4. Jamii

Kamari: Hawajui uharamu wake au uasi?


Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaocheza kamari au inayoitwa michezo ya kubahatisha katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa miongoni mwa washiriki wakubwa wa michezo hii ni baadhi ya Waislamu, licha ya ukweli kuwa dini yao imeharamisha michezo hiyo, kama ilivyokuja katika Qur’an, pale Mwenyezi Mungu aliposema:

Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.”

Ushahidi wa ongezeko la baadhi ya Waislamu wanaocheza kamari upo wazi, hasa mitaani ambako ofisi za michezo hiyo ipo. Katika ofisi hizo, vijana wengi wanaoonekana kucheza ni wakina Rashid, Yusuf, Abdallah, Juma, Sofia na mfano wa hao. Ushahidi mkubwa zaidi unaothibitisha kuwa baadhi ya Waislamu wanacheza kamari unaopatikana katika majina ya washindi wanaotangazwa kila siku, ambapo kuna majina mengi tu yanayoashiria kuwa baadhi ya washindi hao ni Waislamu.

Ukiacha wachezaji kuna kundi la wahamasishaji wa michezo hiyo, ambao baadhi yao ni vijana watangazaji maarufu wa redio na televisheni. Katika vipindi vyao mbalimbali, utawasikia vijana hao wakisifu na kuhimiza watu kucheza michezo ya kamari inayotokana na makampuni yaliyowaajiri.

Kutokana na hali hiyo ya kusikitisha, swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa na wachambuzi wengi wa mambo ya dini, ni je, Waislamu wanaocheza kamari hawajui uharamu wa michezo hiyo au wameamua tu kuasi? Katika kulijibu swali hilo, gazeti Imaan limewahoji wadau mbalimbali ili kusikia maoni yao. Miongoni mwa waliohojiwa ni vijana wa Kiislamu ambao wamewahi kucheza au wanaendelea kucheza kamari mpaka sasa.

Umaskini?

Musa Issa, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam ni mmoja wa vijana waliowahi kucheza kamari, ambaye yeye binafsi amesema alikuwa mshiriki wa michezo hiyo, hasa kwenye kamari ya kubashiri matokeo ya michezo, ingawa alikuwa akifahamu kuwa ni dhambi kufanya hivyo.

Niliwahi kubeti (kucheza
kamari) miaka mitano nyuma. Nilikuwa najua kuwa ni dhambi ila mtu unacheza kwa ajili ya kusaka pesa za ubwete,” anasema Issa na kuongeza kuwa hali ni hiyohiyo kwa vijana wengi.

Kwa mujibu wa Issa, ukitaka kujua Waislamu wanaocheza kamari wanafahamu kuwa ni haramu na ni dhambi angalia katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo wengi huacha kucheza.

Kamari ni kama zinaa, pombe na dhambi nyingine. Vijana wanajua lakini kuendekeza umaskini na tamaa vinawafanya watafute pesa kwa njia yoyote, ikiwemo kamari,” alisema Issa.

Naye Hamza Hadd ambae ni miongoni mwa wapenzi wakubwa wa mpira wa miguu anasema amekuwa akiwaona vijana wengi wa Kiislamu wakishiriki kamari hali ya kuwa wanajua kuwa michezo hiyo ni haramu katika Uislamu.
Mimi binafsi sichezi ila nimekuwa nikiwaona vijana wengi tu wa Kiislamu ambao wanajua kamari ni haramu ila ukifuatilia mazungumzo yao wanaonekana kusukumwa zaidi na tamaa ya pesa za haraka haraka,” anasema Hadd. Aliongeza kuwa suala la umasikini na kutaka mafanikio ya haraka haraka ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vinavyosababisha watu wengi wakiwemo Waislamu kuingia kwenye michezo ya kamari.

Kauli za masheikh

Kwa mujibu wa Sheikh Hashim Rusaganya, Mlinganiaji wa dini ya Kiislamu hapa nchini, asilimia 95 ya vijana wa Kiislamu wanashiriki michezo hiyo haramu. Ni kwa kuona kuwa kamari ni janga kubwa hapa nchini, Sheikh Rusaganya amesema juhudi zinahitajika ili kupambana na hali hiyo.

Moja kati ya mambo yaliyopendekezwa na Sheikh Rusaganya, ni taasisi na jumuiya za Kiislamu kuendesha semina za mara kwa mara za Maimamu wa misikiti kwa lengo la kuwapa mbinu na mikakati ya jinsi ya kuwalingania Waumini wao waache kushiriki michezo ya kamari.

Sheikh Rusaganya alitaka semina hizo zifanyike mara kwa mara zikiwalenga maimamu ndani ya misikiti ili nao waende katika maeneo zinapochezwa kamari kulingania vijana.

Ni kweli Masheikh hawawezi kwenda baa, hawawezi kwenda kwenye nyumba za kuchezeshea kamari, lakini haya mazingira ni lazima wayazoee. Lazima tujichanganye na hawa watu, tusigombane nao, tuseme nao, tucheke nao na tufurahi nao kwa njia ya utani na mazungumzo, kwa kufanya hivyo kuna mambo mengi mabaya tutayaondoa,” alisema Sheikh Rusaganya.

Naye, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum amesema kuwa tatizo la kamari hapa nchini ni kubwa mno na kwamba mbinu za kisasa za kilinganiaji zinahitajika ili kukabiliana na hali hiyo. “Vijana wengi wa Kiislamu hawajui kwamba kamari ni haramu kutokana na michezo hiyo kupambwa kwa majina mazuri na yenye kupendeza. Ni kwa sababu hii ndio utawaona watu wengi wanashiriki,” alisema Sheikh al-Hadi na kuongeza: “Wengi wanaichukulia kamari kama mchezo wa bahati nasibu kwa hiyo wao wanabahatisha tu.

Aina za kamari

Utafiti uliofanywa na gazeti hili umeonesha kuwa kutokujua kamari na kuamua kuasi tu kwa tamaa, zote mbili ni sababu za vijana wa Kiislamu kucheza kamari, licha ya kuwa ni moja kati ya dhambi kubwa. Moja kati ya mambo yanayowafanya vijana wasijue kuwa wanachofanya ni haramu ni ulaghai unaofanywa na wachezeshaji ambapo wamekuwa wakiita michezo hiyo kwa majina mbalimbali ya kuvutia.

Mbaya zaidi ni kuwa, makampuni ya kamari yameingia ubia na vyombo vya habari kuwatangazia matangazo yao ya kamari ili mchezo huo haramu kidini uonekena ni njia nzuri ya kujiongezea kipato; huku kwa upande mwingine kila watu wanavyozidi kucheza ndivyo vyombo hivyo vya habari vinavyopata mgao wa matangazo kutoka makampuni hayo ya kamari.

Hata hivyo ukweli ni kuwa, michezo ya kamari ni mibaya kiuchumi na inafilisi watu. Wanacheza maelfu, anashinda mmoja. Kisha vyombo vya habari vinamtumia kumtangaza sana ili kuwatia mshawasha wengine wacheze zaidi wakitegemea kubahatika kumbe wanapoteza fedha, kulaaniwa na kuwafaidisha mabwanyenye,”

Kwa sasa katika michezo ya kamari inayotamba zaidi ni pamoja na ile inayohusisha kutabiri matokeo ya mechi za michezo mbalimbali, kutabiri namba za bahati, michezo inayohusiha karata nk. Yote hii ni haramu kwa mujibu wa Uislamu.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close