5. Fatawa

Wanazuoni Waaswa Kutowakatisha Tamaa Watendao Dhambi

Wanazuoni wa Kiislamu nchini wametahadharishwa wasiwakatishe watu tamaa ya kusamehewa na Mwenyezi Mungu kutokana na maasi wanayoyatenda na badala yake wawaelekeze watu kufanya toba. Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini (Hay-atul Ulamaa), Sheikh Ibrahim Ghulaam, amebainisha hayo wiki iliyopita wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa Mwinyimkuu uliopo Magomeni jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ghulaam alisema, wanazuoni wana nafasi kubwa katika Uislamu na jamii hivyo ni muhimu wakatumia elimu waliyoipata kuitahadharisha jamii juu ya makosa yanayotendeka na athari zake pamoja na kuwabainishia mambo wasioyajua kuhusu dini yao. “Wanazuoni wanaweza kuwa madaktari bora wa tabia za watu hivyo ni vema wakawa na utaratibu wa kuwakaribisha wafanyao makosa na kuwaelekeza katika njia ya sawa (dini ya Mwenyezi Mungu) na siyo kuwakaripia na kuwafukuza,” alisema Sheikh Ghulaam.

Sheikh Ghulaam alisema kuwa moja ya majukumu na wajibu wa wanazuoni wa Kiislamu ni kuilea jamii kwa kuwaelekeza watu kutoka kwenye hatua ya ufahamu mdogo wa kuijua dini na kuwapeleka katika kiwango kizuri na bora. Kutokana na hali hiyo, wanazuoni wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa ufafanuzi juu ya uhalali na uharamu wa mambo mbalimbali ili jamii iweze kufahamu sheria za dini kwa usahihi na ukamilifu wake.

“Wanazuoni ndiyo wenye mamlaka ya kuiongoza jamii na kutoa hukumu za kisheria (fat-wa), na si kama ilivyozoeleka na watu wengi kwamba Muislamu yeyote anaweza kutoa fat-wa,” aliongeza kusema. Sheikh Ghulaam aliwaambia waumini hao kuwa elimu ni katika mambo machache yapaswayo kuhusudiwa, hivyo wana wajibu kuitafuta kadiri wawezavyo kwa kuwa hilo ni jambo la kwanza aliloamrishwa Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie).

Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close