1. Fahamu Usiyoyajua

Tuchukue tahadhari kuepuka majanga misimu ya mvua

Kwa takriban wiki moja sasa, nchi yetu imebarikiwa kuwa na mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini, ukiwamo mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Morogoro na visiwa vya Zanzibar.

Awali, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitahadharisha juu ya ujio wa mvua hizo huku ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari. Jambo la kusikitisha ni kuwa mvua hizo zinazoendelea kunyesha zimeshaleta madhara ambayo yalishatabiriwa na TMA.

Pamoja na kwamba mvua ni moja kati ya neema kubwa kutoka kwa Mwenyenzi Mungu, mvua pia zinaweza kusababisha vifo na kuharibu miundombinu muhimu ya barabara, nyumba na madaraja.

Hivyo, tunawashauri wananchi kusoma taarifa zilizotolewa na TMA na kuzifanyia kazi, kwa kuwa zitawasaidia katika kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza. Tunasema hayo kwa sababu, tayari watu wanne akiwamo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, wameshapoteza maisha huko jijini Mbeya baada ya daraja walilokuwa wakipita kukatika na kutumbukia mtoni.

Madhara haya pengine yangeweza kuepukika kama watu wangechukua tahadhari kama walivyotangaziwa mapema na mamlaka husika. Ukiachilia mbali jukumu la Serikali kufanya uokoaji katika majanga mbalimbali, wajibu wa kwanza ni watu wenyewe kuchukua tahadhari kwa kujiepusha na madhara hususan vifo.

Maeneo ambayo huathiriwa na mvua kila mara yanafahamika, lakini watu wanaendelea kukaa katika maeneo hayo, huku wakiendelea kupoteza mali na hata uhai.

Serikali imekuwa ikihimiza mara kwa mara watu wahame katika maeneo ya mabondeni kuepusha majanga. Lakini masikio ya walio wengi yamewekwa nta. Wengine wanaopaswa kuchukua tahadhari ni wale wanaothamini mali kuliko uhai wakati wa mafuriko.

Si lengo letu kuwakebehi waliotangulia mbele ya haki, lakini inashangaza kuona mtu anapoteza maisha kwa kujaribu kuokoa luninga au samani za nyumba yake badala ya kuokoa nafsi yake.

Sisi wanadamu tunapaswa tutambue kuwa uhai wetu una thamani kuliko mali tunazomiliki. Hivyo, ni vema uokoaji wa mali ufanywe mapema kabla hatari haijaanza kuonekana. Mwenyezi Mungu anatuambiaa: “Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizi.” [Qur’ an, 2: 195].

Tunamalizia tahariri hii kwa kuuliza swali, je, wananchi wanatafakari taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa? Na je, mamlaka za miji zimehakikisha njia za kupitisha maji zinajengwa kwa viwango stahili ili ziweze kusafirisha maji hayo na kuacha makazi salama? Kama hatujafanya hayo, hatujachelewa. Tuchukue hatua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close