1. Fahamu Usiyoyajua

Tembo: Mnyama mkubwa kuliko wote ardhin

Ndugu yangu msomaji wa safu hii, karibu tena tukujuze ambayo huenda huyajui katika maisha na tabia za viumbe mbalimbali kwa madhumuni ya kuujua na kuuona ukubwa wa Mola wetu Muumba, Allah Aliyetukuka. Juma hili, nataka nikujuze kuhusu mnyama tembo, ambaye hufahamika pia kwa jina la ndovu au kwa jina la kisayansi Loxodanta Africana.


Tembo wa Afrika pekee ndiye mwenye uwezo wa kutofautisha kabila, jinsia na umri wa mwanadamu

Tembo ni katika jamii ya wanyama ambao huishi kijamaa, kila mara wapo huwa kwenye makundi. Katika kundi huwa kuna dume na jike, watoto. Pia kundi huwa na kiongozi mwenye uwezo wa kuwajua tembo wote waliopo katika kundi lake. Katika familia moja, tembo wanaweza kuishi kuanzia wawili hadi 45. Kila tembo dume kwa kawaida huwa na majike wawili mpaka wanne.

Tembo pia ni mnyama mkubwa kuliko wote ardhini, ambapo inatajwa kuwa, tembo dume huweza kufikia hadi kilo 2000 hadi 6000 (yaani tani mbili hadi sita). Jike nalo huweza kufikia kilo 2000 hadi 4000 (tani mbili hadi nne). Naye mtoto wa tembo huzaliwa akiwa na kilo zisizopungua 120.

Tembo wapo aina mbili, wale wa Afrika na wale wa Asia, ambapo wale wa Afrika ni wakubwa na masikio yao yana muonekano wa ramani ya bara la Afrika. Wale wa bara la Asia wana masikio madogo na pia wanaweza kufundishwa kulima na michezo mbalimbali.

Kuna mengi yanayomhusu mnyama huyu ambayo huwezi kuyakuta kwa mnyama mwingine wa porini. Tembo ni mnyama aliyejaaliwa uwezo wa kumsikia tembo mwenzake akilia kutoka umbali wa hadi kilometa tano.

Hata hivyo, tembo hana uwezo mkubwa wa kutambua vitu kwa kuona bali hutegemea zaidi pua na masikio katika maisha yake. Kutokana na hali hiyo, ukiwa porini unashauriwa kumpiga picha tembo bila ya kutumia ‘flashi’ [mwanga] kwani tembo akiona mwanga hawezi kutofautisha kama ni kitu cha kawaida au ni hatari. Katika mazingira hayo, tembo huanza huelekea kwa hasira upande ulipotoka mwanga.

Umri wa tembo wa kuishi kwa sasa ni miaka 60-75 lakini miaka ya nyuma walikuwa na uwezo wa kuishi hadi miaka 80-120. Sababu za kupungua muda wa kuishi inatajwa kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi.

Mambo usiyoyajua kuhusu tembo
Tembo pamoja na ukubwa wake, akitembea hana kishindo kabisa. Miguu yake kwa chini ni kama ina sponji hivi.

Wakati binadamu hubeba ujauzito kwa kipindi cha miezi tisa, jike la tembo hubeba ujauzito kwa jumla ya miaka miwili yaani miezi 24.

Ukimwondoa mwanadamu ambaye ana kidevu, tembo ndiye mnyama mwingine ambaye pia ana kidevu.

Tembo wa Afrika pekee ndiye mwenye uwezo wa kutofautisha kabila, jinsia na umri wa mwanadamu. Ikiwa jana alijeruhiwa na mtu anayezungumza Kiingereza, akisikia Kiingereza anakumbuka upesi.

Kila mnyama kuna kitu anakiogopa, ajabu ya tembo ni kuwa anamuogopa nyuki. Tembo mkubwa na mzito kupita wote anapatikana Afrika.

Mwanadamu hulala walau masaa nane kwa siku, lakini kwa tembo ni tofauti. Tembo hulala masaa mawili hadi matatu tu kwa siku!!

Tembo mkubwa huhitaji walau kilo mia tatu za chakula na maji lita 160 kwa siku, hivyo kama unataka kumfuga jiandae kweli kweli.

Tembo anategemea sana uwezo wake wa kunusa kutambua mazingira aliyopo na vitu vinavyomzunguka. Sambamba na harufu, tembo pia ana uwezo mkubwa wa kusikia.

Tembo hunyonyesha mtoto wake kwa takribani miaka miwili hadi mitatu. Akifikisha miaka 15,tembo huhesabika kuwa ameshakua na hutakiwa kuondoka katika familia hiyo na kwenda kujitegemea.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close