1. Fahamu Usiyoyajua

Kaboko: Nyoka mrefu, mwenye sumu kali kutoka Afrika

Ndugu yangu msomaji, dunia ya Muumba wetu (Allah), mbora wa uumbaji, ina mapambo mengi. Ukiachilia mbali milima, bahari, mito, maziwa, majangwa; pia kuna wadudu na wanyama wa aina nyingi. Wanyama hawa ni hisani kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi kwa ajili yetu sisi wanadamu

Ninapozungumzia tabia za wadudu, wanyama na viumbe wengine; nauona ukubwa na uwezo wa Muumbaji katika fikra zangu. Katika makala hii ya ‘Fahamu Usiyoyajua’ leo tutamzungumzia nyoka aitwae koboko. Koboko ni miongoni mwa nyoka hatari zaidi duniani. Koboko wanapendelea kuishi katika mabwawa, milima mirefu, misitu, sehemu zenye hali ya hewa ya joto na unyevunyevu, maeneo yenye miamba na ukanda wa savanna. Meno ya mbele ya koboko yanafanana sana na meno ya kobra.

Koboko ni miongoni mwa nyoka warefu zaidi wanaopatikana barani Afrika. Uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa shughuli za kilimo kumewafanya binadamu kukutana na nyoka hawa mara kwa mara.

Nyoka hawa wanapatikana kwa wingi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania, Sudan, Eritrea, Somalia, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Namibia, Msumbiji, Angola, Malawi na nyinginezo.

Mtaalamu mmoja kutoka nchini Ujerumani, Albert Gunther, ambaye ni miongoni mwa watu wa kwanza kumuelezea koboko anasema, koboko mkubwa anaweza kufikia urefu wa mita 2 hadi 3. Hata hivyo, kumbukumbu zinaonesha kuwa, koboko mkubwa na mrefu zaidi kuwahi kuonekana alikuwa na urefu wa mita 4.5. Kimaumbile, koboko wako wa aina nyingi, hali inayowafanya kutofautiana kimaumbo, tabia, mazingira ya kuishi na umri pia. Wapo koboko wenye rangi ya kijivu, weusi na kahawia ya giza.

Kwa hapa Tanzania, inasemekana nyoka hawa wanapatikana kwa wingi katika mkoa wa Tabora na wilaya ya Manyoni mkoani Singida, ingawa pia wanapatikana maeneo mengine ya Tanzania.

Uzazi na chakula

Mwezi Aprili hadi Juni ndio kipindi ambacho koboko hukutana kwa ajili ya kupandana. Ili kukubalika na majike, madume ya koboko hupambana kwanza na atakayeshinda anamchukua jike. Jike la koboko linapokuwa tayari hunyanyua mkia wake na dume akiona hivyo humpanda jike. Kupandana kwa nyoka hawa kunaweza kuchukua hadi masaa mawili.

Dume linapoanza kutoa mbegu hutetemeka na kukosa nguvu. Baada ya hapo jike anaweza kutaga mayai kuanzia 6 hadi 17 kutegemeana na hali ya hewa katika eneo husika.

Makinda ya koboko yanaweza kukua hadi kufikia urefu wa sentimita 40, 60 hadi mita 2 baada ya kutimiza mwaka mmoja. Wastani wa umri wa kuishi wa koboko ni miaka 11 au zaidi.

Koboko wanapendelea zaidi kula panya, ndege wadogo na mara chache hula nyoka wenzao.

 Mambo 10 usiyoyafahamu kuhusu koboko

  • Koboko ana uwezo wa kukugonga kwa kasi ya ajabu akiwa mbali.
  • Sumu ya koboko inapoingia mwilini huharibu chembe hai za mwili na kusababisha maumivu makali. Endapo mtu aliyegongwa na koboko hatapatiwa tiba mapema anaweza kufa.
  • Inasemekana kuwa koboko ndiye nyoka mwenye kasi zaidi kuliko wote. Nyoka huyu anaweza kutambaa kwa kasi ya kilomita 11 kwa saa iwe kwenye mchanga au nyasi.
  • Mdomo wa koboko kwa ndani ni mweusi tii na ndio maana jina lake la asili anaitwa ‘Black mamba’.
  • Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa koboko ni wa haraka na ndio maana humchukua masaa 8 hadi 10 kulainisha kiumbe alichokimeza.
  • Licha ya kuwa na sumu kali, Allah Aliyetukuka amewajaalia nyoka hawa huruma pale wanapomuona binadamu. Aghalabu koboko hukimbia anapomuona binadamu isipokuwa kwa mtu aliyedhamiria kumdhuru.
  • Koboko wanaweza kuishi na kushirikiana na nyoka wengine kama Egyptian cobra na wengineo.
  • Ni nyoka mwenye uwezo wa kuinua nusu ya mwili wake na kumgonga mtu aliyesimama au aliyekaa sehemu ya juu.
  • Koboko hapendi kusogelewa na binadamu kwa umbali wa mita 40.
  •  Muda mfupi baada ya kutotolewa, makinda ya koboko hutengeneza sumu kali inayoweza kumuua mtu ndani ya muda mfupi endapo atachelewa kupatiwa matibabu.
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close