6. Malezi

Athari ya Dawa za Kulevya kwa Jamii

Tafiti na takwimu nyingi zimethibitisha madhara makubwa ya dawa za kulevya kwa afya ya mwanadamu, kiakili na kimwili. Dawa zinaharibu akili na kudhoofisha kumbukumbu na ufahamu wa mwanadamu.

Si hayo tu, dawa za kulevya husababisha mtu kupata wasiwasi, woga na hisia mbalimbali zinazomvuruga mwanadamu vibaya kiakili na mwenendo wake wa jumla.

Takwimu za mwaka 2019 zilizotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Udhibiti wa Dawa za na Kuzuia Uhalifu UNODC zimebainisha kuwa watu milioni 35 ulimwenguni wameathirika kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya. Zaidi ya hayo watu laki mbili wanakufa kila mwaka wakiathiriwa na dawa hizo, achilia mbali wale wanaojiua.

Kutokana na takwimu hizo, utaona wazi kuwa dawa za kulevya, pombe, mihadarati ni msingi wa shari kubwa na uharibifu kwa sababu zinaharibu akili, ambayo ndio inategemewa katika kumuongoza na kumwelekeza kwenye njia ya manufaa na kumwepusha na njia ya shari.

Kwa upande mwingine, ukiacha kuathiri mwili na akili, ulevi, mihadarati na dawa za kulevya humkaribisha mtu na maovu na kumuweka mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu. Katika athari mbaya za dawa za kulevya ni dua za wahusika kutokubalika kwa sababu wamepinga ukaribu na Mwenyezi Mungu kwa kukumbatia aliyoyaharamisha.

Vilevile, ulevi humpelekea mtu alaaniwe na kufukuzwa kutoka katika rehma na amani ya Mwenyezi Mungu na ridhaa ya Mtume. Dawa za kulevya pia hupelekea mtumiaji kupata maradhi mengi yanayoweza kumuangamiza. Licha ya hayo, utumiaji dawa za kulevya huharibu mahusiano ya mtu ya kijamii na na kuchochea jinai nyingi na uhalifu wa aina mbalimbali.

Kwa kuangalia namna dini ilivyoiangalia akili, tunatambua kuwa utaona kuwa sheria imekataza dawa za kulevya kwa sababu ya athari zake mbaya kwa akili na mwili. Athari haziishii katika afya ya mwili na akili, bali pia kuna madhara ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa kwani baadhi ya waathirika wana vipaji vikubwa vya uongozi.

Madhara ya Kiuchumi

Kuhusu athari za kiuchumi, ni wazi kuwa familia, jamii na mataifa yanaathrika sana kwa uwepo wa watumiaji dawa za kulevya. Watumiaji wa dawa za kulevya hawasaidii uchumi wa nchi zao ila huuharibu kwa kuwa kwao katika hali ya kushindwa kuzalisha.

Vilevile, familia nyingi zimefilisika kwa kuwa na mtumiaji miongoni mwao. Watumiaji wengine wameingia katika wizi kwa sababu ya kushindwa kuzuia hamu ya kupata dawa za kulevya (uraibu). Wengine wanatumia fedha nyingi katika kununua ulevi huo, huku familia ikishimdwa kutimiza mahitaji muhimu ya familia.

Biashara hii inapoendelea, ikumbukwe, uchumi wa nchi haufaidiki chochote. Hakuna kodi inayolipwa, ukizingatia ni bidhaa haramu. Zaidi, nchi hupata hasara tu kwa kutumia majeshi kupambana na biashara hiyo huku fedha nyingi pia zikitumika kutibu waathirika.

Kwa ujumla, watumiaji wa dawa za kulevya hawana mchango wowote katika kuusukuma na kuusaidia uchumi wa nchi yao uimarike na kuendelezwa.

Kuharamishwa pombe

Kwa kweli, katika kutoa hukumu ya kuharamisha na kukataza ulevi, ikiwemo dawa za kulevya, sheria ya Kiislamu ilifuata mfumo wa kutoa hukumu kidogo kidogo ili kusisitiza uharamu wake na hatimaye kumaliza kabisa tabia hiyo.

Kuharamisha mabaya haya kidogo kidogo kama njia ya kuziandaa nafsi (hasa za waliozoea kufanya mabaya haya) zikubali hukumu za Mwenyezi Mungu na hatimaye ili kuhakikisha mwitikio wa hukumu za dini kwa walengwa.

Pia, mfumo huo wa kuharamisha na kutoa makatazo kidogo kidogo unalenga kutoa hukumu kwa ulaini na upole na kuwapa walinganiwa fursa ya kupata nafuu kutokana na mabaya haya ambayo ni kama maradhi yanayohitaji muda kiasi mpaka kufikia kupona kabisa.

Mfumo wa kutoa hukumu za kisheria kidogo kidogo ulihitajika hasa katika mambo yaliyoendelea kwa muda mrefu katika jamii ya kabla ya Uislamu kama ulevi na ibada ya masanamu.

Aya ya kwanza kuhusu hukumu ya ulevi ilibainisha tu madhara yake, kama ilivyokuja katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

“Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema, ‘Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake.” [Qur’an, 2:219].

Hatua ya pili ya uharamishwaji wake Mwenyezi Mungu alikataza mlevi kusali wala au kufanya ibada mpaka akili irejee. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema:

“Enyi mlioamini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayo yasema.” [Qur’an, 4:43].

Katika hatua ya tatu imekuja matini ya wazi ya kukataza ulevi na kuharamisha unywaji pombe vikitajwa kuwa ni sehemu ya kazi za shetani ambayo Waislamu wanatakiwa kuepukana nayo. Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa} [Qur’an, 5:90].

Katika aya inayofuata, Mwenyezi Mungu anabainisha sababu za kuharamisha ulevi. Pia, anataja baadhi ya athari mbaya za ulevi:

“Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha?” [Qur’an, 5:91].

Hitimisho

Kwa hakika kutumia dawa za kulevya ni tabia mbaya inayomharibu mtu na jamii nzima. Jamii iliyojaa watumiaji dawa za kulevya haina nguvu yoyote ya kupambana na maadui wala uwezo wa kutumiza malengo yao kiuchumi, kisiasa, kijamii. Hii ni kwa sababu malengo hayo yote yanategemea rasilimali watu.

Juu ya yote hayo, ulevi, kama tulivyoona, humuweka mtu mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Ulevi umeitwa kazi ya shetani. Hakika ulevi ni mama sio tu wa maasi bali pia baba wa kila uovu. Hakuna jema linaloweza kupatikana kwa kujihusisha na ulevi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close