1. Fahamu Usiyoyajua

NG’E:Mdudu anayeweza kukaa muda mrefu bila kula

Kwa hakika, hakuna shaka juu ya kuwepo kwa Allah Aliyetukuka na dalili ya kuwe ni viumbe vyake alivyoviumba ambavyo tunaviona na tusivyoviona.

Ni kwa faida yako msomaji wangu, kama wakati wote utakuwa unatafakari kuwepo kwa Allah Mbora wa uumbaji na nguvu zake, dalili na maamuzi yake kuhusiana na maisha haya na yale yajayo.

Kutafakari uwepo wa Allah ni njia ya kujinyenyekeza katika ibada. Kwa hakika hakuna mwingine anayestahiki kuabudiwa kwa haki kama Allah, ambaye kupitia viumbe vyake tunavyovisoma kuna mazingatio makubwa kama tutamakinika.

Juma hili acha tukaone ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwa kumtazama mdudu Nge. Nge, ni mdudu anayewinda kwa kushambulia, ni kiumbe aliyejaaliwa kuwa na miguu nane ingawa kama usipomtazama vizuri utasema ana miguu sita. Ile miwili mingine ipo mbele kabisa, unaweza usiione.

Nge amejaaliwa kuwa na mkia mrefu ambao mwishowe una mwiba wa kumdungia adui. Wataalamu wa elimu ya viumbe wanasema, kuna takriban aina 1750 za Nge, kati yao aina 13 wametoweka. Hata hivyo, wataalamu wameshindwa kujua sababu ya kutoweka aina hizo 13, ila Allah pekee ndiye mwenye kujua mambo ya siri na ya dhahiri.

Nge ni wadudu wanaopatikana karibu kwenye maeneo yote ya dunia isipokuwa zile sehemu za ncha ya Kaskazini. Wapo kuanzia wenye urefu wa kuanzia milimita 9 hadi sentimita Mwili wa nge umegawanyika katika sehemu mbili kichwa na kiwiliwili.

Katika zile aina 1750 nilizokutajia, ni aina 25 pekee ambao wanatajwa kuwa na sumu inayoweza kumuua binadamu. Sumu ya nge inabadilika ukali na wanasayansi wanasema itaendelea kubadilika ukali, ingawa hawajajua sababu.

Nge anagonga kwa kutumia ncha ya mkia na anapokugonga inauma sana. Mara nyingi anapokugonga haina madhara makubwa kwa binadamu ila kama ikitokea ukagongwa ukapata maumivu makali ni bora uenda Hospitali.

Uzazi na chakula

Katika uzazi, nge wanazaliana kwa jike na dume kukutana katika namna Wanasayansi wanasema ni tata na ya kushangaza sana (complex).

Katika kukutana huko, kwanza husikika harufu ambayo inawasaidia kutambuana. Kwa harufu hii, kila mzazi hujua kuwa mwenza wake yupo tayari kwa uzazi.

Dume huwa ndio linalomuongoza jike kuelekea sehemu ambayo wanaenda kukutana (kupandana). Kuna wakati mwingine dume la nge linaweza kuweka sumu katika sehemu ile ya uke wa nge, sio kwa ajili ya kumuua bali katika kuamshana kihisia. Jike huwa halitoi mayai nje bali dume hutia mbegu na mayai yanayokomaa ndani ya tumbo la jike. Kisha, watoto wanaanguliwa ndani ya tumbo.

Baada ya kuzaliwa, mama yao anavibeba vitoto mgongoni ili kuwalinda dhidi ya maadui.

Kwa upande wa chakula, nge wadogo wanakula minyoo na viwavi.Nge wakubwa wanakula panya wadogo pamoja na mijusi.

Mambo 10 usiyo yafahamu kuhusu nge

  • Kuna wakati mama anaweza kula watoto wake na kuna wakati watoto wanaweza kumla mama yao.
  • Nge ana kitu, mfano wa kemikali mdomoni inayoanza kumsagasaga kiumbe na kumfyonza kabla hajammeza. Hii ni kwa sababu hawezi kula kitu kigumu.
  • Nge wanaweza kumshika kiumbe na kumuua kwa ile mikono (au unaweza kuita miguu ya mbele) yao kisha wanamtia sumu ambayo inamlemaza kiumbe na kufa
  • Nge anaweza kuzaa hadi watoto 100. Kuna aina nyingine za nge wanachukua muda mrefu (hadi miezi 9) kuzaa tangu apandwe na dume.
  • Nge akimulikwa na mwanga fulani unaitwa Ultra Violet (UV) huwa anang’aa sana na kuwa na rangi kama ya kijani hata kama yupo gizani.
  • Nge wanafanana na mama yao lakini mara nyingi wakiwa wadogo wanakuwa na rangi nyeupe.
  • Nge anaweza kukaa muda mrefu bila ya kula. Ngozi ya nge inabadilika mara kwa mara katika kukua kwao (hadi mara saba).
  • Kwa nge wenye sumu, hawakusudii kumdhuru binadamu bali ni kwa ajili ya mawindo yao na ulinzi dhidi ya viumbe wanaotaka kuwashambulia.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close