5. Fatawa

Ujue uwalii na mawalii

Katika toleo lililopita tulitaja baadhi ya sifa za mawalii wa Allah ikiwemo: imani, uchamungu, kumhofu Allah, tabia njema, upendo, kujitolea kwa ajili ya maslahi ya wengine na kujiweka mbali na maasi ya maneno na matendo.

Jambo linalofuata kwa umuhimu katika mada yetu hii ni kwanza ni kumkumbusha msomaji kwamba duniani kuna mawalii wa Allah na mawalii wa shetani. Kwa hiyo ni vyema kujua vigezo na tofauti kati ya makundi haya mawili kwa usalama wa imani, itikadi na matendo ya Muumini katika safari yake ya kumuelekea Allah.

Amesema Ibn Taimiya (Allah amrehemu): “Ikishakueleweka kwamba miongoni mwa watu wamo mawalii wa Allah na wapo mawalii wa shetani, hapo inapasa ijuilikane pia tofauti baina yao kama alivyowatenganisha Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie).”

Haja ya kuyajua vyema makundi haya inazidi kubainishwa katika aya ifuatayo:

“ Allah ni walii (kipenzi) wa waumini, huwatoa katika giza na huwapeleka katika nuru. Na waliokufuru, walii wao ni shetani. Huwatoa katika nuru na kuwapeleka gizani, hao ndiyo watu wa motoni humo watakaa milele.” [Qur’an 2: 257].

Katika aya tuliyoirejea hapo juu, licha ya kutajwa aina mbili za mawalii, tumejifunza pia kwamba, kuna waliomfanya shetani kuwa ndiye kipenzi chao wakiongozwa na waliomkufuru Mwenyezi Mungu. Shetani amewapoteza watu hao kutoka katika njia sahihi ya maisha na mwisho wao ni motoni.

Kwa upande mwingine, vipenzi wa Allah wamebaki ndani ya nuru na muongozo wa Mola wao. Mwenyezi Mungu anawalinda vipenzi vyake hao dhidi ya vishawishi vya mashetani na wafuasi wao na kisha Mwenyezi Mungu atawaingiza peponi.

Kundi la Mtume

Mtume katika hadith ifuatayo anazidi kuweka wazi msimamo wa Uislamu kuhusu mawalii. Abdallah bin Amr bin al-As (Allah amridhie) amehadithia kuwa amemsikia Mtume wa Allah akisema:

“Hakika jamaa wa kina fulani si katika mawalii wangu (niwapendao), lakini mpenzi wangu ni Allah na wema miongoni mwa Waumini.” [Muslim].

Maneno haya matukufu ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) yanaendana kabisa na kauli ya Allah isemayo:

“Kama nyinyi wawili hamkutubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwisha elekea huko. Na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye kipenzi chake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia.” [Qur’an, 66:4].

Tahadhari na wapenzi wa shetani

Chanzo cha uadui ni kuchukia na kujiweka mbali na maagizo ya Allah. Na hizi ndizo sifa na mwenendo wa shetani aliyelaaniwa pamoja na wapenzi wake.

Basi ikiwa walii ni mtu aliye karibu na Allah kwa kumtii na kumuabudu na ambaye mwishowe hujivunia mapezi na ulinzi kutoka kwake; basi ifahamike tu kwamba Mwenyezi Mungu ametahadharisha dhidi ya kujiakaribisha kwa maadui zake kwa sababu hawawapendelei Waumini mema.

Allah Aliyetukuka amesema: “Enyi mlioamini, msiwafanye maadui zangu na maadui zenu kuwa marafiki mkawapa mapenzi ili hali wao wamekwishaikataa haki iliyokujieni, wakamfukuza Mtume na nyinyi kwa sababu tu mmeamini Mwenyezi Mungu mlezi wenu..” [Qur’an, 60:1].

Vipenzi vya shetani ni wale wanaofanya matendo ya kishetani yenye malengo ya kumridhisha kiumbe huyo aliyelaaniwa.

Madai potofu ya uwalii

Mara nyingi watu hujipa uwalii (wakidai kwamba wao ni wapendwa wa Allah) au kuwadhani watu fulani ni mawalii au watawa, licha ya watu hao kuonekana wakizama katika madimbwi ya maasi.

Lakini ukweli unabaki kwamba uwalii unafikiwa kwa kwa kupita njia zake sahihi ambazo ni pamoja na imani, uchajimungu, utiifu na unyenyekevu wa kweli kwa Allah.

Dhana ya kujipachika uwalii ni kongwe sana katika historia ya mwanadamu anayeamini juu ya uwepo Mwenyezi Mungu. Kujipachika huku na kukosea katika kuwajua mawalii kunatokea kwa sababu ya kutumiwa vigezo ambavyo si sahihi.

Katika Qur’an, tunaelezwa kwamba Wayahudi na Wanasara walifikia hatua ya kujigamba eti wao ni wana wa Mwenyezi Mungu na ni vipenzi wake.

Kadhalika, washirikina wa Kiarabu nao walikuwa wakidai kwamba wao ni vipenzi wa Allah kwa vile tu waliishi jirani na Nyumba Takatifu (Ka’aba), lakini Allah akabainisha kwamba wao si mawalii wake kwa vile walikufuru na kuzuia dini kwa kumuudhi Mtume.

Washirikina hao pia waliwatesa wafuasi wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), na mwishowe wakamtoa katika mji aliozaliwa na kukulia (Makka), kama inavyobainishwa katika Qur’an.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na (kumbuka washirikina) walivyokufanyia hila walio kufuru wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe. Wakafanya hila lakini Allah akapangua hila zao, na Allah ni mbora wa kupangua (hila za maadui).” [Qur’an, 8: 30].

Tusome tena aya zifuatazo: “Na Mwenyezi Mungu hakua wa kuwaadhibu na wewe umo pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu si wa kuwaadhibu hali ya kuwa wanaomba msamaha. Na kwa nini Mwenyezi Mungu asiwaadhibu ilihali wanazuia (watu) Msikiti Mtukufu? Wala wao hawakuwa ndiyo walinzi wake, bali walinzi wake hawakuwa ila wachamungu tu. Lakini wengi katika wao hawajui..” [Qur’an, 8:34].

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close