3. Kitabu Nilichokisoma

Zifahamu njia za uwekezaji wa Pamoja

Uzeofu unaonyesha kuwa kumekuwa na hamasa kubwa ya watu wengi kutaka kuwekeza na kukuza vipato vyao, na hii inaweza kuwa ni kiasharia cha mambo mengi yakiwemo:

  • Kuongezeka kwa gharama za maisha na watu kuitaja njia za ziada za kuongeza vipato vyao
  • Kuwa na haja ya watu kufanya safari ya hijja, na hivyo kutafuta namna ya kukuza vipato vyao kidogo kidogo kwa muda flani
  • Kuwepo na fursa mbalimbali ambazo zimekuwa zikitangazwa katika vyombo mbali mbali na watu kupata hamu ya kuwekeza.

Lakini uwekezaji wa mtu mmoja mmoja umekuwa ni mgumu kutokana na mahitaji ya vyanzo vya mitaji ya kuwekeza kuwa viko juu kidogo ya uwezo wa watu wengi, na hivyo kufikiria njia bora ni kufanya uwekezaji wa pamoja (collective investment)

Je, nini faida za kuwekeza kwa pamoja?

  • Inapunguza mahitaji ya mtaji ya mmoja mmoja kwa kuwa sasa fedha zinaweza kukusanywa kutoka watu wengi na kupata kiwango kikubwa cha kuwekeza
  • Uwekezaji wa pamoja unapunguza gharama za moja kwa moja za uwekezaji kama vile gharama za kulipa washauri wa uwekezaji, wanasheria, na hata gharama za mamlaka husika
  • Uwekezaji wa pamoja pia unasaidia kupungua kiasi cha hasara (risk exposure) ambacho kinaweza kupatikana katika uwekaji huo (risk pooling).

Njia zipi zitumike kusaidia uwekezaji wa pamoja?

Zipo njia na mifumo mingi ambayo inayoweza kusaidia jamii kuwekeza kwa pamoja, kuanzia idadi wa watu 10 hadi watu mamilioni.

Njia hizi ni pamoja na zifuatazo:

Kuanzisha kampuni ya uwekezaji

Njia hii inawataka wahusika kusajili aina ya kampuni (investment holding company) ambayo itakusanya fedha toka kwa watu, na kila mtu atakuwa mwana hisa wa kampuni hiyo husika.

Kampuni itaajiri watu wachache wataalamu ili kuisimamia kampuni hiyo, na wanahisa wote watafaidika kupitia gawio ambalo kampuni itatoa kila mwaka. Ila ni muhimu kufahamu kuwa kampuni itaweza tu kutoa gawio kama kuna faida.

Kampuni hii inaweza kutumia mfumo kama vile Shirkat-ul-Milk au Shirkat-ul-Aqd, inategemea na aina ya kampuni na uwekezaji mnaotaka kufanya

Kuwekeza kwenye mradi maalumu

Njia nyingine ni kuwekeza kwenye mradi fulani bila kuanzisha kampuni, na bila kuwa mwanahisa. Katika mfumo huu, mtu mwenye mradi anaweza kuwa mwingine, na wawezekaji wakawekeza katika mradi huu kwa kipindi maalum tu, na kwa makubaliano maalumu.

Katika njia hii, mwenye mradi atawajibika kuendesha na kusimamia mradi huo, na kuleta gawio la faida kwa wawekezaji, pamoja na kurudisha mitaji yao. Mfumo huu unaweza kutumia njia ya Mudaraba au hata Murabaha kama watu hawa watatoa pesa zao kama mkopo.

Ili kurahisha njia hii, kuna njia zinaweza kutumika kama vile ‘crowdfunding, ambayo inasaidia pesa kukusanywa kirahisi kwa njia ya mtandao kutoka kwa watu wengi hata wakiwa katika maelfu.

Mfuko wa uwekezaji (investment fund/mutual fund)

Katika njia hii, wawekezaji wanaweza kuwekeza kupitia mfuko maalumu wa uwekezaji. Mfuko huu unaanzishwa na mtu au watu wachache ambao ni wataalamu wa mambo ya uwekezaji, na kisha kukusanya fedha toka kwa wawekezaji wengi na kuziwekeza fedha hizo. Katika mfumo huu pia, wawekezaji wanakuwa siyo wanahisa ila wanaweka fedha zao moja moja katika mfuko husika, na linakuwa ni jukumu la msimamizi wa mfuko huo kutafuta njia za kuwekeza fedha hizi.

Mfano tunavyoona kampuni ya UTT inavyofanya. Mara nyingi mifuko hii inawekeza katika maeneo kama vile soko la hisa, hatifungani, na maeneo mengine katika masoko ya fedha. Muhimu tu maeneo hayo ya uwekezaji yawe yanakubalika kisharia.

Mtandao wa wawekezaji (investment network)

Hii ni njia nyingine ya kuwekeza kwa pamoja ambapo wawekezaji wanajiunga na mtandao fulani kama wanachama, na mtandao huo unawasaidia wanachama wake kuyafahamu na kuwekeza katika maeneo mbali mbali.

Kazi za mtandao zinakuwa ni pamoja na kutafuta fursa za uwekezaji, kuzifanyia tathmini fursa hizo, na kuandaa mfumo rahisi ili wanachama wake waweze kuwekeza.

Katika mfumo huu, msimamizi wa mtandao hachukui pesa za wanachama, ila wanachama wenyewe watawekeza moja kwa moja kwenye fursa husika.

Mfano wa njia hii ni mtandao uliopo sasa Tanzania unaojulikana kama Shirkah Investors Network ambao unatarajia kuwasaidia wanachama wake kupata fursa mbali mbali za kuwekeza.

Klabu ya uwekezaji (investment club)

Hii ni njia inayotumika kwa watu ambao wana mahusiano fulani, aidha ni ndugu, marafiki, au watu wenye kitu kinachowaunganisha (common bond).

Mfumo huu unatumika kuendeleza umoja wao na pia kuwasaidia kuwekeza pamoja. Wanaweza kuamua kusajilia klabu yao kama kampuni na wote wakawa wana hisa, au wanaweza kufanya uwekezaji kwa kukusanya pesa pale tu panapokuwa na fursa

Show More
Back to top button
Close
Close