1. Fahamu Usiyoyajua

Sungura mnyama anayekula kinyesi chake | Fahamu Usiyoyajua

Naam, ndugu yangu msomaji, sungura ni kiumbe anayepatikana karibu maeneo yote duniani isipokuwa sehemu za ncha ya kaskazini. Inaelezwa kuwa nusu ya sungura wote duniani wapo katika bara la Amerika ya Kaskazini.

Wanyama hawa wanajulikana kwa masikio yao marefu yaliyoelekea juu, miguu minne; miwili mbele na miwili nyuma. Tofauti na wanyama wengine, miguu ya nyuma ya sungura ina nguvu zaidi kuliko ile ya mbele. Pia sungura ana macho kwa pembeni ambayo huona vizuri.

Sungura wapo wenye rangi nyeupe, kijivu, na kahawia. Sungura hupendelea sana kuishi porini ingawa pia wapo wanaofugwa nyumbani. Sungura mkubwa anaweza kufikia uzito wa hadi kilo mbili. Wastani wa maisha ya sungura hasa waishio porini ni kati ya mwaka mmoja hadi miwili. Hata hivyo, katika kisiwa cha Tasman kilichopo kusini mwa Australia, aliwahi kupatikana sungura aliyeishi takriban miaka 18.

Barani Afrika, sungura huonekana kama kiumbe mjanja kutokana na kutajwa sana katika hadithi za ‘Pauka, pakawa’ ambazo watoto husimuliwa na wazazi au walimu wao kama sehemu ya kuwaburudisha.

Tofauti na hivyo, baadhi ya tamaduni barani Ulaya humchukulia sungura kama kiumbe mwenye bahati sana. Kadhalika, nchini Japan na Korea jamii nyingi zinaamini kuwa sungura ni kiumbe anayeishi mwezini.

Ukweli ni kwamba, sungura ni mnyama kama walivyo wanyama wengine na hana sifa wala uwezo huo kama wanavyodai watu.

Hata ujanja anaotajwa kuwa nao sungura katika vitabu vya watoto na katika hadithi tunazosimuliwa na wazee wetu hazina ukweli wowote bali ni uongo uliotungwa kwa malengo ya kupumbaza akili za watu.

Uzazi Na Chakula
Baada ya kufikisha miezi sita tangu kuzaliwa, sungura anakuwa tayari amekomaa na anaweza kupata mimba nyingine.

Sungura huchukua siku 31 kupata mimba hadi kuzaa na hutumia wiki 5 hadi 7 kunyonyesha. Anapomaliza muda wa kunyonyesha huwaachisha watoto wake ziwa ili kujiweka huru kwa ajili ya kushika mimba nyingine.

Katika chakula, sungura hula matunda na mbogamboga (vegetables), pia hupendelea kunywa maji mengi hasa yale yanayotokana na mito (Herbivorous).

Mambo 10 usiyoyajua kuhusu sungura
  • Sungura anayefugwa anaweza kulala mpaka saa nane.
  • Umeng’enyaji chakula wa sungura si mzuri sana wakati anaposaga chakula na ndio maana hula kinyesi chake kwa sababu hakisagwi vizuri.
  • Sungura anatoa vinyesi vya aina mbili; kinyesi kigumu na laini, lakini mara nyingi hukifanya kinyesi laini kama chakula chake.
  • Ni viumbe wanaopenda kubebwa na kupapaswa.
  • Sungura anaweza kutambua jina alilopewa na pindi anapoitwa kwa jina lake hufanya haraka ya kusogea eneo aliloitwa.
  • Sungura hawapendi kula vyakula vyenye mizizi na karoti
  • Sungura hawali mbegu za tufaha au apple, majani ya nyanya na vitunguu kwa kuwa vyakula hivyo vyote ni sumu kwao.
  • Sungura wana tabia ya kukimbia upande upande wakati wanapofukuzwa, yaani kulia na kushoto (zigzag).
  • Aghalabu sungura huwindwa na wanyama wakali wa mwituni akiwemo mbweha na paka pori aina ya Lynxes.
  • Jicho la sungura lina uwezo mkubwa wa kuona, anaweza kulizungusha hadi nyuzi 360.
Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close