1. Fahamu Usiyoyajua

NJIWA: Ndege wasiopenda fujo

Ndugu msomaji wa safu hii, juma hili tunamsoma ndege aina ya njiwa. Njiwa ni aina ya ndege wafugwao waliojaaliwa kuwa na rangi mbalimbali zinazopendeza katika mbawa zao zikiwemo nyeupe, nyeusi, kijivu. Ndege huyu maarufu duniani kote anatajwa kuwa ni rafiki mkubwa wa binadamu.

Njiwa huishi kwenye viota ambavyo huvijenga wao wenyewe kwa kutumia vijiti au miwamba. Pia, njiwa ni ndege mpenda amani, asiyependa usumbufu na hivyo wana tabia ya kuhama nyumba zenye magomvi na kwenda kukaa sehemu zenye utulivu. Ni vigumu kwa njiwa kuishi katika sehemu kunakofugwa paka; na huweza hata kuhama mahali hapo kwani paka ni miongoni mwa maadui zao wakubwa! Kwa upande wa chakula, njiwa hupendelea kula nafaka kama mtama, mahindi, mbaazi na kadhalika. Pia hula matunda na baadhi ya mimea (majani).

Njiwa ndiyo viumbe pekee duniani wenye mpenzi mmoja. Hata hivyo, njiwa anaweza kubadilisha mpenzi ikitokea yule mwenza ameuzwa mbali, amekufa au amepotea.

Matano usiyoyajua kuhusu njiwa

  • Njiwa huenda ndiyo ndege wa kwanza kufugwa na mwanadamu kwani kumbukumbu zao zipo kwenye kazi za sanaa za miaka mingi iliyopita hadi 4500 BC. Kazi hizo ziligundulika huko Iraq.
  • Kwa upande wa uzazi, njiwa jike kwa kawaida hutaga mayai mawili – hazidishi wala hapunguzi. Na vilevile, kawaida njiwa huzaa jike na dume. Na hao jike na dume, wakikua huanzisha mahusiano na kuendelea kuzaliana.
  • Njiwa ni ndege wasiopenda fujo. Kama ukiwafuga katika nyumba iliyojaa ugomvi na vurugu, ndege hawa huamua kuondoka.
  • Ukimfuga njiwa; hata akiruka umbali gani, hasahau nyumbani. Lazima atarudi kwao. Tafiti zinaonesha kuwa njiwa anaweza kurejea nyumbani hadi umbali wa kilomita 2000! Hii ni hatari kwa wale wanaonunua njiwa kwa mtu kwa ajili ya kutaka kuwafuga. Njiwa hao walionunuliwa ni rahisi kurudi kwao. Mbaya zaidi, hata ukipita muda mrefu, mathalan mwezi mmoja, njiwa bado anaweza kurudi nyumbani kwao.
  • Njiwa ndiyo viumbe pekee duniani wenye mpenzi mmoja. Hata hivyo, njiwa anaweza kubadilisha mpenzi ikitokea yule mwenza ameuzwa mbali, amekufa au amepotea. Hata hivyo, ikitokea mwenza wake kurudi, kama ameanzisha uhusiano mpya na mwengine, atamkataa na kumrudia mwenza wake wa zamani.
  • Njiwa hutajwa kuwa wazazi wazuri sana kwani dume na jike wote hushirikiana katika jukumu la kuwalisha watoto.
  • Stadi moja imeonesha kuwa, akipewa mafunzo sahihi, njiwa anaweza kutumika katika fani ya utabibu kung’amua kansa, tena kwa usahihi kabisa, kama ambavyo dokta anaweza. Hii ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanyika huko Marekani.
  • Njiwa anaweza kupaa hewani kwa kasi kubwa sana na kwa umbali mrefu. Baadhi ya aina ya njiwa huweza kwenda kwa kasi ya hadi kilomita 160 kwa saa moja.
  • Utafiti umethibitisha kuwa, njiwa wana uwezo mkubwa wa kujua watu wema kwao. Na hii hutokea kwa sababu ndege hao wana uwezo mkubwa wa kukumbuka sura za watu wanaokutana nao.
  • Njiwa wametumika sana katika kutuma ujumbe katika Vita ya Kwanza na ya Pili ya Dunia. Njiwa mmoja katika Vita ya Kwanza ya Dunia mwaka 1918, aliokoa wanajeshi 194 wa Marekani ambao walizingirwa na adui. Baada ya njiwa wawili kuuawa, njiwa wa tatu aliyeitwa Cher Ami alifanikisha kupeleka ujumbe (licha ya jaribio la kutaka kumuua) na hivyo wanajeshi hao wakaokolewa. Kwa ushujaa wake, njiwa huyo alipewa nishani.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close