1. Fahamu Usiyoyajua

LAMPROLOGOUS LETHOPS: Samaki asiyeona aishiye katika maji ya kina kirefu

Shukurani zote ni kwa Allah Mtukufu aliyeumba kila kitu, na rehema na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja na Ahli zake na Maswahaba wake na kila aliyeongoka mpaka siku ya Malipo.

Kwa hakika, hakuna shaka juu ya uwepo wa Allah Mtukufu. Dalili za uwepo wake zinapatikana katika uumbaji wake wa viumbe vyake tunavyoviona na tusivyoviona. Kwa hakika, kila kiumbe ni dalili ya uwepo wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.

Ni kwa faida yako ikiwa utakuwa ni mtu mwenye kutafakari juu ya uwepo wa Allah Mbora wa uumbaji na nguvu, dalili na maamuzi yake. Kutambua kuweko wa Mwenyezi Mungu ni njia mojawapo ya kuleta khushui na unyenyekevu katika ibada zetu mbalimbali, kwani yeye ni Mmoja Aliyetukuka wa Pekee kabisa, hakuna mwingine kama Yeye.

Kupitia viumbe vyake tunavyovisoma kuna mazingatio makubwa kama tutamakinika. Juma hili Acha tukaone ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwa kumtazama mmoja wa viumbe wake, samaki anayefahamika kama ‘Lamprologous Lethops’ kwa lugha ya kigeni.

Lamprologous Lethops ni samaki asiyeona, aliye katika kundi la jamii ya Cichild. Samaki huyu anapatikana katika maji yanayokwenda kwa kasi katika Mto Congo. Mtaalamu mmoja wa elimu ya viumbe anasema, aina hii ya samaki inaaminika wanaishi kwenye maji ya kina kirefu sana cha takriban mita 160 (sawa na kama futi 520).

Urefu wa samaki huyo ni sentimita 10 (sawa na kama inchi 4), hata hivyo madume yake ni wakubwa kidogo kuliko majike. Kimuonekano Allah Mbora wa kuumba, hajawajaalia kuwa na rangi. Badala yake, samaki hawa ni weupe, kwa namna walivyo wanaonekana kama Albino kwa kiasi fulani.

Samaki hawa pia wamejaaliwa kuwa na kichwa kikubwa na mkia wao ni mfupi. Juu ya mwili wake, samaki huyu ana miba miba. Kama tulivyosema, samaki huyu haoni ingawa ana macho.

Wataalamu wanasema, kuna ngozi nene juu ya macho yao inayopelekea kuzibwa kwa macho, na hivyo kuwasababishia kutoona; nayo ndiyo mipango ya Mwenyezi Mungu Mbora wa Uumbaji. Hata hivyo, ajabu ni kuwa, kwa utukufu wa Mola Muumba wa mbingu, nchi na vilivyomo baina ya viwili hivyo, licha ya kutoona, samaki huyu anapata riziki yake.

Ndugu yangu msomaji samaki huyu hajagunduliwa siku nyingi. Kwa mara ya kwanza, waligunduliwa na wavuvi wenyeji wa huko katika nchi ya Kongo baada ya kuvuliwa kutoka katika kina kirefu na kuwaleta juu. Hata hivyo, samaki hawa walipoletwa juu katika kina kifupi walikufa kwa sababu ya kushindwa kuhimili presha/msukumo wa maji ya juu ambayo ni tofauti na walipozoea kuishi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close