5. Fatawa

FATAAWA

Chanzo cha itikadi katikaUislamu
Swali: Itikadi yetu tunaitoa
wapi?
Jawabu: Itikadi katika Uislamu
inatolewa kwenye Qur’an na
Sunna.
Lengo la kuumbwa majini na watu
Swali: Kwa nini Allah aliwaumba
majini na watu?
Jawabu: Allah amewaumba
majini na watu kwa ajili ya kumuabudu.
Allah anasema: “Nami
sikuwaumba majini na watu ila
waniabudu Mimi” (Qur’an,
51:56).
Maana ya kuabudu
Swali: Nini maana ya
kuabudu?
Jawabu: Maana ya kuabudu
ni kupwekesha.
Maana ya Laailaha illa llah
Swali: Nini maana ya
Lailaha illa llah?
Jawabu: Maana ya ‘Lailaha
illa llah’ ni kuthibitisha kuwa:
“Hakuna Mola anayestahiki
kuabudiwa kwa haki isipokuwa
Allah.” Na sivyo kama wanavyosema
baadhi ya watu eti: Hakuna
Mola isipokuwa Allah. Hili ni
kosa.
Maana ya Shirki
Swali: Shirki ni nini?
Jawabu: Ni kuabudu kitu
kingine pamoja na Mwenyezi
Mungu
Aswali Ijumaa na familia yake nyumbani
Swali: Je inajuzu mtu
kuswali Ijumaa na familia
yake?
Jawabu: Ikiwa mtu ataswali
nyumbani Ijumaa na familia
yake, swala yao haisihi na wanatakiwa
waswali adhuhuri. Ni wajibu
kwa wanaume kwenda
kuswali Ijumaa msikitini. Ama
kwa wanawake, Ijumaa kwao si
wajibu. Wao wanatakiwa wakaswali
adhuhuri nyumbani, ingawa
iwapo watakwenda msikitini
kuswali kwa lengo la kusikiliza
mawaidha, hakuna ubaya.
Swala ya Safari
Swali: Naomba unifahamishe
taratibu za Swala
ya Safari?
Jawabu: Msafiri anaruhusiwa
kupunguza swala, lakini swala
zinayoruhusiwa kupunguzwa ni
zile za rakaa nne; Adhuhuri, Alasiri
na Isha, na badala yake
msafiri ataswali rakaa mbili. Ama
swala ya Magharibi na Alfajiri
huswaliwa kama zilivyo, hazipunguzwi.
Na upunguzaji huanza
mara baada ya kutoka nje ya
mpaka wa mji kama alivyofanya
Mtume (rehema na amani ya Allah
imshukie).
Baadhi ya wanazuoni wameukadiria
umbali wa masafa ya kupunguza
Swala ni Kilomita 80,
na wapo waliosema kinyume na
hivyo. Na iwapo msafiri ataswali
nyuma ya Imamu anayetimiza
naye atatimiza. Na muda
wa kupunguza ni kuanzia
siku moja, mbili, tatu mpaka
nne; baada ya hapo
utaswali rakaa kamili
kama mkazi wa mji,
isipokuwa kama una shaka
ya kuondoka muda wowote,
hapo hata kama zitazidi
siku nne unaweza kuendelea
kupunguza. Na Allah
ndiye Mjuzi.
Kumpa lakabu (nick name) mtu au mtoto hata kama hana mtoto
Swali: Je, inafaa kumwita
mtoto wangu Abu/
baba fulani au kama ni wa
kike, Umu/mama fulani
hata kama hana mtoto au
kabla hajafikia umri wa kuzaa?
Jawabu: Naam, unaweza
kumwita mtu asiye na mtoto au
mtoto mdogo kwa lakabu uipendayo
kwani kuna faida nyingi zilizoelezwa
na wanazuoni za kumpa
mtu asiye na mtoto au mtoto
mdogo lakabu kabla ya kuwa na
mtoto. Faida hizo ni pamoja na,
mosi, kumjenga kisaikolojia, pili,
kumuepusha na majina mabaya
na tatu, kumpa matumaini ya
kuishi na kuja kupata watoto.
Vilevile, upo ushahidi wa
Mtume mwenyewe (rehema na
amani ya Allah imshukie) kumuita
Bi, Aisha, Ummu Abdillah, au
yule mtoto mdogo aliyekuwa
anachezea ndege ambaye Mtume
alimuita Aba Umayr.
Kuwapa pole wafiwa ni ibada au ada?
Swali: Twataka kujua
kuhusu hii desturi ya baadhi
ya watu kukusanyika
msibani. Tunapowahoji
hutuambia hii ni jadi. Je, hili
likoje?
Jawabu: Kwenda kutoa
pole/kuhani msibani ni Sunna na
ni Ibada, lakini kama watu
wataitekeleza ibada hii kinyume
na ilivyokuwa enzi za Mtume, bila
shaka itakuwa ni uzushi (bid’ah).
Lakini kwa kuwa kuhani ni Sunna
ndiyo maana kuna kupata thawabu
kwa mtu anayemhani mfiwa,
lakini pia thawabu haziwezi
kupatikana kwenye uzushi.
Asiyefuata Sunna ni Muislamu pia
Swali: Je, mtu asiyefuata
Sunna si Muislamu?
Jawabu: Hatusemi, mtu asiyefuata
Sunna si Muislamu. Suala
hili linahitaji ufafanuzi na
kuliangalia kwa kina na si kulichukulia
kijuujuu. Yawezekana
mtu akatoka kwenye Uislamu
kama ataenda kinyume na masuala
ya kiitikadi, kama vile kumshirikisha
Mwenyezi Mungu au
kumuomba asiye Mungu nk.
Ama ikiwa amekhalifu Sunna
au kwenda kinyume na baadhi ya
mambo ya kisunna huyo hawezi
kukufurishwa muda wa kuwa
hakani na wala hazikebehi Sunna,
isipokuwa atazingatiwa kuwa
ni mzushi na ni mpotovu kwa kadiri
ya uzushi wake.
Kuswali na nguo yenye matone ya damu
Swali: Je, nguo yangu ikiingiwa
na damu ninaweza
kuswali nayo au la?
Jawabu: Kama damu
itakuwa nyingi ni najisi na
hairuhusiwi kuswali na nguo
hizo, na kama itakuwa chache na
damu twahara, kama damu ya ini
au ya nyama baada ya kuchinja,
hiyo haidhuru.
Swala haiharibiki kwa najisi uliyoisahau au usiyoijua
Swali: Ni ipi hukumu ya
swala ya mtu aliyeswali na
nguo aliyosahau kama ina
najisi au alikumbuka baada
ya kumaliza kuswali?
Jawabu: Swala yake ni sahihi.
Allah anasema: “(Ombeni),
‘Mola wetu Mlezi! Usituchukulie
tukisahau au tukikosea. Mola
wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo
kama ulio wabebesha wale walio
kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi!
Usitutwike tusiyoyaweza, na
utusamehe, na utughufirie, na
uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi
wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde
Kaumu ya Makafiri”
(Qur’an, 2: 286).
Na hata Mtume aliwahi kujiwa
na Malaika Jibril wakati akiwa
ndani ya Swala anawaswalisha
watu na akiwa amevaa viatu
vilivyokuwa na uchafu. Alijiwa na
Malaika na kumueleza kama viatu
vyake vilikuwa na uchafu,
Mtume alivivua ndani
ya Swala na akaendelea na
Swala. Lau Swala ingekuwa
inabatilika kwa
kutojua kama alikuwa na
najisi Mtume angeswali
tena.
Kumswalia maiti baada ya kuzikwa
Swali: Je, ninaweza
kumswalia maiti aliyekwishazikwa
kaburini?
Jawabu: Iwapo kama maiti
alishazikwa unaweza ukamswalia,
na ushahidi wa hilo ni
Mtume mwenyewe kuwahi
kumswalia mwanamke aliyekuwa
anafagia msikiti, ambaye
alikufa na kuzikwa pasipo yeye
kupata habari.
Kujiita kwa jina la Alhafiydh,
Al-hadiy, nk…
Swali: Je, inajuzu mtu kujiita
kwa jina la Mwenyezi
Mungu kama vile al-Kariym
(Karim), al-Hadiy, (Hadi) alHafiydh
(Hafidh), al-Rauf
(Raufu) mathalan na bila ya
kutanguliwa na Abdu?
Jawabu: Sahihi ni kujiita
Abdul Hadiy au Abdul Kariym,
Abdul Haafidh, na hii ndiyo sawa.
Ama kujiita al-Hadiy au al-Kariym
kavukavu, hilo ni jina la Mungu
na siyo sahihi.
Kutoa siri za ndani
Swali: Ni ipi hukumu ya
mume au mke anayetoa
siri za ndani?
Jawabu: Mtume amesema:
“Mtu muovu zaidi na aliye na
makazi mabaya mbele ya
Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama
ni mume na mke wanaotoa
siri zao za na ndani au faragha.”
Imam An- Nawawiy anaeleza:
“Ni haramu kwa mwanaume na
mke kueneza siri zao za ndani ya
nyumba yao au starehe zinazojiri
baina yao. Na tabia hizi zipo kwa
wanaume na kwa wanawake pia.
Haifai na ni haramu.”
Kusoma Fatiha wakati
wa kufunga ndoa
Swali: Ni ipi hukumu ya
kusoma ‘Fatiha’ wakati wa
kufunga ndoa?
Jawabu: Kwa kweli hiyo siyo
Sunna bali Sunna ni kuanza kwa
kutoa hotuba ya haja.
Haki za Muislamu kwa
nduguye Muislamu
Swali: Ni zipi haki za mwislamu
kwa nduguye Muislamu ?
Jawabu: Haki za Muislamu
kwa nduguye Muislamu ni nyingi,
ikiwemo kumsalimia unapokutana
naye, anapokuita kumuitikia,
anapokutaka nasaha
kumnasihi, anapokwenda chafya
kumuombea Mungu, kumtembelea
anapoumwa, na anapokufa
kusindikiza jeneza lake.
Kusijishughulisha na
jambo jingine unapokaa
na mtu
Swali: Dunia yetu ya leo
mtu akipata upenyo wa kutuliza
makalio yake chini
tu, kitu cha kwanza atafungua
simu yake na kuanza
kuchati. Je, kuna mafunzo
yoyote kutoka kwa Mtume
yanayoelekeza namna ya
kuheshimu kikao na
mwenzako?
Jawabu: Kuna wakati
Mtume (rehema na amani ya Allah
iwe juu yake) alitengeneza
pete na kuivaa. Halafu akawaambia
watu: “Hii imenishughulisha,
mara naiangalia na mara nawaangalia
ninyi, akaivua na
kuitupa. Na hii ndiyo ilikuwa desturi
na adabu ya Mtume kwenye
vikao. Hakupenda kujishughulisha
na kitu anapokuwa mbele ya
wengine.”
Ndugu hawaswali
nifanyeje
Swali: Alhamdulillahi!
Mimi ni kijana ninayefuata
dini, lakini nina tatizo
kubwa la kuishi na ndugu
wasioswali, na nimefanya
jitihada kubwa na bila ya
mafanikio. Je, unaninasihi
niishi nao vipi?
Jawabu: Kilicho wajibu
kwako ni kuendelea kuwalingania
na kuwapa nasaha huenda
Allah akawafungua, na iwapo
wataonesha kuwa wazito wewe
usiwakatie tamaa, na ujue hata
Mtume alikuwa na watu wa aina
hiyo katika familia yake na wala
hakukata tamaa katika kuwalingania.
Mtume alimlingania ami
yake hata wakati anakata roho,
lakini ami yake alihiyari kubaki
katika ushirikina. Licha ya hivyo,
Mtume alimuahidi ami yake kumuombea
kwa Allah amsamehe,
iwapo Allah hatomkataza.
Mwenyezi Mungu akateremsha
aya: “Haimpasi Mtume na
wale walioamini kuwatakia msamaha
washirikina ijapokuwa ni
jamaa (zao); baada ya kuwabainikia
kuwa wao ni watu wa motoni”
(Qur’an, 9:113).
Hivyo ndugu yangu, wewe
unachotakiwa ni kuwalingania
wanaokuzunguka wala usiwakatie
tamaa, Waombee hidaya na
utumie mbinu mbalimbali za kuwafikishia
ujumbe ikiwemo kuwaombea
dua. Na wala usikimbilie
kuwafukuza
nyumbani
au kujitenga
nao,
huenda kule
kubaki kwako
kukawa na usalama
na
ahueni kimaadili
kuliko
kuwa mbali
nao.

Tags
Show More

Related Articles

Check Also

Close
Back to top button
Close