1. Fahamu Usiyoyajua

NGUVA: Ng’ombe wa baharini

Sifa njema zote anastahiki Mola Muumba wa mbingu na nchi na vilivyomo baina ya mbingu na ardhi ikiwemo binadamu, mimea na wanyama. Ni hakika yenye hakika kuwa Allah ndiye peke anayestahiki kuabudiwa kwani yeye sio tu ndiye Muumba wa kila kitu baki pia ndiye anayeruzuku vumbe hai wote.

Kwa mara nyingine tukumbushane dalili na alama za uwepo wa Mwenyezi Mungu na ukubwa wake kupitia viumbe vyake. Ndugu yangu msomaji, tujifunze kuhusu kiumbe wa Allah aishiye baharini anayeitwa ‘nguva.’

Nguva ni kiumbe wa baharini aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na kuzushiwa kuwa ana umbo la nusu samaki nusu mtu. Uvumi huu umepelekea baadhi ya watu kuhariri picha zikionesha kiumbe anayedhaniwa kuwa ndiye nguva, akiwa na nusu mtu (kichwani mpaka kiunoni) nusu samaki (kiunoni mpaka chini). Ukweli ni kuwa, hakuna kiumbe wa aina hiyo; bali huo ni uzushi tu.

Nguva ni kiumbe wa baharini kama walivyo viumbe wengine na wala hana mahusiano na ubinadamu hata kidogo.

Kwa mujibu wa wataalamu, nguva si samaki bali ni mamalia, kama ilivyo kwa nyangumi na mamalia wengine wa baharini. Ukiacha kuzaa na kunyonyesha, jambo jingine linalothibitisha kuwa nguva sio samaki ni ukweli kwamba, hawezi kupumua ndani ya maji, kama semaki wengine bali hutoa pua yake juu ya maji ili kuvuta hewa na kisha kuzama tena majini.

Nguva ana mwili mkubwa ulio mviringo na shingo isiyoonekana au kushikana na kichwa chake kidogo kilicho na macho madogo.

Sehemu ya pua ya nguva ni kubwa, nyororo, butu na yenye manyoya kama miba. Kinywa chake cha juu ni nyama kubwa inayokaa kama ilioangukia mdomo na kwa chini inafanana na kiatu cha farasi. Nguva ana rangi ya kijivu na udongo; lakini rangi hiyo ya kijivu imekolea zaidi sehemu ya juu kuliko ya chini. Kiumbile, nguva wanaweza kufikia urefu wa mita 2.5 hadi 4 na uzito wa kg 1,500.

Nguva ni mamalia anayependelea kuishi kwenye maeneo ya kina kifupi katika maji ya tropiki (katika nchi za joto) katika maeneo yote ya bahari ya Hindi na Pasifiki. Lakini pia viumbe hawa wanapatikana katika bahari ya Carribean, Afrika ya Magharibi na katika mto wa Amazonas.

Inasemekana Katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, nguva wana hatari kubwa ya kutoweka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uharibifu wa maeneo yao ya malisho, kukamatwa kwenye nyavu za uvuvi na kuwindwa.

Ikiwa nguva atakamatwa kwenye nyavu iliyotegwa chini ya maji, hufa mara moja kwa kushindwa kuja juu kuvuta hewa.

Hatari hii inayowakabili ndio inafanya viumbe hawa wahifadhiwe rasmi chini ya Sheria ya Taifa ya Uvuvi na wameorodheshwa na Shirikisho la Uhifadhi Duniani (IUCN) kama wanyama walio katika tishio la kutoweka.

Wataalamu husema, kutokana kuwindwa, idadi ya nguva nchini imepungua mno, ingawa jitahada zinafanyika kuchunguza waliyoripotiwa kuonekana ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na wenyeji ili kuelewa vizuri ukubwa wa idadi yao kwa sasa.

Uzazi na chakula

Katika uzazi, nguva wanazaa mtoto mmoja tu baada ya kukutana na kubeba mimba kati ya miezi 13 hadi 15.

Ndama aliyezaliwa anaweza kufikia uzito wa kilo 30 na hunyonya kwa kipindi cha miaka miwili na nusu hadi mitatu. Jike la nguva linakuwa tayari kuzaa anapofikisha umri wa miaka kati ya 10 hadi 17.

Nguva hula majani ya baharini ambapo hung’oa mmea wote na kuacha alama ya sehemu walizokula. Ushahidi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba nguva pia hula wanyama wadogo wa bahari.

Mambo usiyoyafahamu kuhusu nguva

  • Nguva ni wanyama watulivu, hawana vishindo wala fujo hata katika kuibuka kwa ajili ya kuvuta pumzi kila baada ya dakika tatu au zaidi.
  • Endapo nguva jike atazaa mtoto dume, atahitaji kujitenga na kundi la nguva wengine kwa kuhofia mtoto wake kuuwawa na dume kubwa katika kundi.
  • Nguva huogelea kwa kutumia mkia wake bapa, kama wa nyangumi, akisaidiwa na mapezi ya mbele kwa kujihimili na kugeuka.
  • Tofauti na wanyama wengine wa majini kama vile nyangumi au pomboo, nguva hawezi kuzuia pumzi kwa muda mrefu haswa anapokuwa anaogelea kwa kasi.
  • Nguva wana uwezo mdogo wa kuona lakini wana uwezo mkubwa wa kusikia.
  • Meno ya nguva yapo kama vipembe kiasi yanaweza kuonekana haswa kwa nguva dume na baadhi ya majike yenye umri mkubwa.
  • Wakati wa kuzaliana, nguva dume hutumia vipembe vyao kupigana na madume wenzake.
  • Nguva wanaweza kuishi hadi kufikia miaka 70
  • Ndama wa nguva anapozaliwa huwa na urefu wa kama mita moja nukta mbili na hunyonya kwa mamake kwa miezi 18.
  • Nguva analindwa chini ya usimamizi na udhamini wa mashirika ya uhifadhi duniani ikiwemo IUCN na mengineyo.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close