1. Fahamu Usiyoyajua

SIMBA: Mnyama anayewinda kwa kutumia akili sana

Ni dhahiri katika uumbaji wa mbingu na ardhi, kupishana kwa usiku na mchana, kuwepo kwa ndege na wanyama zimo ishara kwa wenye akili kuwa yupo aliyevileta. Juma hili nitakujuza mambo mengi kuhusu simba, mnyama mkubwa, jamii ya paka, mwenye nguvu na anayekula nyama.

Simba ndiye mnyama mkubwa anayewinda katika jamii ya paka wa kubwa. Pia, huyu ni mnyama anayependa kuishi katika makundi makundi, yaani kijamaa kama ilivyokwa binadamu. Familia ya simba inaweza kuwa na wanafamilia takribani 15 hadi 20.

Simba ni miongoni mwa wanyama ambao hupendelea kukaa katika miamba na nyasi kavu kavu ambazo kwa mbali hufanana kwa mbali na rangi yake (camouflage). Mazingira haya humsaidia kujificha dhidi ya adui anaowavizia ili kuwala. Simba anafanikiwa kwa njia hiyo kwani akiwa katika majani makavu ambayo yanafanana na rangi yake, si rahisi kwa swala, pundamilia au mnyama yoyote kujua kwamba kuna simba.

Kwa kuwa simba huishi kifamilia,dume ndiyo huanzisha makazi mapya, ambapo likiunguruma, sauti hiyo husafiri umbali mrefu sana. Sehemu inapoishia sauti hiyo ndiyo mpaka wa makazi yao. Iwapo sauti hiyo itakumbana na makazi ya simba wengine, basi dume jingine litaitikia, na hapo kinachofuata ni simba hao kuhama.

Iwapo simba hao wa kundi moja hawatakubaliana kutoka, basi madume ya pande hizo mbili yatakutana na kuoneshana ubabe na liatakaloshindwa litaondoka na familia yake. Simba wakiwa mawindoni, wana uwezo wa kuangusha hata wanyama wakubwa, ingawa si mara nyingi kuwashambulia wanyama wakubwa (kama vile twiga au nyati) kwa kuhofia kujeruhiwa.

Simba wana nguvu nyingi na mara zote huwinda kwa makundi, wakikazania windo moja walilochagua. Hata hivyo,simba hawana stamina sana. Kwa mfano, moyo wa simba jike ni asilimia 0.57 ya uzito wa mwili wake huku wa dume ni asilimia 0.45. Linganisha na moyo wa fisi ambao uzito wa moyo wake ni karibu asilimia moja ya uzito wake.

Hivyo basi, ingawa simba anaweza kufikia mwendokasi wa km 81 kwa saa, wanaweza kufanya hivyo kwa mwendo mfupi tu na inawapasa kuwa karibu na mawindo kabla ya kuanza shambulio. Simba hutumia mwanya wa kupunguza uoni wa adui kwa kufanya uwindaji sana nyakati za usiku.

Simba humnyatia adui mpaka karibu kwa walau mita 30 au pungufu. Baada ya kukaribia, huchagua mnyama aliye karibu. Shambulio huwa fupi na la nguvu. Simba hujaribu kumkamata kwa kumkurupusha kwa kasi na kisha kumrukia. Mnyama huyo anayewindwa huuawa kwa kunyongwa. Mara kadhaa,mnyama anayewindwa huweza kuuawa kwa kuzibwa mdomo na pua zake kwa taya za simba. Wanyama wadogo huuawa tu kwa kupigwa ngwala kwa mguu wa simba.

Simba anafanikiwa sana katika mbinu zake za uwindaji kwa sababu hana tamaa.Mnyama ambaye simba anapanga kumkamata, huhangaika naye huyo huyo; hata kama kuna nafasi ya kumkamata mwingine. Wataalamu wa elimu ya viumbe husema, simba hulenga mnyama mmoja kwasababu huhofia kuharibu mahesabu ya washirika alionao katika mawindo.

Miongoni mwa wanyama wa jamii ya paka, simba ndiye mrefu mabegani ila kwa uzito yeye ni wa pili baada ya chui. Kutokana na kujaaliwa miguu yenye nguvu na taya imara,ana uwezo wa hali ya juu ya kumuangusha hata mnyama mkubwa.

Uzazi

Simba jike hubeba ujauzito kwa siku 110 sawa na miezi mitatu na wiki tatu, kisha hujifungua mtoto mmoja mpaka wanne kwenye sehemu maalumu, mara nyingi mbali na lilipo kundi lake. Watotowa Simba huzaliwa wakiwa hawaoni.Huanza kuona baada ya wiki moja!

Simba jike huweza kujamiiana na zaidi ya dume mmoja. Muda wa kujamiiana unaweza kuchukua hadi siku kadhaa.

Mambo usiyoyafahamu kuhusu simba

  • Simba ana uwezo mkubwa wa kuona mbali na kusikia kutoka mbali. Uwezo wake huo humsaidia kuwinda wakati wowote ule anaojisikia, usiku au mchana.
  • Simba hana papara anapowinda na hutumia mahesabu makali. Kwanza hutafiti udhaifu wa anayemuwinda na baada ya hapo huanza shughuli. Kama mnyama anayemuhitaji ana uwezo mkubwa wa kunusa basi atacheza na upepo, kama anayemuwinda ana uwezo wa kuona mbali basi atajificha kwa ustadi sana.
  • Simba anapowinda, unyayo wake huwa haugusi kabisa chini
  • Simba anapendelea kupumzika na hutumia muda mwingi kupumzika, hata kama hajachoka. Hupumzika kati ya saa 15 hadi 20 katika saa 24 za siku.
  • Ni kiumbe anayewindwa au mtu mwingine kumuona simba awapo katika mawindo
Show More

Related Articles

Back to top button
Close