1. Fahamu Usiyoyajua

Nyumbu: Wanyama waoga, wasahaulifu na wasiosaidiana

Shukrani zote ni kwa Allah Aliyretukuka aliyeumba kila kitu, na rehema na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad pamoja na Ahli zake na Maswahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Kwa hakika kuwepo kwa Allah Aliyetukuka hakuna shaka ndani na dalili ya kuwepo kwake ni uumbaji wake ambao atharinyake tunaiona kupitia viumbe vyake.

Juma hili, tumsome nyumbu, mnyama mkubwa anayepatikana Afrika katika maeneo ya Savanna. Huyu ni katika wanyama ambao hawapendi maeneo ya ukame au yenye unyevunyevu mwingi. Maeneo yao ya kukidai ni uwanda wa nyasi fupi na vichaka vya hapa na pale (Savanna).

Wataalamu wanasema kuwa kuna aina mbili za nyumbu, wa rangi nyeusi na wale wenye mng’ao wa bluu au kahawia. Katika ukanda wa Afrika Mashariki, hususan Tanzania na Kenya ndiyo wanapatikana zaidi nyumbu wenye mng’ao wa bluu au kahawia ambao ni wakubwa zaidi. Nyumbu pia hupatikana kusini mwa Afrika katika nchi za Angola, Zambia, Afrika Kusini Zimbabwe, Msumbiji, na hata katika Nchi ya Swaziland.

Nyumbu huishi kijamaa katika kundi moja kubwa na ni nadra kumkuta mmoja peke yake. Pia, hupenda kujichanganya na wanyama wengine kama pundamilia, nyani wakubwa na baadhi ya ndege wakiwemo yangeyange.

Tabia yao ya kujichanganya inatajwa kuwa ni mbinu ya kujikinga dhidi ya maadui zake. Nyumbu ana uwezo mdogo wa kufikiri hususani katika maeneo ya hatari. Wanaweza kuwa na kiu wakenda kunywa maji mtoni kwenye mamba, lakini hata mwenzao akiliwa wataendelea kunywa maji hapo hapo au watarudi siku nyingine na kusahau balaa walilokumbana nalo mara ya mwisho.

Nyumbu hawana utamaduni wa kusaidiana pindi mmoja wao anapokamatwa au kufukuzwa na adui bali kila mmoja anatafuta namna ya kujiokoa mwenyewe.

Uzazi, chakula na tabia zao

Nyumbu anazaa pale mvua zinapoishia. Nyumbu huzaliwa na uzito wa haid kg 21 na ni kawaida kwa nyumbu ndama kuongozana na wakubwa. Nyumbu huwa hawana muda wa kuwatunza ndama wao.

Nyumbu hula mimea (herbivorous), wakipendelea zaidi majani mafupi.

Kitabia, wanatabia za kushangaza. Mfano, hawasaidiani mwenzao anapopatwa na tatizo, hususan akishambuliwa na adui. Pia hupenda kuhamahama kwa makundi makubwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Katika Mbuga ya Serengeti, nyumbu nao ni katika wanyama wanaohama kuelekea Mbuga ya Masai Mara nchini Kenya kutafuta malisho, wakiwa katika kundi kubwa na pia wakiwa wamechanganyikana na wanyama wengine.

Hata hivyo siyo nyumbu wote wana tabia ya kuhamahama bali ni wale tu wenye mng’ao wa bluu au kahawia. Nyumbu weusi huwa na eneo maalum kwajili ya malisho.

Mbali ya yote hayo, nyumbu pia ni waoga na wasahaulifu.

Maumbile sita ya nyumbu yanayofanana na wanyama wengine

Ndugu msomaji, Allah Mbora wa Uumbaji amemjaalia nyumbu kufanana kimaumbile na wanyama wengine kadhaa.

  • Sehemu ya miguu ya nyuma na kiuno cha nyumbu wanafanana na fisi.
  • Mkia wao ni kama wa farasi
  • Michirizi yao ni kama ya la pundamilia.
  • Pembe zao ni kama za nyati au ng’ombe.
  • Ndevu zao hazina tofauti na za pofu na
  • Nywele za mgongoni zinawiana na za pundamilia.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close