1. Fahamu Usiyoyajua

Mikataba ya kisheria na taratibu zake

BAADA ya kuangalia mwenendo wa mashauri ya jinai kwa kina, sasa tugeukie kwenye suala la mikataba, ingawa ikionekana iko haja ya kuyatolea ufafanuzi baadhi ya masuala kwenye mada kuhusu mashauri ya jinai, basi nitarudi kufanya hivyo.

Hakuna shaka kwamba watu wengi hupoteza haki zao kwa kutoelewa sheria mbalimbali, ikiwemo katika eneo hili `la mikataba.

Utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na hata za kijamii bila ya kufuata misingi na taratibu za kisheria imekuwa ni chanzo cha vilio na majonzi kwa walio wengi. Watu wengi huingia katika makubaliano mbalimbali bila ya kujitathmini, na hatimaye huja kushtuka baada ya kutokea hasara au dhuluma.

Ni wazi kwamba, asilimia kubwa ya Watanzania hawaelewi kuhusu maswala ya mkataba hususan lengo kuu la mkataba na ndiyo maana mtu hatimaye hujikuta na madeni asiyoyatarajia.

Katika makala haya, nimeona ni vema tuelimishane juu ya mambo anuwai yahusuyo mkataba kwani maisha ya sasa yanawalazimu watu wengi kuendea shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuingia katika mikataba.

Maana ya mkataba

Mkataba ni makubaliano yenye nguvu kisheria. Makubaliano hayo lazima yawe kati ya pande mbili tofauti na pia yafuate misingi ya sheria za nchi. Pia, ni muhimu kusiwe na kulazimishwa kwa upande wowote ule wa walioingia mkataba .

Hii ni kusema kuwa, mikataba yote ni makubaliano lakini siyo makubaliano yote ni mikataba. Kwa maana hiyo, ingawaje watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya mkataba na makubaliano, lakini kuna tofauti kubwa kati viwili hivi.

Ili kujiridhisha kuwa makubaliano baina yenu ni mkataba wa kisheria, lazima muhakikishe kuwa yamekidhi vigezo vyote vya kuwa mkataba halali. Katika muendelezo wa makala haya, hapo baadae, tutakuja kuangalia vigezo vinavyofanya makubaliano kuwa na nguvu kisheria mpaka kufikia hatua ya kuitwa mkataba.

Kimsingi, mkataba unaweza kuwa wa maandishi, mdomo au wa vitendo.

Mkataba wa maandishi

Mkataba wa maandishi ni makubaliano yanayofikiwa kwa kuwekwa katika maandishi. Katika aina hii ya mkataba, pande mbili zinazoingia katika mkataba huandika makubaliano yao ndani ya karatasi maalumu kwa lugha yenye kueleweke baina yao, huku kila mmoja baina yao akiweka saini makubaliano hayo kuonesha kuwa kile kilichoandikwa wamekubaliana nacho kwa pamoja.

Huu ndiyo mkataba ambao unasisitizwa sana kwa sababu linapokuja kutokea suala la kutolea ushahidi mahakamani juu ya makubalino fulani, inakuwa ni rahisi kuleta yanapoletwa maandishi.

Ikiwa kama wanatumia mkataba wa maandishi, ni vyema kwa pande zote za mkataba, yaani mtoa pendekezo (offerer) na mpokea pendekezo (offerree), kuhakikisha kuwa mambo yote ya msingi yahusuyo makubaliano yao yameandikwa. Pia, kanuni za kiuandishi ni sharti zizingatiwe ili kuondoa utata unaoweza kujitokeza mbeleni kwenye tafsiri ya mkataba huo.

Mkataba wa mdomo

Mkataba wa mdomo ni ule ambao pande mbili zinazoingia makubaliano zinafanya hivyo kwa kupitia maneno tu.

Kwa mfano, unapokwenda dukani kununua bidhaa fulani huwa hakuna maandishi yanayotumika baina ya muuzaji na mnunuzi, bali mnakubaliana kwa njia ya mdomo tu.

Mkataba wa vitendo

Mkataba wa vitendo ni mkataba a m b a o unaoweza kufungwa kutokana tu na matendo ya wahusika wa mkataba huo.

Kwa mfano msambazaji wa mchele wa jumla anaweza kuwa na kawaida ya kuleta gunia kadhaa za mchele na kumwachia muuzaji, kisha muuzaji akimaliza kuuza anamlipa yule msambazaji.

Ingawaje hawakuandikishiana popote, makubaliano haya yatakuwa na nguvu kisheria. Mkataba huu ndiyo tunauita kuwa ni wa vitendo (implied contract).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close