1. Fahamu Usiyoyajua

Orangutan: Sokwe anayepatikana Indonesia na Malaysia

Naam ndugu yangu mfuatiliaji wa makala kuhusu viumbe wa Allah, Mbora wa uumbaji, leo ninakuletea dondoo chache kuhusu mnyama aitwaye ‘orangutan.’

Neno orangutan linatokana na maneno ya Kimalaysia ‘orang’ na ‘hutan’ likiwa na maana ya ‘mwanadamu wa msituni.’ Hata hivyo, huyu katu si binadamu. Waswahili humuita mnyama huyu ‘pongo.’ Mnyama huyu ni moja kati za aina ya sokwe na anapatikana katika Bara la Asia katika nchi za Indonesia na Malyasia hususan katika visiwa vya Borneo na Sumatra.

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanasema wanyama hawa walikuwepo kwa miaka mingi sio tu katika misitu ya Indonesia na Malaysia bali pia katika maeneo mengine ya Asia hususan Kusini mwa China. Kuna aina mbili za sokwe orangutan, wakiwemo orangutan wa Kiborneo na orangutan wa Kisumatra.

Maisha ya sokwe orangutan yanashangaza sana. Orangutan ana umbile kubwa hasa sehemu za mikononi na kifuani na amejaaliwa manyoya mengi yanayoonekana pembezoni mwa mikono yake na katika sehemu za mabega mpaka mgongoni.

Orangutan ana rangi nyekundu ya kiza au damu ya mzee, kama ambavyo wengine huiita. Mnyama huyu ana uzito wa takriban kilogramu 50 hadi 100 na urefu wa mita 1.2 hadi mita 1.4. Umri wao wa kuishi ni mrefu si haba. Kwa mujibu wa wataalamu orangutan anaweza kufikisha hadi kati ya miaka 30 hadi 40 lakini wa kufugwa huweza kuishi hadi miaka kati ya 50 na 60. .

 Chakula na uzazi

Kwa upande wa chakula, orangutan wanakula mimea na nyama (omnivorous). Riziki yao huitafuta riziki nyakati za mchana na hutumia usiku kupumzika. Orangutan wanakula vitu vingi vikiwemo matunda, majani, asali, wadudu, mayai ya ndege na hata udongo. Utafiti unaonesha kuwa wanyama hawa wanakula zaidi ya aina 500 za mimea, kati ya hiyo asilimia 60 ni matunda.

Orangutan hubeba mimba na kuzaa. Mimba yao, kama ilivyo kwa mwanadamu, huchukua takriban miezi tisa. Kawaida, Orangutan huzaa mtoto mmoja, na mara chache huzaa mapacha.

Mambo 10 Usiyoyajua kuhusu orangutan

 • Sokwe orangutan wamejaaliwa akili nyingi sana kiasi kwamba huweza kutumia zana. Kwa mfano, kama kuna wadudu kwenye tundu la miti, wanaweza kuchukua kijiti kuwatoa na kuwala. Sokwe orangutan pia wanaweza kutumia mawe kuvunjia mbegu ili wapate karanga.
 • Orangutan hutengeneza kiota cha kulalia juu ya miti kwa kutumia majani na matawi ya miti. Hii inawasaidia kuwaweka salama dhidi ya wanyama wakali ambao ni maadui zao kama vile chui. Na wakati wa mvua, orangutan wana uwezo wa kutengeneza majani mfano wa mwamvuli ili kujiziba na mvua.
 • Wataalamu wanasema orangutan ni jamaa wa karibu zaidi wa wanadamu na kwamba tuna mfanano wa vinasaba (DNA) kwa karibu 97%. Inasimuliwa kuwa orangutan wamewahi kutumia boti kuvuka mto kwa kuiga baada ya kuona wanadaamu wakifanya hivyo. Kisa hiki ni kwa mujibu wa Bustani ya wanyama ya San Diego. (Sani Diego Zoo).
 • Orangutan hutumia muda wao mwingi juu ya miti. Kwa mikono yao mirefu, yenye nguvu na umbo la ndoano, orangutan hupanda na kuhama kutoka tawi hadi tawi.
 • Orangutan jike huzaa mara moja kila baada ya miaka nane. Watoto wachanga hukaa na mama yao kwa miaka sita hadi saba mpaka wakijifunza stadi muhimu za maisha. Baada ya hapo hutoka kwenda kujitegemea. Kwa hiyo, mama, kwa orangutan, ni muhimu mno.
 • Orangutan wanaweza kutembea kwa miguu yake ya nyuma tu akiwa amesimama, kama ilivyo kwa wanadamu.
 • Tofauti na nyani wengine wakubwa kama sokwe na bonobos, orangutan hawapendi kuishi katika vikundi.
 • Oranguten jike anaweza walau anaweza kuwa na mwanawe lakini madume wanapenda kuwa peke yao.
 • Sokwe orangutan ni wanyama wenye kelele wakiamua. Kelele zao huweza kusikika hadi umbali wa maili 1.2 (sawa na kilometa mbili). Ni ma- orangutan madume ndio wapigao kelele hizi ili kutishana wasiingiliane katika maeneo yao.
 • Hawa ni miongoni mwa viumbe walio katika hatari kubwa ya kutoweka kwa sababu ya maeneo yao kuingiliwa na shughli za wanadamu ikiwemo ukataji magogo, uchimbaji dhahabu na uchomaji misitu. Shirika la kimataifa la uhifadhi wa asili (IUCN) limewaweka orangutan katika kundi la wanyama walio katika hatari kubwa ya kutoweka (critically endangered).
 • Majike ya orangutan yana mfumo wa ajabu wa uzazi. Wanazaa mara moja katika kila miaka nane. Rekodi zinaonesha kuwa hiki ni kipindi kirefu zaidi kati ya uzazi hadi uzazi ukilinganisha na mwenendo wa wanyama wote wengine duniani. Na pia wanyama hawa huendelea kuzaa kwa zaidi ya miaka 30 ya uhai wao.
 • Orangutan ndio wanyama wakubwa zaidi walau matunda duniani. Kuna zaidi ya aina 300 za matunda katika wanayoweza kuyala katika mazingira yao.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close