6. Malezi

Haki za Mke asiye Muislamu katika Sheria ya Kiislamu

Mwanamke ana nafasi kubwa katika jamii. Katika kuonesha taadhima kwa mwanamke wapo waliomuita ‘nusu ya jamii’akikamilisha nusu nyingine ambayo ni mwanamme.

Mwanamke amepewa nafasi, cheo na majukumu yanayomfanya ashirikiane na mwanamme katika kutekeleza wajibu wake, kwani mwanamke anamsaidia mwanamme maishani.

Kwa hiyo, Uislamu unamheshimu mwanamke na kumpa nafasi ya juu. Mwanamke anafanya shughuli sambamba na mwanamme katika kujenga familia, kutafuta riziki na kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo, kuchagua mke au mume bora ni jambo lililohimizwa katika sheria ya Kiislamu huku viikiwekwa vigezo mahususi vya zoezi hili. Uchaguzi ni muhimu kwa sababu mke na mume ndiyo nguzo kuu za familia na jamii.

Kwa upande wa mke, yeye ndiye msingi wa malezi ya familia yote, na hivyo anaweza kuathiri malezi ya watoto na kuwafanya aidha wawe na tabia na maadili mazuri au la.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.” [Qur’an, 30:21].

Katika tafsiri yake ya aya hii, Imam al-Tabariy amesema: “Maana ya aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu amekujaalieni utulivu na mapenzi ya kukuunganisheni na rehma kwenu wenyewe kwa wenyewe.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ameainisha sifa muhimu za mke na vigezo vya kuchagua pale aliposema:

“Mwanamke huchaguliwa kuolewa kwa kuzingatia utajiri wake au nasaba yake au uzuri au urembo wake au dini yake; basi chagua mwenye dini ni bora kwako.”

Katika hadith nyingine iliyosimu – liwa na Abdullah bin Omar bin al-As (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Dunia ni anasa na anasa bora zaidi katika dunia hii ni mke bora.”

Mjukuu wa Mtume, Hasan, alijiwa na mtu, akasema: “Ewe Hasan binti yangu ameombwa kuolewa na wanaume wengi, basi ni nani nimkubali awe mumewe?” Akasema: “Aliye mchamungu kwani akimpenda atamkirimu na kumtunza; na akimchukia hatamfanyia dhuluma.”

Japokuwa Muislamu anatakiwa kuchagua mke kwa mujibu wa vigezo hivyo vilivyotajwa juu, pia anaruhusiwa kumuoa mke ambaye si Muislamu; kama ambavyo pia anaruhusiwa kuwa na wake wawili, watatu au wanne. Hata hivyo, anapaswa kuzingatia masharti na misingi iliyowekwa na sheria.

Kuhusu suala la mitala, sheria ya Kiislamu haimaanishi kila Muislamu ana haki ya kuoa wake wanne hovyo hovyo tu, bali imeweka masharti, vidhibiti, vigezo ambavyo mume yampasa kuvizingatia na kuvitekeleza.

Ikumbukwe pia kuwa sheria ya Kiislamu juu ya mitala ilizingatia mazingira ya jamii kwani kimaumbile wanawake wako wengi zaidi kuliko wanaume .

Hivyo, iwapo kila mwanamme akioa mke mmoja, wanawake wengi wanaweza kubaki bila kuolewa.

Wakati huo huo, yapo baadhi ya matukio yanayomruhusu mwanamume awe na mke wa pili kama vile mke wa kwanza kuwa tasa. Kwa hiyo, kimsingi suala la mitala halikuachwa kufanywa hovyo, bali lina taratibu na vigezo vyake. Pia, kuna hekima katika Uislamu kuruhusu mitala. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema:

“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu.” [Qur’an, 4:3].

Ieleweke pia kuwa sheria ya Kiislamu haikutofautisha baina ya mke Muislamu na asiye Muislamu katika haki za wake katika Uislamu. Mume anatakiwa awe muadilifu kwa wake zake wote bila kujali dini ya mke.

Kama mume Muislamu amemuoa Mkristo au Myahudi, anatakiwa kumheshimu na kumfanyia hisani. Mume hana haki ya kumlazimisha mke ajiunge na Uislamu ila anatakiwa amlinganie halafu ampe uhuru wa kufuata dini aitakayo.

Ieleweke kuwa, mke ambaye si Muislamu ana haki ya kutunzwa na mumewe na mume anawajibika kushauriana naye katika masuala ya maisha yao na watoto wao. Vile vile, mume Muislamu anatakiwa kumvumilia mke wake ambaye si Muislamu kama akikosea jambo lisilo kuwa ni upungufu katika dini.

Kwa ujumla, sheria ya Kiislamu ilipoainisha haki za mke, haikumhusisha mke ambaye ni Muislamu tu na kumpuuza na kumdharau yule asiye Muislamu.

Sheria hiyo imemuwajibisha mume amtunze mkewe na kuishi naye kwa hisani na wema bila ya kujali dini yake wala ukoo wake wala kabila wala nchi anayotoka. Mume katika sheria ya Kiislamu ana wajibu wa kuwatunza mke na watoto kwa chakula, malezi, upendo, nasaha, ulinzi na maisha mazuri

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close