1. Fahamu Usiyoyajua

OKAPI: Mnyama anayepatikana nchi moja tu duniani

Okapi ni kati ya wanyama wenye kwato zilizogawanyika kati kama ilivyo kwa mbuzi, kondoo na kadhalika. Mnyama huyu anapatikana katika Bara la Afrika tu katika Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huko Kaskazini Mashariki katika misitu wa mvua.

Wataalamu wa elimu ya viumbe husema kuwa okapi na twiga ndiyo pekee waliobakia katika kundi la Girrafidae. Okapi, kimuonekano, ana miraba kama ya pundamilia lakini kinasaba yupo karibu zaidi na twiga. Rangi yake ni kahawia na wengine ni wekundu wa kahawia.

Urefu wa okapi ni mita moja na nusu, wakati Uzito wake ni kilogramu 200 hadi 350. Okapi amejaaliwa kuwa na shingo ndefu na kichwani kwake, kwa dume, ana pembe kama zile za twiga. Badala yake, majike ya Okapi yana manyoya laini kichwani. Okapi ana masikio makubwa, yaliyosimama na yanayokamata sauti kirahisi na hivyo kumsaidia kuepuka hatari.

Okapi si wanyama wanaoishi kijamaa bali ingawa mara kadhaa huonekana wakiwa pamoja katika vikundi vidogo wakiwa wanakula na hata kucheza.

Chakula na uzazi

Okapi hula majani ya miti, nyasi na matunda Yeye kitaalamu huitwa ‘herbivorous’ (wanyama walao mimea tu). Okapi hutafuta riziki mchana na jioni na hupumzika zaidi usiku.

Kwa upande wa uzazi, okapi hubeba mimba kwa siku 440 hadi 450, kisha huzaa mtoto mmoja. Kitoto cha okapi huanza kunyonya mara tu baada ya kuzaliwa hadi anapofikisha miezi mitatu. Baada ya miezi mitatu, okapi huanza kula majani huku akiendelea pia kunyonya. Baada ya miezi sita, okapi huacha kabisa kunyonya.

Mambo 7 usiyoyajua kuhusu okapi

  • Kama vile ilivyo kwa twiga na ng’ombe, okapi ana matumbo manne ambayo husaidia kumeng’enya majani magumu aliyoyala.
  • Okapi ana ulimi mrefu, mweusi ambao unaweza kumsaidia kuvuta majani kwenye matawi akiwa mbali. Okapi wana tabia ya kutenga maeneo yao kwa kutumia kwato zao ambazo huacha alama nene inayoonekana wazi. Madume hutumia mkojo kuweka alama zao.
  • Ndama wa okapi ana uwezo wa kutembea dakika 30 tu baada ya kuzaliwa lakini hawezi kujisaidia, siyo haja kubwa wala ndogo, mpaka afikishe umri wa mwezi mmoja.
  • Wataalamu wanasema kuwa Okapi anawasiliana na mwanawe kwa kutengeneza sauti (infrasound) mfano wa kelele ambazo haziwezi kusikika kwa sikio la mwanadamu.
  • Okapi huwa hataki masikhara kabisa kwa watoto wake, na hivyo ni mkali sana pale mtoto wake anapotaka kudhuriwa na adui.
  • Kwa mujibu wa takwimu za Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili (IUCN), okapi ni aina ya viumbe walio hatarini. Ingawa haijulikani ni wangapi wanasalia porini, wanasayansi wanakadiria kwamba idadi yao inaweza kuwa imepunguzwa kwa nusu katika miongo miwili iliyopita.
  • Kuanzia maumivu ya uzazi yanapoanza hadi kujifungua (labour period) ni saa 3 – 4.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close