1. Fahamu Usiyoyajua

Lama Glama: Ngamia wa Amerika ya Kusini

Katika makala yetu ya leo katika safu hii inayojadili maisha na tabia za viumbe mbalimbali wa Allah tutazungumzia mnyama anayefahamika kwa jina la lama glama anayefanana mno na ngamia. Hata wataalamu wamethibitisha kuwa mnyama huyu ni jamii moja na ngamia (camelid)

Lama glama ni mnyama wa kufugwa anayepatikana Amerika ya Kusini zaidi katika nchi za Peru na Chile na hususan katika miinuko isiyo zaidi ya mita 4,000 juu ya usawa wa bahari. Maeneo maarufu wanapopatikana ni pembezoni mwa milima ya Andes. Lama glama kamwe huwezi kuwakuta porini.

Wakazi wa asili wa nchi za Argentina, Ecuador, Chile, Bolivia na Peru hupenda kuwahifadhi na kuwatumia wanyama hawa wa kufugwa kwa shughuli mbalimbali.

Pia, kibiashara, lama glama wanaweza kupatikana sehemu nyingi duniani ikiwemo nchi nyingi za Amerika ya Kaskazini na Ulaya sambamba na taifa la Australia. Allah, Mbora wa Uumbaji, amemjaalia lama glama urefu wa mita 1.7 hadi 1.8 na Uzito wa kilogramu 130 hadi 170. Pia, wanyama hawa wana manyonya mengi mwilini na shingo ndefu mithili ya ngamia, ingawa wao hawana nundu.

Chakula na Uzazi

Kwanza ijulikane kuwa lama grama ni wanyama wapendao kuishi kijamii kwa hiyo mara nyingi utawakuta kwenye makundi.

Kama ilivyo kwa ng’ombe, lama glama hupendelea kula nyasi na mimea mingine (herbivorous). Aina wanazokula za mimea ni nyingi mno. Pia, lama glama wana kawaida ya kurejeshea chakula chao (kucheua) na kutafuna kwa mara nyingine.

Katika uzazi, lama glama hubeba mimba na kunyonyesha. Mimba yao huchukua takriban siku 360, yaani wastani wa mwaka mzima. Mara nyingi jike huzaa mtoto mmoja karibu kila mara.

Lama Glama wakizaliwa huwa na uzito wa kilo 10 na wanaweza kukimbia karibu saa moja baada ya kuzaliwa. Mama hunyonyesha watoto kwa miezi minne.

Mambo 10 usiyoyajua kuhusu Lama Glama

  • Wenyeji wa Amerika ya Kusini wanamtumia lama grama kuwabebea mizigo, ila siyo mizito sana.
  • Tofauti na wanyama wengine, wanapokutana aina ya lama grama dume na jike hulala chini. Pia, kitendo chao huchukua kati ya dakika 20 hadi 45.
  • Lama glama wana tabia ya kuwatemea watu mate lakini wakifundishwa wanaacha.
  • Lama Glama wanazaa huku wamesimama. Ajabu zaidi ni kuwa jike linapozaa wenzake humzunguka na kumlinda
  • Lama glama wanafugwa zaidi kwa ajili ya ngozi yao na manyoya yao kwa ajili ya kutengenezea bidhaa za viwandani. Mfano, manyoya yao hutumika zaidi kutengeneza kamba na vitambaa.
  • Lama glama iwapo watabebeshwa mizigo mikubwa hukataa kwenda. Wakati mwingine huweza hata kumpiga mateke anayemmliki hadi mzigo upunguzwe.
  • Lama glama wana kiwango cha juu kuliko kawaida cha hemoglobini katika damu yao na pia huwa na mwili myembamba wenye umbo la mviringo. Inatajwa kuwa hali hizi zinatokana na kuishi katika mazingira oksijeni duni.
  • Lama glama hupendelea zaidi kuzaa wakati wa asubuhi kuanzia saa mbili hadi saa tisa ili kukwepa hali baridi ya usiku inayoweza kuleta athari kwa mtoto anayezaliwa.
  • Lama glama jike ndiye anayewajibika kumlea mtoto na hufanya hivyo hadi mtoto afikishe mwaka mmoja. Lama glama wana uwezo wa kunywa maji lita mbili hadi tatu kwa siku.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close