3. Kitabu Nilichokisoma

Mwanamke wa Kiislamu ajiandaaje kwa Ramadhan? sehemu ya 2

Kujiandaa kwa Mwezi wa Ramadhan

Dada yangu katika imani, katika kujiandaa kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan tunapaswa kujitakasa kwa ajili ya Allah (tazkiyyah). Haiwezekani ukafuzu kuwekwa huru na moto wa Jahannam na kupata msamaha wa Allah katika mwezi mtukufu wa Ramadhan huku moyo wako umeghafilika na kushughulishwa na pumbao na kuitafuta dunia. Hivyo basi, Pia, tumia kila ulicho nacho kufanya juhudi za kujiandaa kwa ajili ya kuutumia mwezi huu ili upate kufaulu na kupata radhi za Allah.

Ramadhan ni kama mashindano yoyote yale ambayo kuna kufaulu na kufeli. Mwenye kutaka kushiriki katika mashindano hayo, na kushinda, lazima afanye mazoezi kujiweka tayari kupambana na washindani wengine. Hayo ni katika mambo ya kidunia ambayo mshindi hupewa zawadi zenye kuisha kama medali au pesa; basi iweje tutegemee kupata zawadi ya thamani ya pepo na akhera yenye kubakia milele bila maandalizi? Bila shaka maandalizi makubwa yanahitajika kupata ushindi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Ewe dada yangu kipenzi, maandalizi kwa ajili ya mwezi wa Ramadhan huanzia ndani ya mwezi mtakatifu wa Rajab. Rajab ni mwezi wa kuzitoharisha nyoyo ili ziepukane na maasi. Anasema Ibnul Qayyim Al-Jawziyyi (Allah amrehemu): “Utoharishe moyo wako dhidi ya madhambi kwani mafanikio hayapatikani isipokuwa ndani ya moyo ulio tohara. Je huoni mkulima anaandaa ardhi yenye rutuba na anaimwagia maji na kuitifua na kila akiona jiwe au kila chenye kuukwaza mmea hukiondoa kisha ndiyo anapanda mbegu na kuilinda dhidi ya hatari zote.” (Kitabu ‘Mawaaidh’ cha Ibn Jawziyyi).

Wajibu wa kwanza
Basi ewe dada yangu mtukufu, Rajab imeshamalizika na sasa tuko ndani ya mwezi wa Shaaban. Anza kuanzia sasa kujiandaa kwa ajili ya mwezi wa Ramadhan bila kuchelewa. Anza kuanzia sasa hivi unaposoma makala hii. Achana na madhambi na fanya haraka kukimbilia msamaha wa Mola wako Mtukufu. Fanya haraka kumlilia Allah na ufanye toba ya kweli kabla ya mwezi wa Ramadhan kwa madhambi uliyoyatenda huko nyuma.

Tubia kwa Allah kwa kila dhambi kubwa au ndogo, uijuayo na usiyoijua. Irejee ile dua ya kipenzi cha Allah Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) isemayo: “Allwaahumma ighfir lii khatwiiatiy, wa jahliy, wa israafiy fii amriy, wa maa anta aghlam bihii minniy. Allwaahumma ighfir lii hazzliy wajiddiy, wa khatwaiy, waghamdiy, wa kulla dhaalika ghindiy. All-waahumma ighfirlii maa qaddamtu wamaa akkhartu wa maa asrartu wa maa aghlantu wa maa anta aghlam bihii minniy anta Al-Muqaddim wa anta Al-Muakkhir wa anta ghalaa kulli shay-in qadiir.” (Muslim).

Tafsiri ya dua hii inasema: “Ewe Mola wangu nisamehe makosa yangu na ujinga wangu na kupituka mipaka (yako) katika mambo yangu na unayoyajua juu yangu. Ewe Mola wangu nisamehe niliyoyafanya kwa mzaha na niliyofanya kwa msisitizo, na makosa yangu ya bila kujua na makosa ya kukusudia na kila moja katika hayo niliyonayo. Ewe Mola wangu nisamehe makosa niliyotanguliza na ambayo bado sijayatenda na niliyoyafanya kwa siri na niliyoyafanya kwa dhahiri na yote uyajuayo juu langu. Wewe ni Mwenye Kutanguliza na wewe ni Mwenye Kubakisha nyuma na wewe unauwezo juu ya kila kitu au jambo.”

Ewe dada yangu, hiyo hapo dua aliyoiomba Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) ambayo ni ukamilifu wa kumuomba Allah Ta’ala msamaha. Basi, usifanye ajizi. Dumu nayo dua hiyo kuanzia sasa na katika uhai wako wote. Katika dua hiyo, unakiri upungufu wako, na kufanya hivyo kunaweza kuwa sababu za kukubaliwa toba yako na Mola wako Mtukufu. Ihifadhi dua hii dada yangu kipenzi na uirudierudie kila mara hasa ukiwa katika sijda zako siku nzima.

Vilevile, uombe toba na msamaha wa Allah Ta’ala na ujinyenyekeze kwake na umuombe kwa unyenyekevu ukisema: “Rabbi ighfir warham wa anta khayru Ar-raahimiyna.” (Qur’an, 23:118), ikimaanisha: “Ewe Mola wangu samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wenye kusamehe.”

Pia, omba kwa dua aliyoiomba Nabii Yunus alipokuwa ndani ya tumbo la samaki na useme: “Laa ilaaha illa anta subhaanaka inniy kuntu mina dhwaalimiyna,” (Qur’an 21:87), ikimaanisha: “Hakuna Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa wewe umetakasika hakika mimi nilikuwa katika wenye kuzidhulumu nafsi zao.” (Qur’an 21:87).

Dada yangu kipenzi, leo nikuache hapa na wajibu huu wa kwanza wa maandalizi ya kuuelekea mwezi wa Ramadhan. Jipinde kuzisoma dua hizi ukitaraji toba kutoka kwa Allah.

Huku ndiko kuutakasa moyo ili uwe ‘qalbun saliimum’ yaani moyo uliosalimika kutokana na madhambi na ghadhabu za Allah. Lakini pia, tambua kwamba toba pekee haitoshi. Toba lazima iendane na matendo mema. Matendo mema ndiyo yanayozivuta huruma za Allah Ta’ala.

Miongoni mwa matendo mema ni kijibidiisha na sala, swaumu, kusoma Qur’an na kuwafanyia wema wanadamu, sambamba na kumuabudu Allah kama vile hatujapata kumwabudu huko nyuma. (Itaendelea in shaa Allah)

Show More
Back to top button
Close