1. Fahamu Usiyoyajua

SHAWISHI: Samaki wenye umbo la mwamvuli(Jelly Fish)

Sifa njema zote anastahiki Mola Muumba wa Mbingu na Nchi na vilivyomo.

Ni Hakika yenye hakika kuwa Allah ndie peke anayestahiki kuabudiwa, kwani Yeye ndiye Muumba wa kila kitu. Katika dunia hii, Allah ameumba mbingu na ardhi, Jua na Mwezi, bara na bahari, na wanyama waishio humo ambao ni Yeye Allah pia ndiye anayewaruzuku.

Katika viumbe vyote alivyoviumba Mwenyezi Mungu, kuna dalili na ishara ya kuwa Allah Aliyetukuka peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa.

Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuamini kwamba yuko na kuna Aya nyingi zinazozungumzia suala hili. Pia, Allah ameumba viumbe, ambavyo ni ushahidi kwamba Yeye yupo kwani uwepo wa viumbe ni ushahidi wa uwepo wa aliyeumba.

Leo tunajifunza kuhusu kiumbe wa ajabu wa baharini aitwaye Jelly Fish.

Jelly Fish au shawishi kwa anavyojulikana kwa Kiswahili ni kiumbe wa baharini mwenye umbo la mwamvuli na ambaye ni laini, mwenye ngozi inayoteleza.

Ukimuona Jelly Fish, ni ngumu kujua kama ni kiumbe kwani alivyo ni kama vile ua zuuuri. Kiumbe huyu ni wa ajabu kidogo. Kwanza kabisa, hana Kichwa, ubongo, moyo, masikio, miguu wala mifupa. Hata hivyo, jelly fish amejaaliwa kuwa na seli nyingi za fahamu.

Baadhi ya hawa Jelly Fish wanaelea na kuogelea baharini na wengine wanajibanza kwenye mawe huko chini ya bahari.

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanatueleza kuwa, kuna takriban aina zaidi ya elfu moja ya viumbe hawa wanaozunguka katika bahari yetu ya dunia. Wapo jelly fish wenye sumu inayoweza kumdhuru mwanadamu na wapo wengine ambao sumu yao haimdhuru mwanadamu.

Kwa ujumla, ingawa jelly fish wengi hawana madhara, zipo aina kama 70 wenye madhara kwa binadamu. Hawa wanaweza kusababisha maumivu makali, muwasho, mbabuko wa ngozi na hata kifo.

Hata hivyo, uwezekano wa kukutana na jelly fish baharini ni mdogo sana kwa sababu wenyewe ni adimu kuonekana baharini.

Mikono ya jelly fish ndiyo inawasaidia kukamata malisho yao na kujilinda dhidi ya maadui. Wapo wengine ambao wana mikono na katika kila mkono kuna visindano vya kudunga vyenye sumu ambayo inaathiri mishipa ya fahamu (neuro toxin).

Uzazi

Katika uzazi, baadhi ya Jelly Fish huyatoa mayai mdomoni na kuendelea kuyarutubisha nje ya miili yao, na wengine huendelea kuyahifadhi mdomoni hadi yatakapokuwa tayari kiumbe anayeweza kujitegemea.

Kwa wale wanaorutubisha nje ya miili yao baada ya jike kupata mbegu kutoka kwa dume, yai linabadilika na kuwa kiwavi, kisha kiwavi kinakuwa Polybs (duara) wengine wanaruka hatua na kuwa kiumbe kamili.

Chakula

Jelly Fish wanakula viumbe wadogo wa baharini, mayai ya samaki na minyoo. Baadhi hulana wenyewe kwa wenyewe. Lakini pia wapo aina nyingine ambao mbali ya kula vyakula hivyo nilivyovitaja wanakula pia mimea fulani inayoota chini ya bahari.

Mambo 10 usiyoyajua kuhusu jelly fish

  • Allah hajawajaalia kuishi muda mrefu. Wanapozaa tu wanakufa.
  • Jelly fish wapo dume na jike na wapo wengine wana jinsia mbili.
  • Jelly fish anapenda kuwinda kwenye maji ya kina kifupi wakati wa mchana.
  • Iwapo jelly fish mwenye madhara akikudunga, usipowahi kupata matibabu unaweza kupata mshituko wa moyo au kufa.
  • Jelly fish mmoja aina ya ‘box’ ndiye hatari zaidi na ni mmoja kati ya wale wanaoweza kusababisha kifo akimdunga mwanadamu.
  • Kuna utafiti ulifanywa nchini Australia ambapo vifo 63 vilirikodiwa kutokana na shambulizi la jelly fish kwa muda wa miaka 80.
  • Wapo jelly fish wanaopatikana katika maji matamu na wapo wanaopatikana kwenye maji chumvi.
  • Utafiti umeonesha kuwa jelly fish ni kama kioo yaani ukiwaona unaweza kuona kila kitu cha ndani au upande wa pili.
  • Adui mkubwa wa jelly fish ni papa, jodari, kasa, penguin na wenyewe kwa wenyewe.
  • Rekodi zinaonesha kuwa jelly fish wanaongoza kwa kusababisha vifo vya watu majini kuliko mauaji yanayofanywa na papa kila mwaka.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close