1. Fahamu Usiyoyajua

KIROBOTO: mdudu anayeishi kwa kufyonza damu

Shukurani zote ni kwa Allah Mtukufu aliyeumba kila kitu, na rehma na amani zimuendee Mtume wetu Muhammad pamoja na Ahali zake na Maswahaba zake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka Siku ya Malipo.

Kwa hakika, hakuna shaka juu ya kuwepo kwa Allah Aliyetukuka. Dalili ya uwepo wake ni uumbaji wake unaothibitika kupitia viumbe tunavyoviona na tusivyoviona. Kila kiumbe kilichopo ni dalili ya uwepo wa Muumbaji ambaye ni Allah Aliyetukuka.

Ni kwa faida yako ndugu yangu msomaji iwapo utakuwa una tafakari uwepo kwa Allah, Mbora wa uumbaji na nguvu zake, dalili na maamuzi yake kuhusiana na maisha haya na yale yajayo.

Kutambua kuweko Kwake ni njia mojawapo ya kuleta khushui kwenye moyo wako na kujinyenyekeza katika ibada zetu kwake Muumba Aliyetukuka, Mmoja na wa Pekee kabisa. Hakuna mwingine kama Yeye.

Juma hili Acha tukaone ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwa kumtazama mdudu kiroboto. Kiroboto ni katika jamii ya wadudu wasiyo na mbawa, kama ilivyo kwa chawa. Allah amewajaalia wadudu hawa kutembea kwa kurukaruka.

Wataalamu wanasema, kiroboto anaweza kuruka mara 50 umbali wa umbo lake, huku mwenyewe akiwa na urefu wa milimita tatu. Kwa urefu huo, ina maana kiroboto ni mdudu mdogo sana, labda kama sisiminzi.

Kiroboto ni katika wadudu ambao wanaishi kwa kunyonya damu za wanyama, ndege na hata binadamu. Mdudu huyu ana rangi ya kahawia (brown). ingawa ni mdogo lakini kucha zake zina nguvu sana ili kumfanya anapomnata mnyama au binadamu, asianguke.

Mdomo wa kunguni una sehemu maalumu ya kutobolea mnyama na kunyonya da mu na tena anafanya tukio hilo kwa haraka sana. Kama miondoko ya mdudu huyu ni ya kurukaruka, ila hawezi kupaa. Wataalamu wanasema, kuna aina takriban 2, 500 za viroboto wanaopatikana karibu maeneo yote ya dunia isipokuwa zile sehemu zenye baridi kali. Kiroboto anapatikana pia kwa wanyama fulani maalum kama tembo, popo. Hata hivyo wale wanaoishi na panya na binadamu ndiyo wanatuhusu sisi.

Uzazi

Katika uzazi, Allah amepanga hatua maalumu ambazo mdudu huyu anapitia katika uzazi wake. Kwanza anataga mayai, ambayo kisha yanabadilika kuwa kiwavi (kama funza). Anapofika hatua hiyo ya pili, anakula kwa bidii sana. Baada ya hapo, anabadilika na kuwa pupa, ambapo katika hatua hii huwa hali kitu. Mwishowe pupa anabadilika na kuwa kiroboto.

Ndugu yangu msomaji, sio kwamba kiroboto anaendesha mabadiliko haya yeye mwenyewe kwa matakwa yake, bali taratibu hizi ni katika uumbaji wa Allah.

Mambo muhimu kuhusu Kiroboto

Kitu ambacho wengi tunakosea ni kuamini kiroboto analeta maradhi. Mdudu huyu haleti maradhi. Maradhi yanaletwa na Allah, muangalizi wa viumbe vyote. Kiroboto ni, kama mbu na nzi, ni msambazaji tu (vector).

Kiroboto hubeba vimelea fulani vya bacteria vinavyoitwa ‘Yasernia pestis’kutoka kwa panya na kuvileta kwa binadamu. Hivyo ni muhimu pia kuelewa kuwa panya hawaleti ugonjwa wa tauni bali kiroboto ndiyo anasambaza kutoka kwa panya hadi kwa binadamu.

Mwaka 1346 hadi 1353 kulizuka ugonjwa uliosambazwa na kiroboto kutoka kwa panya na kusambaa karibu maeneo mengi ya dunia – ukianzia Asia ya Kati, hadi China hadi Ulaya hususan katika nchi za Urusi, Uingereza.

Inakisiwa kuwa karibu watu kati ya milioni 75 hadi 200 walikufa. Hakuna ugonjwa uliowahi kupoteza maisha ya idadi kubwa ya watu kama huo. Wakati huo hakukuwa na dawa na hata madaktari walishindwa kutambua chanzo cha ugonjwa huo. Tunashukuru Mwenyezi Mungu ugonjwa huo kwa sasa unatibika.

Namna ya kuwaepuka viroboto

Hakikisha nyumba inakuwa safi. Epuka mavi ya panya. Pia, jaribu kutolala chini kwani wadudu hawa hawana mbawa. Tumia dawa za kuwaua ila pia ni muhimu dawa unayotumia iwe rafiki kwa binadamu. Kwa maelezo zaidi ya namna ya kupambana nao, wasiliana na wataalamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close