1. Fahamu Usiyoyajua

Muhogo: Chakula Kinachotegemewa Zaidi Barani Afrika

Naam ndugu msomaji wa safu hii ya Fahamu Usiyoyajua, leo tunazungumzia mambo kadhaa kuhusu zao maarufu la muhogo. Muhogo ni moja kati ya mazao ya chakula na biashara ambalo hustahimili ukame na huweza kustawi katika udongo usio na rutuba ya kutosha.

Joto linalofaa zaidi kwa ustawi wa muhogo ni kati ya nyuzi joto 25-30. Muhogo hudumaa ikiwa joto litapungua kufikia nyuzi 10 au chini kwani haiwezi kustamihili baridi kali, hasa ukungu kwa muda mrefu katika kipindi chake cha ukuaji.

Ndugu msomaji, muhogo ni zao la tatu miongoni mwa mazao ya wanga linaloweza kustawi katika nchi zenye joto au tropiki. Zao la kwanza ni mahindi na la pili ni mchele. Barani Afrika muhogo hulimwa sana katika nchi za ukanda wa jangwa la Sahara. Asilimia 60 ya kilimo chake kinafanywa kwenye nchi tano; Nigeria, Brazil, Thailand, Indonesia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo [DRC] huku Nigeria ikishika nafasi ya kwanza kwa kulima kwa wingi zao la muhogo.

Hata hivyo, Thailand ndio inayoongoza kuuza mihogo nje ya mipaka yake. Asilimia 80 ya mihogo inayouzwa kwenye soko la kimataifa  inatoka nchini humo huku Vietnam na Indonesia zikifuata, kila moja ikiwa na asilimia nane tu. Kiasi kinachobaki kinatoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani [FAO], muhogo ni zao la tatu kwa kuwa na kiwango kikubwa cha wanga nyuma ya mchele na mahindi. Inakadiriwa zaidi ya watu milioni 800 Duniani kote wanategemea mihogo kwa chakula, kati ya hao milioni 500 wapo Afrika.

Asili ya muhogo

Muhogo ulianza kulimwa miaka elfu kumi iliyopita huko Amerika ya kusini katika nchi ya Brazil. Katika maeneo mengi ya Brazil hasa porini, mihogo hustawi yenyewe [bila ya kupandwa]. Muhogo ni zao lenye faida na hasara pia. Kuna mihogo mitamu na michungu [yenye aina fulani ya sumu inayojulikana kama ‘Cynaid’].

 

 

Je, utaijuaje mihogo yenye sumu?

Wataalamu wa masuala ya mimea wanashauri watu kuwa makini na mihogo yenye rangi ya manjano na kijani kwa ndani kutokana na madhara yake makubwa kiafya. Mihogo mizuri ni ile yenye rangi nyeupe kwa ndani. Muhogo ni chakula kinachotegemewa sana barani Afrika hasa wakati wa ukame. Kwa waislamu, muhogo hutumika kama futari wakati wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwingineko, watu wengi katika nchi za Afrika ikiwemo Ghana, Togo na Benin wanaamini hakuna maisha bila muhogo.

Ifuatayo ni orodha ya nchi zinazolima kwa wingi zao la muhogo kwa mwaka Nigeria tani milion 57.1 Thailand tani milion 31.1 Brazil tani milion 21.1 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo [DRC] tani 14.7

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close