6. Malezi

Chunga yafuatayo katika malezi

Wapenzi wasomaji, leo katika safu ya malezi, tutaangalia vitu vinavyoharibu maadili ya watoto. Kama tujuavyo watoto hujifunza kwa kuiga au kuona kutoka kwa watu wao wa karibu ikiwemo wazazi, walezi, ndugu, jamaa pamoja na marafiki wao wa karibu.

Watu hao wote huweza kuathiri tabia na makuzi ya watoto katika nyanja kuu mbili tofauti: athari chanya na athari hasi.

Kwa miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia kuporomoka kwa maadili ya watoto kwa kiwango kikubwa.

Jambo hili limepelekea kuibuka kwa maswali mengi juu ya nini hasa chanzo cha kudondoka huko kwa maadili. Viashiria vya kudondoka huko kwa maadili ni pale tuonapo watoto wengi hawaheshimu wazazi wala watu wengine waliowazidi umri, wanatumia pombe na madawa, wanaiba, wana kiburi na pia kuonesha tabia zote mbaya.

Hapa tutataja baadhi ya vitu vinavyoharibu maadili ya watoto. Wazazi kuwa mfano mbaya Wazazi au walezi wamekuwa mfano mbaya kwa watoto.

Wazazi kuwa mfano mbaya

Wazazi au walezi wamekuwa mfano mbaya kwa watoto. Wazazi, kwa mfano, wamekuwa wakilewa, wakitukanana, wakipiganana au hata kufanya mambo mengine machafu kama vile uzinzi mbele ya watoto. Matokeo ya hali hii ni watoto kuiga tabia hizo, wakizichukulia kuwa ni jambo la kawaida kabisa.

Kwa mlezi ambaye amekuwa na tabia mbaya, mathalani tabia ya kutukana, hawezi kukataza au kumchapa mtoto wake anayetukana watoto wengine kwa sababu yeye mwenyewe hutukana na kuona kitu cha kawaida.

Wakati mwingine, inawezekana wazazi wakawa na maadili mema lakini ikatokea watoto wakawa na tabia mbaya. Hii huweza kutokea kwenye nyumba za kupanga zinazokusanya watu wa aina, dini na makabila tofauti. Ushawishi unaotokana na watu hawa wenye utamaduni tofauti unaweza kuathiri tabia ya mtoto kwa namna moja au nyingine.

Kudekeza watoto

Wazazi wengine wamekuwa wakiwadekeza watoto pamoja na kutosimamia vyema maadili yao na hivyo kuwafanya wakue bila nidhamu ya kutosha. Waswahili husema: “Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe.” Msemo huu unaelezea gharama ambazo mzazi anaweza kuingia kwa kulealea tabia mbaya za watoto. Mtoto mdokozi nyumbani, ndiye jambazi wa kesho iwapo akiachwa bila kudhibitiwa. Unaijua adhabu ya jambazi anapokamatwa mtaani? Ni kifo. Na hapo ndiyo mzazi hulia yeye. Rekebisha tabia mbaya ya mtoto sasa maana dawa ya jipu ni kulitumbua tu.

Vifaa vya teknolojia

Teknolojia ina faida zake lakini pia ina hasara zake hasa katika malezi ya watoto wetu. Katika miaka ya hivi karibuni, watoto wamekuwa wakitazama mambo maovu kwenye televisheni pamoja na mitandao ya kijamii na kuyaiga. Jambo hiili limepelekea watoto kujifunza tabia chafu kutoka kwenye tamaduni ngeni, hususan za kimagharibi.

Kutokana na maendeleo hayo ya sayansi na teknolojia yanayoruhusu muingiliano mkubwa wa tamaduni, watoto hukua huku wakichukulia kuwa tamaduni zao za Kiafrika hazina maana. Kwa hali hii, wazazi tunatakiwa kuwa makini na watoto wetu hasa pale tunapowapa uhuru wa kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii Mfano; Facebook, WhatsApp, Instagram pamoja na mitandao mingine.

Marafiki

Sababu nyengine inayopelekea kuharibika kwa maadili ya watoto ni marafiki. Inawezekana mtoto amelelewa vizuri nyumbani kwao lakini akajifunza mambo mabaya kutoka kwa marafiki zake anaokutana nao katika mazingira ya shuleni, ujirani na kwingineko anapotembelea.

Bahati mbaya ni kuwa, kama mzazi, huwezi kurekebisha tabia za watoto wote ambao mtoto wake anakutana nao kwani wao wana wazazi wao, lakini walau unaweza kumdhibiti mwanae kwenye suala la marafiki. Hivyo, ukihisi mtoto fulani analeta ushawishi mbaya kwa mwanao, tumia busara za kumuweka mbali na mwanao.

Mazingira unapoishi

Jambo jingine linaloweza kuharibu maadili ya watoto ni mazingira mabaya ya kuishi. Hapa sizungumzii hali ya nyumba au ukubwa wake, wala pia sizungumzii umaskini. Nazungumzia maeneo ya ujirani ilipo nyumba yenu. Je, mazingira hayo ni salama?

Hebu fikiri mtoto anakaa kwenye mazingira yanayouzwa madawa ya kulevya au kuna kijiwe cha ukahaba! Ni wazi kuwa, mtoto huyo ataiga tabia chafu. Hata kama hataiga, huenda anayoyaona yatamuathiri kisaikolojia. Tunachosema ni kuwa, tuwe waangalifu na mitaa tunayoamua kuishi.

Unyanyasaji

Vitendo vya unyanyasaji vimeshamiri sana hivi leo. Watoto wamekuwa wakitukanwa, kuchomwa, kupigwa, kubakwa, kulawitiwa na kufanyiwa ukatili mwingine mbalimbali. Afanyiwapo hivyo, mtoto anaathirika kisaikolojia na kumfanya akue akiwa na majeraha ya nafsi, akili na mwili. Mara nyingi watoto waliofanyiwa unyanyasaji hutaka kulipa kisasi au hukata tamaa na kuamua kuishi maisha ya hovyo.

Mengine ambayo yanaweza kuharibu maadili ya mtoto ni pamoja na kutopewa haki ya kusikilizwa, kunyimwa huduma za msingi stahiki kutegemeana na uwezo wa wazazi na pia. Haya niliyoyataja yanachangia sana kuharibika au kuporomoka kwa maadili ya watoto Ikiwa wazazi na walezi wanataka kunusuru vizazi vijavyo, ni vyema wahakikishe wanakabili vitu hivyo tulivyovitaja.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close