4. Jamii

Hatua saba za kujipangia bajeti binafsi

Katika zama hizi za hali ngumu ya kiuchumi, kila mmoja anazungumzia kuwa mwangalifu zaidi na fedha. Kwa mtazamo wa Kiislamu, bila kujali hali ya uchumi, ni muhimu kuwa muangalifu na matumizi na kuweka akiba ili kuepuka israfu, kuweza kukimu familia, kuzuia madeni kadri inavyowezekana na kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za hisani.

Moja ya tabia muhimu zaidi ambazo wote tunapaswa kuwa nazo ni kufuatilia bajeti (budget tracking). Kwa baadhi yetu, ni kazi ngumu kufuatilia wapi fedha zao zinaenda, lakini leo nataka kuwapa mbinu ya kuifanya kazi hiyo kuwa rahisi na isiyo na maumivu, ikihitaji dakika chache tu kwa wiki. Bila kujali ukubwa au udogo wa kipato na matumizi yako, hii ndiyo njia bora zaidi ya kukaa kwenye mstari unaofaa.

Hatua ya 1:

Pata taarifa mpya ya akaunti zako zote kutoka kwenye benki unakohifadhi fedha zako,au ziangalie kupitia huduma za kibenki mtandaoni (online banking). Pia, unaweza kuzipata taarifa hizi kwa kwenda tawi la benki yako na kuziulizia.

Benki nyingi nchini huwa zinatoa taarifa (statements) hizi bure, ili mradi tu usiwe unaziulizia kila wakati. Wanaweza kukupa mpaka za miezi mitatu bure.Huduma za kibenki mtandaoni (Online banking) ndiyo chaguo bora zaidi, kwa sababu unaweza kuangalia miamala ya akaunti zako zote wewe mwenyewe kwa wakati unaotaka.

Moja ya vipengele muhimu vya ‘online banking’ ni kurahisisha malipo ya bili. Unaweza kuingia kwenye akaunti yako na ukapata taarifa zote za bili zako zinazopaswa kulipwa kama vile rehani (mortgage), huduma na mikopo na ukafanya malipo hapo hapo.

Hii inaweza kusaidia kuepuka kuchelewesha malipo na kuokoa fedha kwa ajili ya gharama za posta. Mabenki mengi yanatoa huduma za ‘online banking’ na malipo ya bili bure. Kama benki yako haifanyi hivyo, basi unapaswa kufikiria kuhamia benki nyingine.

Huduma za kibenki mtandaoni ni salama kama vile ilivyo kupitia barua; uwezekano wa wizi wa utambulisho kupitia ‘online banking’ unafanana na ule unaojitengeneza kwa kutuma bili zako kupitia ofisi ya posta. Hata hivyo, hakikisha unatafuta alama ya usalama ya kufunga ‘browser’ yako ya ‘internet’ kila wakati unapofanya ‘online banking’ au unaponunua kitu kupitia njia ya mtandao.

Hatua ya 2:

Kusanya mapato yako yote ya mwezi kutoka vyanzo vyote – mshahara, ujira wa saa, fedha kutoka familia, posho na kadhalika. Kama kipato chako siyo kile kile kila mwezi, chukua wastani wa kipato chako cha mwezi kama kipato halisi kwa ajili ya malengo ya bajeti.

Hatua ya 3:

Pitia Kila senti inayotumika kwenye taarifa za akaunti zako (statements) na ziweke katika makundi. Kama ni bili inayotumika kila wakati (recurring bill) iweke yenyewe kama kundi. Mfano wa makundi ni pamoja na mortgage (dhamana ya mkopo), credit card, mafuta ya gari, bima, posho/fedha za kutumia, vitabu, huduma za internet, umeme, mahitaji ya nyumbani na kadhalika.

Pia, zingatia kuingiza bili ambazo haziji kila mwezi, na badala yake zinakuja kwa robo mwaka, nusu mwaka au mwaka mzima. Bili hizo ni kama vile malipo ya bima mbalimbali, kodi za mali, usajili wa gari, kuzoa taka na nyinginezo. Vile vile, usisahau kuingiza akiba. Unaweza kutaka kuvunjavunja akiba zako katika makundi kwa malengo. Ni wazo jema kuweka akiba kwa ajili ya kuhudumia nyumbani na matengenezo ya gari na pia kwa ajili ya dharura na kusafiri.

Kama huna akaunti tofauti kwa ajili ya akiba, basi ni vizuri kufungua. Utafiti unaonyesha kwamba watu wenye akaunti tofauti ya benki kwa ajili ya akiba ndiyo wanaofanikiwa zaidi katika kuweka akiba. Kama huna akaunti ya akiba, unaweza ukaifungua kwa urahisi tu.

Hatua ya 4:

Tafuta jumla ya kile unachotumia kwenye kila kundi kwa kila mwezi kwenye taarifa zako za akaunti. Halafu, kama uliunda kundi lolote jipya kama akiba,tenga kiasi cha mwanzo cha lengo
kwa kila moja. Kwa bili ambazo zinakuja mara chache kuliko kwa mwezi, unapaswa kukokotoa au kadiria kiasi gani utadaiwa kwa mwaka na gawanya kiasi hicho kwa 12 na tumia kiasi unachopata.

Kwa mfano, unaweza kuona kwamba, unatumia wastani wa shs 250,000 kila mwezi kwa chakula, shs 300,000 kamili kila mwezi kwa ajili ya pango, na kwamba unataka kuweka akiba Shs 50,000 kila mwezi, na kwamba bili yako ya kuzoa taka ni shs 60,000 kila baada ya miezi mitatu, kwa hiyo unahitaji kuweka bajeti ya Shs 20,000 kila mwezi kwa ajili hiyo.

Hatua ya 5:

Ongeza jumla ya kila kundi kutoka hatua ya 4 na linganisha jumla hii kwenye kipato chako cha mwezi ulichokipata kwenye hatua ya 2. Kama jumla hii ni kubwa kuliko kipato chako, basi lazima urekebishe kila kundi mpaka kiasi katika sehemu hizo mbili ziwe sawa.

Kama matumizi yako yako nje ya mstari, au unakabiliana na upungufu wa ghafla wa kipato, unaweza hata ukahitaji kuondoa baadhi ya makundi ili kufanya namba hizo mbili zilingane (balance). Watu wengi wanaona wanaweza kuondoa gharama za simu za mkononi, kulipia ada ya ving’amuzi na kiasi cha bajeti yao ya chakula. Haishauriwi kuondoa kabisa uwekaji wa akiba katika bajeti yako au matumizi muhimu ingawa vipengele hivyo vinaweza kupungua kama uko katika hali ngumu.

Hatua ya 6:

Weka bajeti yako katika karatasi (spreadsheet). Nashauri sana njia hii kutokana na urahisi wake wa kufanya na upatikanaji. Kwa wale wanaoweza kuipata programu ya ‘Foxway Budget Tracker Spreadsheet’ kwenye Kompyuta ni bora zaidi. Unaweza kuifanya ikidhi mahitaji yako.

Ingiza kile hasa unachotumia katika mwezi fulani kwenye ‘spreadsheet’ hii. Tumia ‘online banking’ kama unaweza au kila unaponunua au kutuma bili ingiza kwenye ‘spreadsheet’ siku ile ile kwenye kundi sahihi. Ukitaka, fanya hivi mara moja kwa wiki, lakini hakikisha kwamba hukosi kurekodi kila ulichotumia.Bajeti yako haitasaidia kitu kama siyo sahihi. Programu hii ya Kompyuta itakuonyesha wapi umetumia zaidi, wapi kuna ziada, upungufu na kadhalika. Usisahau kusevu faili lako la bajeti kila unapofanya mabadiliko.

Hatua ya 7:

Kila baada ya muda fulani, tathmini matumizi yako ukilinganisha na kile ulichobajeti. Kama kuna makundi ambayo kila wakati unatumia zaidi, unaweza kuhitaji kuongeza bajeti ya makundi hayo kwa kuondoa fedha kutoka makundi mengine, au unaweza kuhitaji kujidhibiti wewe mwenyewe katika matumizi ya makundi hayo.

Halkadhalika, kama kuna makundi ambayo unatumia kidogo kuliko ulivyobajeti, basi unaweza kupunguza bajeti yake na kuweka ziada ile mahali pengine. Fuata hatua hizo saba, mpangilio wako wa fedha utaenda vizuri, hata kama hali yako ya kifedha itabadilika Insh’Allah!

Kama huna akaunti tofauti kwa ajili ya akiba, basi ni vizuri kufungua. Utafiti unaonyesha kwamba watu wenye akaunti tofauti ya benki kwa ajili ya akiba ndiyo wanaofanikiwa zaidi katika kuweka akiba.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close