5. Fatawa

Makosa yaliyozoeleka katika biashara

KATIKA ulimwengu wa sasa, kuna makosa mengi ambayo waislamu wamekuwa wakiyafanya. Makosa haya yanapelekea dhambi kubwa na kuondosha baraka katika riziki tunayoitafuta. Katika makala hii, tutataja baadhi ya makosa yanayofanyika.

Kutumia viapo vya uongo kuipamba bidhaa.

Utakuta mtu mwenye muonekano wa kujitambua kidini anauza asali nje ya msikiti. Katika kazi yake hiyo, utamkuta anaapa kuwa, yeye anauza asali halisi na wenzake wanauza asali iliyochakachuliwa. Ukienda kwa wengine, nao wanamsema hivyohivyo, bila kujali kuwa viapo hivyo vinaondosha baraka.

Mfano mwingine. Mtu anapokuja kwako kununua friji, usidanganye eti ni ya Ujerumani au Marekani. Mwambie, kweli inatoka China kwani ndio wasambazaji wakubwa duniani hususan kwa pande hizi za dunia na uchaguzi ubaki kwake mteja aamue aidha atanunua au la.

Kudharau elimu ya biashara katika dini

Wengi katika Waislamu hawajali kutafuta elimu ya miamala ya mikopo, kujua kuhusu sheria za upangaji bei, mauzo ya bidhaa za haramu, michakato ya utoaji zaka na kadhalika. Tunaishi katika Dunia ambayo Waislamu wanatumia nguvu kubwa kusoma elimu ya biashara upande wa mazingira lakini wanapuuza elimu hiyo upande wa dini. Swahaba Umar (Allah amridhie) alikuwa akikataza watu kuuza masokoni bila ujuzi wa sheria na miamala ya halali.

Kuuza bidhaa za haramu

Kosa jingine ni kuuza bidhaa za haramu kama sigara, mirungi na vilevi vingine, magazeti yenye picha za uchi za wanawake, vitabu vyenye kueneza uhuni na ushirikina. Wapo Waislamu wanauza DVD za maigizo ya michezo yenye kuongeza fitna katika jamii. Unaweza toka nje ya msikiti unakuta mtu mwenye haiba ya Uislamu lakini anauza vitabu vya kishirikina na uovu mwingine. Unakuta kitabu mtu kama huyo anauza kitabu kinafundisha jinsi ya kurudisha bikra ndani ya siku 21 bila kuangalia madhara iwapo watoto wa kike wasiojitambua wakivipata vitabu hivyo.

Waislamu tutapataje nusra kama sisi ndio tunaoongoza kwenye biashara za kusambaza munkari katika jamii. Muislam anashirki kutangaza kamari kwenye duka lake kwa kuuza jezi za timu zinazodhaminiwa na kampuni ya kamari. Tumlaumu nani?

Kuzidisha bei ya bidhaa bila kuwa na nia ya kununua.

Jambo hili hutokea zaidi kwenye minada ili kupandisha bei kwa wanunuzi halisi. Jambo hili halikubaliki na ni aina ya udanganyifu kwa sababu inapapelekea kuwatia watu uzito usiostahili katika minada hiyo.

Kuuza au kununua chini au juu ya bei ya mwenzako

Ukikuta mwenzako anataka kununua bidhaa kwa bei fulani usiingilie kuongeza bei ili kununua kwa bei ya juu yake. Hali kadhalika, kama we ni muuza bidhaa, ukiona mwenzako anauza kitu kwa mteja kwa bei fulani, usiingilie na kumshawishi mteja umuuzie kwa bei ya chini. Mfumo huu umekatazwa katika Uislamu kwa sababu unapelekea chuki.

Jambo hili pia limeingia katika masuala ya posa. Isiwe ushaona mwenzako kaposa na wewe unaenda kuharibu kwa kushawishi kwa pesa zako.

Ghishi (udanganyifu)

Si katika sisi mwenye kufanya udanganyifu. Utapeli sio katika tabia za Kiislamu. Kufanya udanganyifu n pamoja na kuficha kasoro ili uuze bidhaa yako. Kuuza bidhaa mbovu kwa kuchanganya na nzima pia ni udanganyifu alioukataza bwana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Kadhalika, usiuze bidhaa, mfano gari, bila kubainisha aibu au kasoro za gari hiyo. Mfano mwingine wa udanganyifu ni mtu anayetaka kuuza ng’ombe lakini hamkamui wiki nzima ili siku ya kumuuza aoneshe kuwa anatoa maziwa mengi sana, kinyume na uhalisia.

Kuuza kisichojulikana

Kuuza samaki kwenye maji kabla hawajavuliwa, ndama kabla hajazaliwa, mazao kabla hayajapandwa – haya yote waswahili huita kuuziana mbuzi kwenye gunia. Yote hayo ni katika makosa wanayofanya wafanyabiashara. Mfano mwingine wa kuuza kisichojulikana ni kitendo cha kuuza matunda ya mti bila kujulikana kiasi chake.

Ikiwa mazao ya shamba yamezoeleka kuwa kiasi fulani kwa heka kadhaa zinazolimwa na akatokea tajiri anayetaka kutoa hela kununua kabla ya msimu wa mavuno, hili linajuzu. Makadirio huwekwa hadharani kutokana na uzoefu wa misimu iliyopita. Na hili lina maslahi kwa mkulima mwenye uzoefu wa kujua makadirio ya mavuno yake ya kila mwaka, ikiwamo ujazo na bei. Kwa kufanya hivyo, wala haitadhuru mavuno yakiongezeka au kupungua kidogo.

Kubadilishana bidhaa sawa kwa mmoja kupunjwa

Kosa la mwisho kwa leo ambalo hufanywa na wafanyabiashara wa Kiislamu ni kubadilisha bidhaa sawa kwa mmoja kupunjwa. Mfano wa jambo hili ni kioe tunachokiona kwenye vituo vya daladala kwa wauza chenji. Utaambiwa, unauziwa shilingi za Kitanzania 850 kwa kubadilishana na noti ya kitanzania shilingi 1,000.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close