6. Malezi

Jamii iache kuchukua sheria mkononi

Katika siku za hivi karibuni kumeendelea kuwapo kwa vitendo na tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga, kuwaua na kuwachoma moto baadhi ya watu wasio na hatia pamoja na wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sharia tukufu za dini Kiislamu na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi la Tanzania za tangu mwezi Januari hadi Machi 2018, jumla ya matukio ya kujichukulia sheria mkononi yaliyoripotiwa yalifikia 479 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2017 ambapo jumla ya matukio 480 yaliripotiwa nchi nzima, ikiwa ni ziada ya tukio moja, sawa na asilimia 0.2.

Ushauri wetu kwa wananchi ni kwamba wawe na busara kwa kuwalinda wahalifu hadi pale vyombo vya dola, hasa polisi watakapofika kwenye eneo la tukio na kufanya kazi yao kwa mujibu wa sheria.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi ni pamoja na baadhi wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya dola kwa kuhisi kwamba wahalifu hawapewi adhabu wanayoitaka wao; na wakati mwingine watuhumiwa huachiwa huru siku chache baada ya kufikishwa kituo cha polisi.

Mbali na hao, pia wapo wanaoamua kuwaua washukiwa wa uhalifu ili kuepuka usumbufu wa kufungua kesi katika vituo vya polisi. Sababu hizi pamoja na nyingine zinazofanana na hizo huchukuliwa kama kigezo cha kuhalalisha mauaji na kuwachoma moto wahalifu. Kimsingi, kuua ni jambo ovu na lisilokubalika kidini na kijamii.

Wananchi wanapaswa kutambua kuwa kitendo cha kuwapiga, kuwaua na kuwachoma moto wahalifu ni kosa kubwa litakalowagharimu hapa duniani na mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya hesabu (Kiyama). Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msiue nafsi ambayo Allah amekataza (kuiua) isipokuwa kwa haki. Na mwenye kuuawa kwa kudhulumiwa, basi tumempa nguvu mrithi wake ( juu ya muuaji huyo, akitaka ataomba kwa hakimu kuwa amuuwe kama alivyomuuwa mtu wake na akitaka atamsamehe, na akitaka atamtoza kitu).” [Qur’an, 17:33].

Mwenyezi Mungu akasema tena: “Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Allah, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Allah isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara. Na atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka milele.” [Qur’an, 68–71].

Kuwaadhibu watu wasio na hatia au kuwapa adhabu kubwa kinyume na ile inayostahili kupata mhalifu kunajenga chuki, uhasama na migawanyiko baina ya wanajamii na vyombo vya dola. Sisi Imaan media, tunatambua kuwapo kwa hatua na juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vya dola katika kuwachukulia hatua watu wanaowaua na kuwachoma moto wahalifu.

Ushauri wetu kwa wananchi ni kwamba wawe na busara kwa kuwalinda wahalifu hadi pale vyombo vya dola, hasa polisi watakapofika kwenye eneo la tukio na kufanya kazi yao kwa mujibu wa sheria. Hapa nchini, matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yameota mizizi katika maeneo mengi ya mijini. Mtu anapopata ajali kwa kugongwa na chombo cha moto kama vile gari au pikipiki, wananchi wamekuwa na tabia ya kumshambulia dereva badala ya kuviachia vyombo vinavyosimamia sheria kuchukua hatua.

Kwa kuzingatia hayo, tunapenda kuwasihi polisi kwamba, pamoja na kuheshimu utekelezaji wao wa majukumu, lakini ni muhimu pia kauli zao za kuonya wanazozitoa kwa wavunja sheria ziambatane na utekelezaji, la sivyo matukio haya yatazidi kushamiri, na wananchi wasio na hatia wataendelea kuumia au kuuawa kwa matukio ya kuhisiwa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close