1. Fahamu Usiyoyajua

JONGOO: Ana miguu mingi, hana macho

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ndiye pekee anayestahiki kuabudiwa. Yeye ndiye Muumba wa mbingu, ardhi, Jua, Mwezi, viumbe hai waliyo mbinguni, ardhini na baharini na kila kitu unachokijua.

Pia, ni Yeye M w e n y e z i Mungu ndiye anayeruzuku viumbe wote na katika hilo kuna dalili na ishara ya kuwa Allah peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa.

Katika Qur’an zipo Aya nyingi zinazozungumzia suala la kuamini uwepo wa Mwenyezi Mungu. Ukiacha Aya, zinaweza kuonekana wazi alama za uwepo wa Mwenyezi Mungu kupitia viumbe vyake mbalimbali, kwa maana hakuna namna ya kuwepo kwa viumbe hivi bila ya kuwepo aliyeviumba.

Hebu leo tumuangalie jongoo, ambaye ni katika viumbe wanaojulikana sana lakini hatajwi mara kwa mara, labda ni kwa sababu hana kawaida ya kuuma watu.

Jongoo yupo katika kundi moja na mdudu tandu, ambaye kitaalamu anaitwa ‘athropods. ’Jongoo wapo wa rangi tofauti tofauti – wekundu, weusi, kahawia – lakini wengi waliopo Tanzania ni weusi.

Jongoo hupatikana karibu maeneo yote ya dunia isipokuwa kwenye baridi kali. Wadudu hawa hupenda kuishi sehemu zenye mapori, kwenye udongo wenye rutuba na sehemu zenye majimaji (mvua).

Kimuonekano, viumbe hawa wana miguu mingi lakini hawana macho. Kinachowasaidia ni antena fulani iliyopo mbele ya miili yao, kama aliyonayo tandu. Tofauti ya antena za wadudu hawa wawili ni kuwa ile ya jongoo ni ndefu zaidi ya ile ya tandu.

Mwili wa jongoo umegawanyika vipande vipande; huku kila kipande kikiwa na jozi mbili za miguu. Maumbile yao yanaanzia milimita mbili hadi sentimita 35. Miili yao kwa juu kuna duara, na chini ni bapa. Wataalamu wanasema kuna aina hadi 12, 000 za jongoo.

CHAKULA

Jongoo wanakula majani yaliyooza. Baadhi wananyonya maji maji ya mimea (detrivorous). Pia, wapo wengine wanaokula vijidudu vidogo vidogo na viwavi. Ukiacha hao, wapo pia wanaokula majani na maua.

UZAZI

Katika kuzaana, jongoo jike na dume hukutana; na kisha jike hutaga mayai kati ya 10 hadi 300 kwa wakati mmoja kutegemeana na aina ya jongoo. Kuna aina ya jongoo ambao huweka mayai yao kwenye udongo na kuyaacha hapo, lakini wengine hubaki na kulinda mayai yao.

MAMBO 9 USIYOYAJUA KUHUSU JONGOO

  • Licha ya kuwa na miguu mingi, ukweli ni kwamba miguu hiyo huota baadae. Jongoo anapozaliwa huwa na jozi tatu tu za miguu na upande wa nyuma huwa hana miguu kabisa. Kama tulivyosema, miguu huota baadae ingawa kipande cha mwisho kabisa cha mwili wake kinakuwa hakina miguu hata jongoo akiwa mkubwa.
  • Jongoo wanapenda na wanaweza kuishi chini ya udongo kwa muda mrefu tu bila kudhurika.
  • Urefu wa moyo wa jongoo ni sawa na urefu wa mwili wake. Sehemu ya kutolea uchafu ya jongoo ipo kati ya tumbo lake, ambako kuna tundu nne.
  • Tezi za mate za jongoo zina tundu nne na tezi hizo ni kwa ajili ya kumeng’enya chakula chake.
  • Kinyesi cha jongoo kinarutubisha sana udongo, ingawa zipo aina chache za jongoo ambao wanaharibu mazao.
  • Jongoo hawaumi na hata zile kemikali zao wanazotoa huwa hazina madhara makubwa kwa binadamu, zaidi ya mara chache kubadilisha rangi ya ngozi. Hata hivyo, wapo baadhi ya jongoo ambao wanaweza kusababisha malengelenge, kubabuka ngozi na hata muwasho.
  • Wapo aina ya jongoo ambao wanaishi katika shimo moja na sungusungu na kamwe hawagombani ila wanategemeana.
  • Allah amewapa mbinu za kujilinda na maadui zao kwa namna mbili. Kwanza, pembeni ya miili yao kuna matundu maalumu ambayo yanatoa aina ya kemikali yenye harufu mbaya kiasi ambacho viumbe wakisikia hawawasogelei. Kiumbe pekee anayeweza kumla jongoo, hata akitoa harufu yake mbaya kujihami ni mnyama anayefanana na nguchiro aitwaye ‘meerket. ’

Namna nyingine ya kujihami ni kujizungusha (coiling). Akiwa katika hali hiyo, baadhi ya viumbe wanapata shida sana kumla na kwa hivyo kumpa ulinzi. Ni kwamba, adui zao wengi, wanaotaka kula jongoo, wamezoea kula viumbe vikiwa virefu na si duara.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close