1. Fahamu Usiyoyajua

Kunguni: Bila damu hana maisha

Uhai hauwezi kuwa ulitokea tu,  bali yupo aliyeuleta; na huyo aliyeuleta, Mwenyezi Mungu, Muumba ameuleta uhai kwa mpango, hekima na makusudi maalumu.

Katika safu yetu hii inayolenga kuimarisha msimamo wako juu ya  uwepo wa Allah Aliyetukuka kupitia maajabu ya uumbaji wake, leo tunamuangazia mdudu kunguni.

Kunguni ni katika wadudu wenye maajabu sana. Mdudu huyu haruki, bali hutambaa. Ni mdudu mdogo aliyejaaliwa miguu sita, kulia mitatu na kushoto mitatu. Mdudu kunguni huishi kwa kutegemea damu, kama chakula chake na ndio maana ni adui mkubwa wa binadamu kutokana na usumbufu wake.

Kunguni wapo wa aina nyingi, mfano wapo wanaouma popo tu na wapo wanaowauma binadamu. Kunguni walikuwepo enzi na enzi lakini mwaka 1940 walimalizwa katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani na Nchi za Ulaya.

Mwaka 1995, walirudi tena upya kwa sababu tatu. Mosi, inasemakena dawa za kuwaua ziliwatengenezea usugu na  hivyo kukosa nguvu tena ya kuwaangamiza. Pili, serikali ya nchi hizo zilipiga marufuku dawa za kuwaua kwa sabahu zilithibitika kuleta madhara kwa binadamu. Tatu, hawa ni wadudu walioweza kusafiri kwa urahisi kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Uzazi

Katika uzazi, kunguni wanapitia  hatua maalumu hadi kuwa kunguni kamili au aliyekomaa. Kwanza anataga yai, kila siku kuanzia yai moja hadi matano hivi. Baada ya yai anakuwa ‘nyimphi’ mdogo mwenye milimita 1.5, kisha nyimphi huyo hukua hatua kwa hatua hadi anafikia kuwa kunguni kamili.

Makazi yao

Kunguni wanapenda kuishi sehemu zenye joto, lakini pia wanapenda kukaa kwenye kona za vitanda, makochi na magodoro, hasa yale ambayo hayana kava.

Kuwagundua na kuwaangamiza

Ndugu yangu msomaji, kuwaona wadudu hawa kwa macho ndio uthibitisho kuwa wamekutembelea. Ama kuhusu njia za kuwaangamiza, kuna njia kadha.

Kwanza, unaweza, kuchemsha maji ya moto na kumwagia maeneo yote ya chumba/nyumba ikiwemo kwenye vitanda, na magodoro, na kisha uyavalishe kava.

Njia ya pili ni kutumia dawa za kuwaua  ingawa nyingi zimekuwa sugu. Kwa usalama zaidi, ni bora upate ushauri wa wataalamu juu ya dawa gani ni mujarabu kwani na nyingine zinasababisha maradhi.

Usiyoyajua kuhusu kunguni

Kunguni wanachangamka sana usiku kuliko mchana. Kunguni ni tofauti na mchwa au kiroboto ambao wakikuuma wanaweza kukuletea madhara makubwa.

Kunguni wao hawana madhara zaidi ya kisaikolojia, aleji, kusisimkwa ukiwaona, kuwashwa mwili na hata upele.

Wataalamu wameshindwa kujua utaalamu/ ufundi anaoutumia kunguni kumnyonya binadamu kwani huwa hatuhisi chochote, yaani ni kama vile wanatudunga ganzi.

Kunguni jike hana ‘jinsia’ ila dume anayo namna anayopandana na jike kwa kutoboa sehemu ya mwili wa jike na kumwaga mbegu zinazokwenda kuzalisha.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close