4. Jamii5. Fatawa

Hukumu, fadhila na thawabu za siku ya Arafa

Kesho ‘InshaaAllah’ tutaipokea siku kubwa na tukufu, nayo ni ‘Yaumul Mash-huud’ au siku ya Arafa kama tulivyozoea kuiita. Siku hii ndiyo kilele cha ibada ya Hijja, na siku inayofuata ni siku ya Idil Adh’ha ambapo mahujaji huanza rasmi ibada ya kuchinja. Siku mbili hizi (siku ya Arafa na Idd Aldh’haa) zina hukumu na umahususi wake kwa kila Muislamu.

Katika makala hii, tutagusia baadhi ya hukumu zinazomhusu Muislamu katika siku mbili hizi, ambazo ni muhimu kuzijua ili aweze kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa weledi, muongozo na nuru. Zaidi tutazungumzia hukumu zinazohusiana na funga ya siku ya Arafa.

Kwanza, ieleweke wazi kuwa, funga au swaumu ni ibada yenye faida nyingi kwa mfungaji, hivyo Muislamu anapaswa kuifuatilia kwa kina funga husika ili aweze kuitekeleza kikamilifu, hasa ikizingatiwa kuwa funga za sunna zina fadhila kubwa mbele ya Allah. Mwenyezi Mungu anasema: “Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.” [Qur’an, 2:184]. Allah akanena tena: “Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.” [Qur’an, 22:77].

Kila mtu anahitaji kufanya mambo mema na mazuri kwa nia ya kujipendekeza (kujikurubisha) kwa Mwenyezi Mungu na kujiongezea thawabu na malipo kwani thawabu za Allah hazina mipaka. Kwa kuzingatia hayo, yafaa kila Muislamu ajibidiishe katika kutenda amali nyingi za heri kwa kutaraji kupata moja ya mambo mawili; mosi, kujikurubisha kwa Allah na kutenda heri, na pili kuziba mianya inayojitokeza katika ibada. Bila shaka kila mwanadamu ni mkosa, na kwa kuwa kila mtu anakosea, Allah Mtukufu ametuletea ibada za wajibu na sunna ikiwamo funga ya Arafa kwa lengo la kuziba upungufu na kujiongezea ujira.

Fadhila za kufunga siku ya Arafa

Arafa ni ile siku ya tisa tokea siku iliyoandama mwezi wa Dhul-Hijja duniani. Wanazuoni wamekubaliana kwamba, funga ya siku ya Arafa ndiyo funga bora mno katika siku za kufunga. Kulifafanua hilo, Mtume wa Mungu (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) amesema: “Funga ya siku ya Arafa nataraji kwa Allah ifute dhambi za mwaka uliopita na ujao.” [Muslim]. Kifupi ni kwamba, funga ya siku ya Arafa inampadisha mtu daraja, inamuongezea mema na kufutiwa dhambi.

Siku ya Arafa inafuta dhambi za aina gani?

Kiujumla, funga ya siku ya Arafa ni sunna kwa wasiokuwa Hijja, na hii inatokana na ujira mkubwa wa kufutiwa dhambi za miaka miwili upatikanao katika siku hii. Ama kwa mahujaji, wao si sunna kufunga siku hii. Ama dhambi zinazosamehewa katika siku ya Arafa ni zile ndogondogo na siyo dhambi kubwa. Ili mtu asamehewe ni sharti aache dhambi kubwa kama ilivyosemwa katika Aya hii: “Mkiziepuka dhambi kubwa mnazokatazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.” [Qur’an, 4:31]. Kadhalika, katika neno lake Mtume wa Allah (rehema na amani ya Allah iwe juu yake): “Sala tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, na Ramadhan hadi Ramadhan, ni kafara ya yaliyojiri kati yake, iwapo dhambi kubwa zitaepukwa.” [Muslim].

Siku ya Arafa inapokutana na siku ya Ijumaa au Jumamosi

Inapotokea siku ya Arafa kusadifiana na siku ya Jumamosi kama ilivyo kwa mwaka huu, hapo inajuzu/inaruhusiwa kufunga siku ya Arafa pekee katika siku ya Jumamosi, na lile katazo lililokuja kukataza kufunga, ni kwa funga isiyokuwa na sababu, au inayolenga kutukuza siku fulani nk.

Ama kwa mtu anayefunga siku ya Arafa kwa sababu ya himizo la Mtume na kutekeleza sisitizo la kisharia, huyo haikatazwi kufunga katika siku iliyokatazwa, na kama atafunga siku moja kabla itakuwa bora. Hii ni kwa kuzifanyia kazi Hadithi zote mbili tulizozitaja.

Hapo, mtu atafunga siku moja kabla, kwa sababu kufunga siku moja baada (yaani siku ya Idd ya Adh’haa) haiwezekani. Kufunga siku ya Idd kisharia ni haramu kwa Waislamu wote (mahujaji na wasio mahujaji) kama ilivyokuja katika Hadithi ya Abi Said (Allah amridhie) aliyesema: “Mtume amekataza kufunga siku mbili; Siku ya Idil fitri, na siku ya Idi Nnahri (ya kuchinja).” Katazo hili linamaanisha kwamba ni haramu kufunga swaumu ya aina yoyote katika siku zilizokatazwa.

Sambamba na hilo, pia hairuhusiwi kufunga siku ya Jumatatu, Alkhamisi, siku nyeupe nk iwapo zitasadifu siku za Tashriiq (siku ya mwezi 11, 12, na 13 Dhul-Hijja) kwa kuwa Mtume amesema: “Siku za Tashriiq ni siku za kula, kunywa na kumtaja Mwenyezi Mungu.”

Hata hivyo, katazo hili halimhusu Hujaji aliyenuia Hijja ya Tamatui na Qirani kisha akakosa mnyama wa kuchinja. Huyu anaruhusiwa kufunga ndani ya siku kumi za Hijja kwani anatakiwa kufunga siku tatu ndani ya siku za Hijja na siku saba wakati atakaporejea nyumbani.

Mwisho, tunamuomba Allah atuwafikishe kutenda yaliyo mema kwa fadhila zake, atuelimishe, na atukirimu elimu yenye tija, na atujaalie tuwe miongoni mwa waongozaji na si wapotoshaji.

 

 

Show More

Related Articles

Back to top button
Close