1. Fahamu Usiyoyajua

Farasi: Ana jicho kubwa kuliko wanyama wote wa ardhini

Farasi ni mnyama wa fahari sana wa kufugwa, anayekula majani chakula kama chakula chake kikuu, sambamba na matunda kama karoti na tufaha. Farasi pia hupenda sana viazi mviringo.

Farasi hubeba mimba kwa miezi 11 mpaka 12. Wakati wa kuzaa, mtoto hutanguliza miguu kisha kichwa. Farasi huhitaji msaada sana wakati wa kuzaa kwani hupata maumivu yanayomfanya tumbo lake liteteme huku akilia kwa uchungu. Hata hivyo, muda mfupi tuu baada ya kuzaa, ndama huanza kuruka ruka kwa fujo akimshukuru Mungu kwa kumleta katika ulimwengu wa tofauti na aliokuwapo awali.

Farasi ni mnyama mwenye faida kuliko wanyama wengi wanaofugwa. Mosi, nyama yake ni chakula, pili maziwa yake pia chakula. Tatu, ngozi yake ni ‘dili’ viwandani. Ukiondoa hayo, farasi ni chombo cha usafiri na ni mlinzi mzuri, kama ilivyo kwa mbwa na paka.


Farasi ni mnyama mwenye faida kuliko wanyama wengi wanaofugwa

Farasi katika ulimwengu wa sasa hutumiwa katika kutawanya maandamano, lakini zamani farasi ni mnyama aliyetumiwa sana katia medani za vita, kwa ushahidi wa vitabu vya kihistoria. Kwa mujibu wa historia, hata Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) pamoja na Maswahaba zake walitumia farasi katika mapambano dhidi ya maadui.

Farasi ni mnyama mwenye nidhamu sana. Ukimpanda, halafu ukaanguka, hawezi kuendelea na safari mpaka utapozinduka, hata kama ulizimia. Pia, farasi ni mnyama mwenye upendo kiasi kwamba hawezi kukupeleka sehemu yenye hatari. Ukiona anagoma kusonga mbele, tambua kuwa aidha kuna nyoka au hatari nyingine usiyoweza kuiona.

Macho ya farasi ni makubwa sana na yana uwezo mzuri wa kunasa matukio vyema, mbele na nyuma, na kwa umakini. Mbali na uwezo huo wa kuona vyema lakini pia farasi yupo vizuri katika kunusa. Ukiwa na farasi, hamuwezi kukamatwa kirahisi na wanyama wakali hasa wale wanaovizia kwa kujificha.

Ukiwa na farasi, unapomfunga, ukaona anapiga kelele na kuinua inua miguu kama anapasha ili atimue mbio, haraka sana mtii na mtoke eneo hilo, vinginevyo atakata kamba na kuondoka mwenyewe kisha ubaki peke yako.

Farasi hula kilo tano mpaka 12 za majani kwa siku, hutegemeana na umri pamoja na uzito wake. Wanyama pekee wanaokula nyama wanaoyeweza kumkamata kwa kumfukuza ni duma na mbwa mwitu wa kizungu (wolf). Hawa wengine akina simba, fisi – nyama yake wataishia kuisikia tuu.

Mbali na uwezo huo wa kuchanja mbuga, farasi pia hupatwa na hisia na maumivu. Ukimtendea ubaya, usichangae akidondosha machozi na akikushusha kuanzia juu mpaka chini. Hapo ujue amekudharau tuu. Wanyama hawa huuzwa ghali sana. Farasi mmoja kwa hapa kwetu hufikia hadi milioni tano na ushee.

Bei ya farasi hupangwa kutokana na rangi, siyo ukubwa. Rangi adimu ndiyo huwa ghali zaidi. Hivyo basi, nyeupe na nyeusi si rangi ghali katika kumnunua farasi, labda ziwe na mngaro wa kipekee. Allah amejaalia umri wa kuishi farasi, wakipata matunzo mazuri, hufikia hadi miaka kati ya 28 hadi 32.


farasi pia hupatwa na hisia na maumivu. Ukimtendea ubaya, usichangae akidondosha machozi na akikushusha kuanzia juu mpaka chini

MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU FARASI

Mbali ya kuwatizama viungo vyao, njia nyingine ya kujua tofauti ya jike na dume ni kuhesabu meno. Dume huwa na meno manne zaidi ya jike; 40 kwa 36.

Ni mnyama ambaye hutumika kama chanzo cha mapato: kukodishwa, kulimia nk.

Farasi ni miongoni mwa wanyama wenye kumbukumbu kali. Farasi hulala huku akiwa amesimama.

Harufu ya uke wa farasi jike ndiyo humpa dume mshawasha au hamu ya kumpanda.

Farasi ana uwezo mzuri wa kunusa na kusikia kuliko binadamu.

Jicho la farasi ni kubwa kuliko wanyama wote wa ardhini.

Farasi hawawapendi kabisa punda. Wawili hawa wakikutana, punda anaweza kufa kutokana na kipigo kikali atakachopata.

Wakati wanawake wanasuka kichwani, farasi husukwa mkiani kwa kuwa kwa kiasi kikubwa, vinyweleo vyake vimechanua.

Akikubeba, anapokimbia katika kupenyapenya sehemu za kupita, yeye hujipigia mahesabu mwili wake tu. Hivyo, ni jukumu lako kujilinda.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close