1. Fahamu Usiyoyajua

Paka wa jangwani

Ndugu yangu msomaji wa safu hii ya ‘Fahamu Usiyoyajua,’ juma hili nataka kukupa dondoo chache kuhusu mnyama aitwaye paka wa jangwani (sand cat).

Huyu ni paka aishiye jangwani – kwenye mchanga na mawe. Ni paka aishiye mbali na vyanzo vya maji. Paka huyu anapatikana katika nchi mbalimbali za Jangwa la Sahara katika nchi za Morocco, Algeria, Niger, Chad na Misri. Paka wa Jangwani pia anapatikana katika majangwa yaliyopo bara Asia.

Paka huyu mwenye urefu wa kati ya sentimita 39 hadi 52, ana kichwa kikubwa na masikio yaliyo juu ya uso yanayomfanya kuwa miongoni mwa wanyama wenye uwezo mzuri sana wa kusikia na hivyo k u m w i n d a adui kirahisi. Manyoya yake ni marefu na hufunika hadi nyayo zake ili kumlinda dhidi ya joto kali na baridi ya jangwani.

Allah, Mbora wa Uumbaji, amejaalia rangi ya mwili wa paka huyu kuwa inafanana na maeneo anayopendelea kuwepo yaani rangi ya mchanga wa jangwa. Hali hii humsaidia asiweze kuonekana kiurahisi katika mazingira (camouflage).

Kufanana kwake na mchanga wa jangwani kunamfanya aweze kukamata mawindo kirahisi. Pia, rangi hiyo huwapa ugumu (kwa kule kutokutambulika kirahisi) watesi wake wanaotaka kumshambulia.

Ukiacha mwili uliopambambwa na rangi ya hudhurungi au kijivu, masikio yao yana rangi nyeusi. Pia, katika kona ya macho kuna mstari mwekundu unaoshuka hadi kwenye mashavu.

Umri wao wa kuishi ni miaka 13 na hata wale ambao wanafugwa ni nadra kuzidi umri huo.

Tabia

Paka wa jangwani wanapenda kunyunyiza mikojo yao katika maeneo yao ili uwepo wao utambulike kwa wenzao. Hii pia ni tabia ya simba, chui na wanyama kadhaa wengine hasa wa jamii ya paka.

Sauti za milio yao wanapolia zinafanana sana na sauti za paka hawa wa kufugwa majumbani. Pia, paka hawa wanapenda sana kuwa peke yao (solitary). Muda pekee wa dume na jike wanakuwa pamoja ni wakati wa kupandana.

Uzazi na chakula

Paka wa jangwani hukomaa baaada ya mwaka mmoja. Jike hubeba mimba kwa siku 59 hadi 66. Paka hawa huzaa kipindi cha baridi na mara nyingi huzaa watoto wawili au watatu. Ni nadra kuzaa mmoja.

Kwa upande wa chakula, paka wa jangwani hupenda kula panya, ndege na hata nyoka wakiwemo wale wenye sumu kali. Muda wao mzuri wa mawindo ni usiku. Wataalamu wanasema, paka hawa huwazidi sana nyoka wakali akili na hivyo kuwaua na kuwala.

Kila anayekula naye huliwa. Utafiti unaonesha kuwa, maadui wakubwa wa paka huyu ni mbwa mwitu, nyoka wakubwa na vilevile binadamu.

Mambo 6 usiyoyajua kuhusu paka wa jangwani

  • Paka wa jangwani hukomaa (baleghe) wakiwa na umri wa kati ya miezi 10 hadi 12.
  • Paka huyu ambaye jina lake la kisayansi ni Felis margarita ndiye pekee anayeishi jangwani.
  • Ni katika wanyama ambao idadi yao imekuwa inapungua. Kwa sasa wanakadiriwa kuwa takriban elfu 27. Kupungua huku kunatokana na kuingiliwa makazi yao, ujangili, uwindaji.
  • Sababu kubwa ya kupendelea kufanya mawindo yao usiku ni kuepuka joto wakati wa mchana ambapo mara nyingi joto hufikia hadi nyuzi 52°C.
  • Paka wa jangwani wana uzito wa kilogramu 3.5 au chini ya hapo. Ingawa kimuonekano ni kama paka wa nyumbani; hawa ni wanyama wakali, wawindaji wazuri, na wasioogopa. Hupambana hata na nyoka mwenye sumu kali na kumfanya kitoweo na wanaishi kwenye mazingira magumu yenye uhaba wa maji. Usiku kwao ndiyo muda sahihi wa kuwinda.
  • Paka wa jangwani wanalia kama paka wa kawaida wa kufugwa lakini pia wanabweka kama mbwa.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close