1. Fahamu Usiyoyajua

Swala, mnyama aliyetawaliwa na wasiwasi

Ndugu yangu msomaji, dunia ya Muumba wetu Allah, mbora wa uumbaji, ina mapambo mengi. Ukiachilia mbali milima, bahari, mito, maziwa, majangwa; pia kuna wanyama wa aina nyingi. Wanyama hawa ni hisani kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi kwa ajili yetu sisi wanadamu.

Ninapozungumzia tabia za wanyama na viumbe wengine; nauona ukubwa na uwezo wa Muumbaji katika fikra zangu. Katika makala hii ya ‘Fahamu Usiyoyajua’ tutamzungumzia swala, mnyama mwenye umbo la wastani, si mkubwa si mdogo, ambaye ni maarufu mno kwetu.

Umaarufu wa swala unatokana pia na ukweli kwamba, ukitembelea mbuga zetu mara nyingi ni rahisi sana kuwaona tofauti na wanyama wengine. Kwa mbuga ya Mikumi ambayo niliwahi kufika, unaweza usibahatike kuingia ndani lakini ukawaona hata barabarani.

Swala hupatikana katika maeneo yenye nyasi fupifupi na vichaka vidogo (savanna, hususan kwenye maeneo mengi ya hifadhi barani Afrika). Kuna aina ya swala hukimbia kilometa 80 kwa saa na wana uwezo wa kuruka mita saba hadi nane juu, akiwa kwenye kasi. Rangi yao ni ya mchanga na nyeupe kidogo kwenye koromeo na sehemu ya chini ya mkia. Simba, chatu na chui ni maadui wakubwa wa swala. Pia ni muhimu kutaja kuwa, mnyama huyu anapatikana sana Afrika Mashariki, lakini hawa ni wale tunaowajua kama swala wa kawaida.

Mtaalamu mmoja kutoka nchini Ujerumani, Hinrich Lichensten, ambaye ni miongoni mwa watu wa kwanza kumuelezea swala, alisema wanyama hawa wapo aina mbili, swala wa kawaida na swala mkubwa mwenye rangi nyeusi usoni ambaye anapatikana kule Angola, na Namibia.

Uzazi

Katika uzazi, swala wanabeba mimba na kuzaa. Mimba yao huchukua miezi sita hadi saba; na mara nyingi wanazaa mtoto mmoja. Pia, swala hunyonyesha kwa muda wa miezi minne mpaka sita.

Chakula

Swala wanakula nyasi na matunda. Wakati wa masika, swala huwa wanapenda kula majani yanayochipukia ila wakati wa kiangazi wanapenda kula majani ya matawi ya miti midogo midogo katika miti inayochipukia.

Mambo sita usiyoyafahamu kuhusu swala

  • Wanashughulika sana na maisha, yaani kutafuta malisho, mchana kuliko usiku.
  • Madume wamepambwa na pembe zilizoenda juu ila majike hawana pembe kabisa.
  • Ili kukubalika na majike, madume hupambana kwanza na atakayeshinda anamchukua jike.
  • Swala ni mnyama ambaye ana tabia ya wasiwasi (hajiamini). Kila muda yupo juu juu tayari anataka kutoroka. Wazungu wanaiita hii ‘anti predator strategy,’ yaani mbinu ya kumkimbia adui.
  • Jike la swala linapokuwa tayari huwa linatoa harufu katika sehemu ya uke na dume akihisi hiyo harufu anajua anatakiwa afanye nini.
  • Kitoto cha swala huwa kinasimama na kutembea dakika chache tu baada ya kuzaliwa.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close