1. Fahamu Usiyoyajua

SNOW LEOPARD: Chui wa kwenye barafu aliye

Chui wa kwenye barafu ni mnyama jamii ya paka wakubwa ambaye hupatikana zaidi katika milima mirefu ya Asia ya Kati na Kusini hasa Afghanstan, milima ya Himalaya, Tibetan Plateau, Saibriya ya Kusini, Mongolia na Magharibi ya China na India.

Miili yao ina rangi nyeupe, kijivu, na madoa meusi. Maeneo yao ya tumboni ni meupe. Rangi yao mara nyingi inakuwa sawa na mawe na udongo wa milima. Pia, wanyama hawa wana manyoya mazito, mengi na marefu kiasi cha inchi tano. Mkia wake ni mfupi kiasi na mnene.

Kwa hekima zake, Allah, Mbora wa Uumbaji na anayejua kukadiria amemjaalia chui wa kwenye barafu kuwa na manyoya mengi na mazito ili kumkinga na baridi kali ya maeneo aliyopo. Mikono na miguu ya chui wa kwenye barafu inatajwa kuwa na nguvu.

Wataalamu wanasema mnyama huyu ana uzito wa kati ya Kilogramu 22 hadi 55, ingawa dume anaweza fika uzito hadi Kilogramu 75. Eneo la pua la chui huyu lina uwazi mkubwa katika tundu lake la pua. Tundu hili humsaidia kupitisha hewa vizuri zaidi.

Jingine kuhusu mnyama huyu ni kuwa anapenda kuwa peke yake isipokuwa muda wa kupandana tu. Ni kipindi hicho ndiyo wanyama hawa hulazimika kukutana. Umri wao wa kuishi ni miaka 15 hadi 18 ila wakifugwa hufika hadi miaka 25.

Uzazi na chakula

Katika uzazi, jike linakomaa miaka miwili au mitatu, kisha hapo huweza kubeba mimba na kuzaa. Umri wa kubeba mimba ni siku 90 hadi 100 sawa na miezi mitatu na siku chache; na aghlabu huzaa watoto wawili hadi watatu. Kipindi chao cha kuzaa ni mwezi wa nne na wa sita.

Kwa upande wa chakula, chui wa kwenye barafu hula nyama, yaani ni ‘carnivorous’. Chakula chao pendwa ni kondoo wa milimani (Himalaya blue sheep).

Mambo 10 usiyoyajua kuhusu snow leopard

  • Snow Leopard wameyazoea zaidi mazingira yao ya kwenye baridi na milimani kuliko maeneo mengine. Maumbile yao yanawawezesha kufurahia maisha huko.
  • Chakula kikubwa cha chui wa kwenye barafu ni kondoo wa bluu. Chui mmoja wa kwenye barafu anaweza kutumia kondoo mmoja kama chakula chake cha juma zima.
  • Chui wa kwenye barafu hupendelea sana kuwepo katika maeneo yenye miinuko ya mita 3000 hadi 4000. Katika milima, hupendelea maeneo miamba iliyovunjika vunjika.
  • Chui wa kwenye barafu, kama walivyo paka wakubwa wengine, wana tabia ya kuweka mipaka ya eneo wanalotawala kwa kutumia mikojo yao.
  • Chui hawa aghalabu huitwa ‘zimwi la milimani’ kwa sababu hawaonekani kirahisi na huishi maisha ya kujitenga na upweke.
  • Tofauti na paka wengine wakubwa, chui wa kwenye barafu hawezi kuunguruma.
  • Chui wa barafuni wanaweza kusafiri hadi maili 25 kwa usiku mmoja.
  • Chui wa kwenye barafu ni wazuri zaidi katika kujificha kuliko jamii nyingine ya paka hasa pale wanapotaka kushambulia wanyama. Uhodari huu wa kujificha unakuja kwa sababu rangi zao za mwili kufanana na mazingira wanayoishi (camouflage).
  • Chui wa kwenye barafu ni hodari zaidi katika kuruka umbali mrefu kuliko paka wengine. Chui hawa wanaweza kuruka hadi mita 9, ikiwa ni mara sita urefu wa mwili wao!
  • Chui wa kwenye barafu wapo hatarini kutoweka kutokana na mazingira yao kuingiliwa na binadamu. Kitisho kikubwa dhidi ya chui hawa ni ujangili na mabadiliko ya hali ya hewa. Shirika la kutunza na kulinda wanyama (WWF) linafanya kazi pamoja na jamii, serikali na mashirika mengine kulinda baadhi wanyama hawa wasitoweka
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close