1. Fahamu Usiyoyajua

Kuku: Ndege waliowazidi idadi wanadamu

Ndugu yangu msomaji, juma hili nakuletea dondoo kuhusu ndege maarufu aina ya kuku – kuku huyuhuyu ambaye tunamla kila siku majumbani.

Binadamu wengi hufuga kuku. Kuku ni ndege aliyeanza kufugwa kwa karne nyingi huko nyuma. Kuku anatajwa kama aina ya ndege ambao wameenea kwa wingi sana duniani kuliko ndege wa aina yoyote nyingine.

Ndege huyu hufugwa kwa sababu mbalimbali kulingana na matakwa ya mfugaji. Wapo wanaofuga kwa ajili ya kupata nyama na wengine kwa ajili ya mayai. Pia wapo wanaoufuga kwa ajili ya matumizi ya nyumbani tu na wapo wanaofuga kwa ajili ya biashara ya reja reja au jumla.

Katika mazingira ya asilia, kuku huishi miaka mitano hadi 11 lakini wale wanaofugwa wanachinjwa baada ya wiki sita mpaka nane (kwa kuku wa nyama) na baada ya mwaka mmoja (kama ni kuku wa mayai).

Kiujumla ndugu yangu msomaji, kuku ni katika ndege mwenye faida kubwa sana kwa mwanadamu na kwa viumbe vinginevyo. Kuku hutaga mayai ambayo hutumika kama chakula kwa wanadamu na viumbe vingine.

Wengi wanaoshindwa kupata faida katika biashara ya ufugaji wa kuku ni kwa sababu hawajui njia sahihi za ufugaji wa kuku. Wanaojua njia sahihi za ufugaji wa ndege huyu hufaidika sana.

Kuku dume huitwa ‘jogoo’, jike ni ‘tembe’ na mtoto wa kuku ni kifaranga. Jogoo ana muonekano tofauti na tembe. Jogoo anakuwa ni mrefu zaidi kwa kwenda juu kuliko jike na amejaaliwa kuwa na kilemba juu ya kichwa chake.

Kuna aina mbalimbali za kuku. Wapo wale kuku ‘vibete’ ambao ni wafupi sana na kuna ‘kuchi’ ambao ni warefu sana na wenye shingo iliyoenda juu. Halafu kuna hawa wa kawaida.

Uzazi

Kuku hutaga mayai mpaka yanapoisha kwenye mfuko wake, kisha huanza kuatamia. Anapotaga mayai hutulia kwenye kiota chake bila ya kutembea wala kula. Kazi kubwa atakayoifanya wakati huo ni kugeuzageuza mayai yake tu.

Kuku hutumia wastani wa siku 21 mpaka kumaliza kuangua mayai. Mayai huanza kukomaa mara tu baada ya kuanza kutamiwa. Wakati wa kuanguliwa, kuku husaidia kuvunja mayai taratibu na kuwasaidia vifaranga kutoka.

Kuku kwa kawaida, hukaa kwenye kiota kwa siku mbili baada ya kuangua mayai yake. Mayai yote ambayo hayakurutubishwa na jogoo, hayataanguliwa.

Chakula

Kwa upande wa chakula, kuku mara nyingi hupenda kula mbegu, wadudu na hata wanyama wakubwa kama vile mijusi, nge wadogo na kadhalika. Kuku wa kufugwa mara nyingi hupewa pumba, chakula ambacho wanakipenda sana.

Mambo 10 usiyoyafahamu kuhusu kuku

  • Husemwa kuwa rangi ya mayai ya kuku yanategemea rangi ya masikio yake. Kuku mwenye masikio mekundu, hutaga mayai ya kahawia (brown) na kuku mwenye masikio meupe hutaga mayai meupe.
  • Ikiwa mchinjaji hatomzuia kuku wakati akitemtenganisha kiwiliwili na kichwa, anaweza kurukaruka umbali wa ukubwa wa uwanja wa mpira. Kuku hujisafisha kwa kutumia vumbi. Huchimba shimo dogo na kujigeuza geuza kwenye vumbi la shimo hilo hadi watakaporidhika, kisha hutoka na kujikung’uta.
  • Wataalamu husema kuwa, mwili wa kuku una asilimia 15 ya maji zaidi ya mwili wa binadamu.
  • Njia ya kipekee ya kuwasiliana kwa kuku ni milio. Kuku wana milio zaidi ya 30.
  • Jogoo anapopata chakula huwaita kuku wengine na kuwapa fursa ya kula kwanza.
  • Kuku jike wana maisha ya ajabu wanapokuwa na vifaranga vyao. Kuku huwapenda vifaranga vyao mno kiasi kwamba huwa wakali kuvilinda vifaranga dhidi ya maadui kwa kuwafunika na kuwasaidia kuwapa joto.
  • Kuku-jike huwaongoza vifaranga na kuwaita kwenye chakula na maji na mara nyingine huwalisha moja kwa moja. Baada ya kukaa na vifaranga vyao kwa wiki kadhaa, kuku- jike hupoteza hamu hamu nao na kuanza kutaga tena.
  • Kuna idadi kubwa ya kuku duniani kuliko idadi ya binadamu. Kuku wanakadiriwa kufikia bilioni 25. Pia, kuku ndiyo ndege wengi zaidi duniani katika kundi ya kisayansi la familia ya ndege.
  • Kuku tetea anayeatamia hugeuza mayai yake mara 50 kwa siku na ana uwezo wa kuatamia mayai 300 kwa mwaka.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close