6. Malezi

Dondoo za ndoa yenye furaha na mafanikio

Vijana wanaotaka kuingia kwenye ndoa mara aghlabu huwa na shauku kubwa mno kuhusu harusi na maisha ya baada ya ndoa. Baada ya miezi mitatu au sita, uhalisia wa ndoa yao huanza kujitokeza. Hapo, wanandoa hao huanza hutambua kwamba kumbe ndoa siyo kazi rahisi bali inahitaji juhudi kubwa, uvumilivu na subra kuijenga.

Zifuatazo ni dondoo zitakazowasaidia vijana wa kike na kiume katika kujenga ndoa ya ili iwe ya furaha na upendo .

Ingia kwenye ndoa kwa dhamira Sahihi

Wenza wote wanapaswa kuingia kwenye ndoa wakiwa na dhamira safi ya kumridhisha Allah ‘Azza wa Jalla’ ili kupata neema na baraka zake. Mkifanya hivyo, ndoa yenyewe sasa inakuwa kitendo cha Ibada, ambacho wanandoa wote watalipwa thawabu na kupata amani, utulivu na furaha.

Kitendo cha Ibada kinapoendelea kwa muda mrefu ni muhimu kurejea upya dhamira ya awali ili muda wote ubaki kwenye njia sahihi ya Mwenyezi Mungu, na kuvuna faida kubwa.

Kumbuka mwenza wako pia ni ndugu katika Imani

Mara nyingi baadhi ya Waislamu huwahudumia watu wa nje ya nyumba zao kwa wema, bashasha na uadilifu lakini hawafanyi hivyo kwa wenza wao. Kumbuka wakati wote kwamba mwenza wake pia ni dada au kaka katika Uislamu na kwamba haki na wajibu kuhusu udugu wa Kiislamu kwa ujumla, pia inahusika katika kujenga msingi wa mahusiano ya ndoa.

Kwa msingi huo, bila shaka mwenza ana haki zaidi kuliko hizi lakini lazima kuwe na ufahamu wa wazi kuhusu haki za udugu wa Kiislamu na kuzingatia misingi inayojenga haki hizo.

Msiwe na matarajio yasiyo halisi

Kabla ya ndoa, aghlab watu huwa na matarajio yasiyo halisi kuhusu wenza wao. Wanandoa hao hutegemea wenza wao wawe wakamilifu katika idara zote, jambo ambalo sio halisi na linaweza kuleta matatizo yasiyo ya lazima katika ndoa iwapo matarajio hayatafikiwa.

Tunapaswa kukumbuka kwamba Allah ‘Azza wa Jalla’ ameumba wanadamu kama viumbe wasio wakamilifu, hivyo kila mwanadamu anafanya makosa katika maisha yake yote. Kwa kutoweka matarajio yasiyo halisi, tutashangazwa sana na kufurahishwa pale mwenza wetu anapokuwa vizuri zaidi ya kile tulichotarajia. Hili litaleta faraja na kuridhika ndani ya ndoa.

Shikilia zaidi mazuri ya mwenza wako

Kwa kuwa hakuna aliyejaaliwa kuwa na sifa bora zote na ukamilifu, mkazo uwekwe kwenye sifa chanya ambazo mwenza anazo. Mwanandoa anapaswa kumtia mwenzake moyo, kumsifia na kumshukuru wakati wote, hatua ambayo itaimarisha zaidi sifa hizi, kuzifanya ziwe na faida katika kuendeleza sifa nyingine.

Pia, tuwe tunajitahidi sana kusahau na kupuuza mapungufu ya wenza wetu, kama alivyosema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Mwanaume Muumini hapaswi kuwa na nongwa dhidi ya mwanamke Muumini. Anaweza asipende kitu kimoja kwa mwanamke huyu lakini anaweza kuona kingine kinachompendeza.” [Muslim]

Kuwa rafiki mkubwa wa mwenza wako

Jaribu kufikiri kitu gani kinachochea urafiki kati ya mtu na mwingine, kisha fanya hivyo kwa mwenza wako. Ili kujemnga urafiki, tafiti mambo ambayo mwenza wako anayapenda na asiyoyapenda, kisha jaribu kumridhisha kwa njia yoyote ile inayowezekana.

Rafiki mkubwa ni yule ambaye anaweza kuaminika na kuambiwa siri za ndani na kutegemewa hata wakati wa matatizo. Mwenza katika ndoa anapaswa kuwa aina ya rafiki ambaye mtu anataka kuwa naye katika maisha yake yote.

Tumieni muda muhimu pamoja

Haitoshi kula pamoja, kusaidiana kazi za nyumbani na kufanya mazungumzo madogo madogo, bali wenza pia wanapaswa kutafuta muda maalumu wa kuimarisha uhusiano wao.

Mara nyingi wanandoa wanakuwa ‘bize’ na kazi zao tofauti za kuwaingizia kipato na kusahau kutumia muda kwa ajili katika vipengele muhimu vya maisha kama mazungumzo ya upole, kutembelea maeneo yenye mandhari tulivu za asili au kushirikiana katika mnayoyapenda pamoja. Wanandoa wachague jambo ambalo wote wanalifurahia na wajitahidi kudhibiti usumbufu wowote utakaowatoa katika jambo hilo bila ya sababu za msingi ikiwemo kwa mfano simu.

Eleza hisia mara kwa mara

Hii pengine ni dhana ya ‘Kimagharibi’ zaidi ambayo baadhi ya watu wanaweza kuwa na ugumu kuitekeleza lakini ni muhimu sana kuwa muwazi na mkweli kuhusu hisia zako zote, chanya na hasi.

Mawasiliano yanapaswa kuwa wazi wakati wote na kero yoyote inapaswa kuwekwa bayana kwa mwenza mwingine pale inapoibuka. Hekima ya hili ni kwamba jambo linaloanza kama kero rahisi, linaweza kukua na kugeuka tatizo kubwa iwapo halitashughulikiwa haraka na kwa usahihi. Kushughulikia kero kwa ‘kukaa kimya’ (silent treatment) haijawahi kuwa tiba ya kero yoyote.

Kubali makosa na omba msamaha 

Kama vile tunavyomuomba Allah ‘Azza wa Jalla’ atusamehe pale tunapofanya makosa, pia tunapaswa kufanya hivyo hivyo kwa wenza wetu.

Mtu madhubuti ni yule ambaye anaweza kukubali pale anapofanya makosa, akaomba msamaha na akajitahidi kuboresha vipengele vya tabia vyenye kasoro. Kama mwanandoa hawezi au hataki kufanya hivi, kutakuwa na ukuaji mdogo na maendeleo katika ndoa hiyo.

Msifufue makosa yaliyopita

Linaweza kuwa jambo linalouma sana kwa mtu mwingine kukumbushwa makosa yake yaliyopita. Katika Uislamu, huwa haishauriwi sana kufufua mambo yaliyopita. Mtu anaweza kukumbuka makosa ambayo yalifanyika ili yasirudiwe tena, lakini hili halipaswi kufanyika kupita kiasi.

Kwa hakika, kama wanadamu, hatuko kwenye nafasi ya kumuhukumu mwingine. Ushauri unaweza kutolewa, lakini siyo katika namna ambayo inaumiza.

Peaneni ‘sapraizi’ wakati mwingine

Hii inaweza kuhusisha kurudi nyumbani na zawadi ndogo au maua, kuandaa chakula maalumu, kuvaa mavazi na kujipamba (hii siyo kwa wanawake tu), au kutuma ujumbe mzuri wa mapenzi kwenye simu. Ukifanya hivyo, hisia za mwenza wako zinakwenda mbali na kujiona anajaliwa. 

Lengo la ‘sapraizi’ hizi ni kuinogesha ndoa na kukwepa kuingia kwenye utaratibu ule ule uliozoeleka na usiotia hamasa, ambao unaweza kuleta athari hasi kwenye ndoa hiyo.

Fanyeni mzaha na ucheshi

Dondoo hii maalumu inaweza kusaidia sana kuzuia mizozo na kutuliza hali ya hewa nyumbani. Maisha ni mtiririko wa kudumu wa changamoto na majaribu. Kukaribiana na changamoto kwa moyo mwepesi husaidia kuifanya safari ya ndoa kuwa nyepesi na yenye furaha zaidi.

Kupitia utani, mizaha na michezo, unaweza kugundua kuwa mwenza wako anafurahia na wakati wote anapenda kuwa pamoja na wewe ili apate kucheka na kutabasamu.

Pale panapotokea mkwaruzano

Pale panapotokea mkwaruzano, anza majadiliano ya kutatua tatizo hilo. Kama wenza wote wawili wana nia hii na wanapanga kuwa pamoja, basi lazima utapatikana ufumbuzi wenye mafanikio.

Kumbuka wanahitajika watu wawili ili kuzozana. Iwapo mtu mmoja ataamua kutozozana, basi hakutakuwa na mzozo hapo. Kwa kawaida, yule mwenye makosa ndiye hasa anayeongea zaidi! Wenza wote wawili hawapaswi kukasirika kwa wakati mmoja. Mmoja anapochukia ni vizuri mwingine akawa mtulivu na aliyedhibiti hasira zake.

Msifokeane na kupayukiana labda nyumba yenu iwe imeshika moto! Bila shaka, matukio ya nyumba kushika moto ni nadra sana kutokea, basi kupayukiana kunapaswa kutokea kwa kiwango kama hicho, siyo iwe utaratibu wenu wa maisha.

Msiende kulala kabla hamjasuluhisha tofauti yenu. Hili ni jambo baya sana ambalo linaweza kutokea kwenye ndoa, na linapaswa kuepukwa kadri inavyowezekana. Kulala bila kusuluhisha tofauti huruhusu hisia za maumivu na hasira kudumu kwa muda mrefu na hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close