1. Fahamu Usiyoyajua

Papa Mweupe: Hatari, ana meno 300!

Shukurani zote ni kwa Allah Aliyetukuka aliyeumba kila kitu, na rehema na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad (rehema na amani ya Allah zimshukie) pamoja na Jamaa zake na Maswahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya Malipo.

Kwa hakika, hakuna shaka juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na dalili ya uwepo wake ni uumbaji wake kama inavyothibitika athari kupitia viumbe tunaowaona na tusiowaona. Kila kiumbe ni dalili ya uwepo Muumbaji ambaye ni Mwenyezi Mungu, Allah Mtukufu.

Ndugu yangu msomaji, kutafakari uwepo na uumbaji wa Allah, nguvu, hekima na uamuzi wake; ni njia mojawapo ya kuleta unyenyekevu (khushui) kwenye moyo wako katika ibada tunazozifanya kuelekea kwake, Mmoja wa Pekee Kabisa, Aliyetukuka. Kupitia viumbe wa Mwenyezi Mungu tunavyovisoma, kuna mazingatio makubwa kama tutamakinika.

Juma hili acha tukaone ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwa kumtazama papa mweupe (Great white shark). Papa mweupe (Great white shark) ni moja ya aina ya papa. Papa wapo aina nyingi, takriban aina 500, kwa mujibu wa wataalamu.

Inadhaniwa papa mweupe ameitwa hivyo kwa sababu ya tumbo lake jeupe. Yeye ni katika viumbe waliojaaliwa akili nyingi na pia anaogopwa baharini, kutokana na umbile lake kubwa. Papa mweupe ana wastani wa urefu ni mita 4.5 (futi 15), ingawa pia yupo aliyewahi kukutwa mwenye urefu wa mita 6 (futi 20) na uzito kilo 2250.

Vipimo hivyo, ni dhahiri vinaonesha, ni papa mkubwa. Wataalamu wanamtaja kuwa ni papa mkubwa kuliko wote wanaofahamika.

Allah Mbora wa Uuumbaji amemjaalia papa mweupe, kama jina lake linavyojieleza, kuwa na rangi nyeupe tumboni, ingawa ana rangi ya bluu katika sehemu nyingine za mwili.

Mkia wake una nguvu sana na humsaidia katika kuogolea. Papa huyu kasi ya kilomita 24 kwa saa. Papa huyu, mara nyingi, hupendelea kutembea katikati ya bahari na anapotembea anaangalia malisho yake kwa juu.

Papa huyu ni aina ya samaki mwenye meno mengi sana. Wataalamu wanasema wana meno Zaidi ya 300, juu na chini. Mwenyezi Mungu amejaalia kila meno yake yanapotoka, yanaota tena. Meno yake yalivyo ni kama vile ncha ya mshale. Ni meno maalumu kwa kung’ata na kukata.

Wanapokuwa wadogo, papa weupe wanakula samaki wadogo na ndege; na wanapokuwa wakubwa wanakula samaki kama vile kasa na wengineo. Mbali na viumbe hawa kuwa hatari, kama ilivyo kwa viumbe wengi, hawakosi maadui. Adui mkubwa wa papa mweupe ni binadamu na nyangumi. Binadamu wanawavua, nao nyangumi huwala hawa papa.

Katika Nchi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, wanapovuliwa samaki hawa huwa tunafurahia kwakuwa tunapata utowezi na tunafurahia nyama, yake lakini kule Asia hasa katika sehemu za China hawapendi papa. Papa akivuliwa, wanachukua zile mapezi (fins), ambazo kwao ni dawa ya maradhi mbalimbali.

Ndugu yangu msomaji, hakika kiumbe huyu ana maajabu mengi. Mbali ya hayo, amejaaliwa uwezo mkubwa sana wa kunusa harufu ya tone moja la damu kiasi cha umbali hata wa kilomita tano na akaja mara moja.

Kwa hali hiyo, inaelezwa kuwa ni hatari kujikata baharini na kutokwa na damu kwani jambo hilo ni kualika mashambulizi ya papa mweupe!

Maajabu mengine ya samaki huyu ni kuwa haijulikani wanavyozaa kwani wanasayansi hawajawahi kuwaona wakipandana, tofauti na viumbe wengine. Wanachokijua wanasayansi ni kuwa, papa hawa wanaangulia mayai yao tumboni.

Jambo linaloshangaza zaidi ndani ya tumbo la samaki huyo ni kwamba, baada ya mayai kuanguliwa yangali tumboni, basi hutokea wale watoto wawili wa kwanza kuyala mayai. Pia, ikipotokea wa kwanza akawa mkubwa kiasi, basi anaweza kuamla yule mwenzie. Kwa sababu hii, papa hawa huzaliwa wachache.

Kuna kipindi samaki hawa huonekana wakikimbia kati kati ya bahari. Katika kipindi hicho, baadhi ya watafiti wanaaamini hicho ndiyo kipindi ambapo wanakwenda kupandana. Hata hivyo, jambo hili halina uhakika, bali ni dhana tu.

Papa mweupe ni katika samaki ambao wanaweza kusafiri masafa marefu sana hadi kilomita 5,000. Licha ya yote hayo, kuna mengi ambayo hayafahamiki kuhusu samaki huyu. Mpaka leo, watafiti hawajui anaishi miaka mingapi wala idadi ya mayai yanayototolewa tumboni.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close