5. Fatawa

Uislamu ulivyomlinda mwanamke katika ndoa za wake wengi

Allah ametuamuru tumlinde mwanamke na tumtendee wema na akaeleza kuwa, watu wote wametokana na mwanaume na mwanamke. “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanaume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.” [Qur’an 49:13].

Licha ya heshima hii aliyopewa mwanamke katika Uislamu, baadhi ya watu hujaribu kupotosha taswira ya Uislamu kuhusu hadhi aliyopewa mwanamke katika Uislamu, huku wakidai Uislamu unamnyima haki na
mwanamke.

Kwa mtazamo wao,Uislamu unambagua mwanamke na kumnyima haki. Pia, wanadai uhusiano wa mwanamke na mwanaume ni wa kikandamizaji na usioleta utulivu na upendo. Pia wanasema, ipo haja ya kuisoma dini upya ili ilingane na wakati na ilinde haki za wanawake, yaani wanajaribu kuzifanyia marekebisho nususi za Sheria ya Kiislamu.

Madai hayo yote si ya kweli kwa sababu awali ya yote,ushahidi unaonesha kuwa, Uislamu unampatia mwanadamu haki zake kiukamilifu, bila kujali jinsia yake. Hakandamizwi, na wala hadhulumiwi yoyote.

Masuala kadhaa yanayohusu wanawake huibua tuhuma dhidi ya Uislamu. Hapa tutajadili machache.

Suala la mwanaume kuwa msimamizi

Mfano ni kipengele cha mwanaume kuwa msimamizi (Qawwam) wa mwanamke. Wapinzani wanahoji haki na mamlaka ya kumsimamia mwanamke, alizopewa mwanaume, pale Mwenyezi Mungu aliposema:

“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake…” [Qur’an 4:34].

Wanaotoa madai haya wamechanganyikiwa na kushindwa kuelewa maana ya usimamizi. Kwa uelewa wao,ukiwa msimamizi ni lazima uwe mkandamizaji, dhalimu na mnyimi!Hapana!

Ukweli ni kuwa, usimamizi unatakiwa uakisi huruma, upendo, na ulinzi kwa mwanamke. Kama ingekuwa huu ni usimamizi unaolenga kumkandamiza mwanamke, mwanaume angekuwa na haki hata ya kupora mali za mkewe au kumzuia kufanya biashara itokanayo na pesa zake mwenyewe.

Kinyume na hivyo, Uislamu unamkataza mwanaume kumkandamiza mwanamke au hata kumlazimisha kubadilisha dini yake. Uislamu unamruhusu mwanaume wa Kiislamu, inapobidi, kuoa mwanamke wa Kinasara au Kiyahudi, na kila mmoja akabaki na dini yake.

Usimamizi, katika Uislamu,unalenga kumfanya mwanaume awajibike katika kuhudumia familia; na ndio asili. Mwanaume anawajibika kufanyakazi, na si mwanamke. Hata hivyo, mwanamke ana uhuru kamili;akipenda afanye kazi, asipotaka halazimishwi.

Suala la wake wengi

Wengine wanapinga sharia ya Kiislamu inayoruhusu mwanaume kuoa
wake wengi, wakidai inamkandamiza mwanamke na kumnyima haki ya heshima na usawa na mwanaume.

Pia,wanadai hiki ndicho chanzo cha migogoro ya kudumu katika ndoa (kati ya mume na wake zake au kati ya wake wenza),jambo linalosababisha migogoro na machafuko kwenye maisha ya familia.

Ni wazi kuwa idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume kwa sababu mbalimbali za kiasili, kijamii, na kadhalika. Sababu za kimaumbile ambazo binadamu hana mamlaka nazo ni wanawake kuzaliwa wengi kuliko wanaume.

Na sababu za kijamii zinarudi kwenye mambo makuu mawili, mgawanyo wa majukumu ya kazi kwa mujibu wa jinsia ambapo wanaume wanafanya kazi nyingi za hatari zinazowaweka katika uwezekano mkubwa wa kufa kuliko wanawake mathalan uaskari na uanajeshi.

Pia, kijamii tunajua mwanaume hawezi kuoa mpaka awe na uwezo wa kumhudumia mkewe kimalazi na makazi na mengineyo, wakati msichana anaweza akaolewa kwa kufikia tu umri wa kubaleghe.

Wingi huu wa wanawake ukilinganisha na wanaume unafanya suala la kuoa wake wengi kuwa ni muhimu.

Pia, hutokea katika maisha ya ndoa vitu vinavyofanya ndoa ya mitala kuwa ni ya lazima mathalan mke kutokuwa na uwezo wa kuzaa au kupata ugonjwa unaomfanya ashindwe kuyamudu maisha ya ndoa.

Uislamu ukaangalia kilicho chema zaidi kwa mke. Badala ya kumpa mke talaka kwa sababu ya ugonjwa au kutozaa, jambo ambalo linamkosesha fursa ya uangalizi na heshima, ikaonekana ni vema akasalia kuwa mke mwema na kuendelea kupata haki zake zote na kumruhusu mume kuoa mke mwingine?

Suala la mirathi

Ukitazama kwa pupa, utadhani Uislamu unamkandamiza msichana kwa kumpa nusu ya anachopewa kaka yake kutoka kwenye urithi wa baba yao, bali Uislamu umewapa wanaume majukumu tofauti na waliyopewa wanawake.

Mwanaume anawajibika kujihudumia na kuwahudumia watoto na ndugu zake ikiwa hawana mtu wa kuwahudumia,wakati sharia haijawapa wanawake majukumu hayo. Mali wanayoirithi kutoka kwa baba zao hubaki kuwa ni mali yake, na hashirikiani na mtu.

Fungu analorithi kijana wa kiume linaweza kupungua wakati wowote kutokana na kuibuka kwa majukumu aliyobebeshwa na Uislamu, lakini fungu la msichana linaweza kuongezeka, kutokana na kupokea mahari na zawadi.

Uislamu umewapa wanawake haki ili nao washiriki katika maendeleo ya nchi yao kama wafanyavyo wanaume au zaidi. Kwa hakika, dini ya Allah ya Uislamu imemuenzi mwanamke na inalinda haki za wanawake.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close