ukurugenzi katika taasisi au asasi yeyote ile ni amana, majukumu ya usimamizi katika mambo ya familia ni amana nk.

Ni wajibu kuhifadhi amana, ziwe ni za mambo yanayohusu jamii kwa ujumla au mambo ya mtu binafsi. Pia ni muhimu kuzitekeleza katika njia inayotakiwa kisharia Ni haramu kuifuja amana, kuiharibu na kuikhini. Allah Aliyetukuka anasema: “Enyi mlioamini! Msimfanyie khiyana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua.” (Qur’an, 8:27).

Na amesema tena Allah Aliyetukuka: “Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe.” (Qur’an, 4:58). Waislamu watambue kuwa khiyana ni jambo baya/ovu linaloleta vurugu na mifarakano miongoni mwa wanajamii.

Ubaya wa kukhini
Kukhini amana ni alama ya unafiki. Imepokewa hadithi na Abdillah bin Amri kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mambo manne iwapo yatapatikana kwa mtu anakuwa ni mnafiki halisi bila ya chembe ya shaka. Na likipatikana moja tu katika manne hayo anakuwa ana sehemu ya unafiki hadi atakapoacha.

Mosi, pindi anapoaminiwa anafanya khiyana. Pili, akiongea huongea uongo. Tatu, akiahidi hatekelezi. Nne, akigombana hupitiliza.” (Bukhari).

Si hivyo tu, kukhini ni katika sifa za watu wapotofu na wanafiki. Khiyana pia husababisha matokeo mabaya kwa watu na jamii, ambapo husaidia kuzuka hitilafu, ugomvi, aidha kunatia wasiwasi kati ya watu wa jamii. Allah Aliyetukuka anasema ndani ya Qur’an: “Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi; bali kwa hakika tuliwakuta wengi wao ni wapotofu.” (7:102).

Ni kwa kuzingatia hilo Waislamu wanapaswa kuheshimu ahadi na mikataba kwani kufanya hivyo kutapelekea kuepusha vurugu na mifarakano katika jamii.

Ni ipi hukumu ya mwenye kukhini
Kukhini kwa njia yoyote ile ni katika madhambi makubwa. Lakini licha ya kuwa ni katika madhambi makubwa, bado mlango wa toba upo wazi, kwani Allah Mtukufu anatuambia: “…Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tama na rehema ya Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Qur’an, 39:53).

Mtu aliyekhini na kuvunja uaminifu ataangalia. Iwapo uaminifu huo aliouvunja ni katika haki za Allah, inapaswa kuzidisha kuleta toba na istighfari. Na iwapo amevunja uaminifu katika haki za watu, hapo ataleta toba na kisha inabidi airudishe haki ya watu kwa mwenyewe au aombe msamaha.

Imepokewa hadithi na Abu Huraira (Allah amridhie) akieleza kwamba Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) amesema: “Mtu yeyote ambaye amemdhulumu mwenzake kwa kumvunjia heshima yake, basi atafute mapema ufumbuzi wa jambo hilo hata kabla ya kufika siku ambayo haitafaa dinari wala diraham (kwa maana ya Siku ya Kiyama). Iwapo aliyemvunjia mwenzake heshima anayo matendo mema yatachukuliwa kulingana na kiasi alichomdhulumu mwenzake katika heshima yake. Na kama hana matendo mema kabisa, basi yatachuliwa mabaya ya aliyemvunjia heshima na kupewa yeye.” (Bukhari).

Ni wazi kila mmoja anapenda kuwa na sifa ya Uumini. Jambo muhimu na la msingi kuliko yote ni kujipima ili kujua kama ametimiza sifa hiyo kikamilifu ili awe Muumini wa kweli na hatimae kufaulu Siku ya Kiyama. Allah Aliyetukuka anasema ndani ya Qur’ an: “Bali mtu juu ya nafsi yake ni mwenye kuiona (kuifahamu). Na ingawa atatoa chungu ya udhuru.” (75: 14-15).

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close